Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Shirika la Posta Tanzania na Kampuni ya usafirishaji TUTUME wametia saini ya makubaliano ya biashara ya usafirishaji wa sampuli za kibaiolojia utakaoongeza tija na hatimae mapato ndani ya shirika, serikali lakini pia kumnufaisha mwananchi kwa kupata huduma bora.
Akizungumza na waandishi wa Habari leo wakati wa utiaji saini huo, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema Ushirikiano huo ni wa manufaa kwa pande zote mbili lakini kikubwa sana ni wa manufaa kwa wananchi;
“Kwa upande wa shirika la posta Tanzania ushirikiano huu utaongeza wigo wa utoaji huduma kwa jamii kutoka kwenye huduma za kiuchumi pekee hadi za kijamii pamoja na viwango vya ubora na utoaji huduma yaani quality of service standards”
Aidha Waziri Nape amesema “Kwa upande wa serikali ushirikiano huu utasaidia kuongeza malengo yake ya kuimarisha huduma za Afya mpaka vijijini kupitia taasisi hizi mbili zinazosaini makubaliano ya ushirikiano leo”
Waziri Nape amesema kwa upande wa TUTUME, ushirikiano huo watapata nafasi ya kushiriki kuihudumia jamii kwa kuwa sehemu ya usafirishaji wa sampuli za damu kutoka katika maeneo ya kukusanyia sampuli hadi kwenye Maeneo ya kupokelea sampuli shirika la posta Tanzania litahakikisha sampuli hizo zinafikishwa zinapotakiwa kufika.
Mbali na hayo Waziri Nape amesema Shirika la posta linafanya kazi ya kuwasaidia wananchi kwa ushirikiano na kampuni ya TUTUME kwenye maeneo ya Afya ili kuongeza kasi na ufanisi pia kuwafikia wananchi wengi zaidi katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu
Nape amewataka shirika la Posta Tanzania kutumia fursa hiyo ya uwekezaji kwenye kilimo katika kusafirisha vitu mbalimbali kama mbegu;
“Serikali tumewekeza sana kwenye sekta ya kilimo, leo tunashuhudia hili ambapo linaenda kufanya mageuzi kwenye sekta ya Afya lakini ni matumaini yangu kwamba posta mtatumia fursa hii ya uwekezaji kwenye kilimo kushuhudie mashirikiano ya posta na sekta ya kilimo katika kusafirisha vitu mbalimbali ikiwemo mbegu na sampuli mbalimbali”
Pia Waziri Nape amesema Lengo la serikali ya awamu ya sita iliyopo chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kurahisisha upatikanaji huduma mbalimbali za kijamii kwa wananchi ambapo yapo maeneo mengi na jitihada mbalimbali ambazo serikali inafanya kuhakikisha wananchi wanakua na maisha bora na uhakika.
Kwa upande wake PostaMasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo amesema serikali kupitia Wizara ya Afya katika kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata huduma za Afya kwa urahisi hususani huduma za uchunguzi wa Afya zao imelipa jukumu shirika la Posta Tanzania la usafirishaji wa sampuli za maabara kutoka vituo vya Afya kwenda maabara za uchunguzi na kurejesha majibu yake baada ya uchunguzi
“Sampuli zinazosafirishwa ni sampuli zinazotokana na magonjwa ya kawaida kama vile kifua kikuu, HIV n.k, na sampuli zinazotokana na magonjwa ya mlipuko kama vile UVUKO-19 n.k”
Mbodo amesema ili kuongeza ufanisi na ubora wa usafirishaji wa sampuli hizi za maabara na majibu yake kwa wananchi waliona vyema kama posta waingie makubaliano ya ushirikiano katika usafirishaji wa sampuli na kampuni ya usafirishaji ya TUTUME ambayo imewahi kujishughulisha na usafirishaji wa sampuli hizi za maabara.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya usafirishaji TUTUME, Misana Manyama amewahakikishia wananchi kuwa fursa hiyo waliyopewa na serikali kupitia shirika la Posta wataitumia kikamilifu kwasababu wanauwezo wa kufanya kazi hiyo kwa ubora zaidi
More Stories
Mhandisi Kundo agoma kuweka jiwe la msingi mradi wa maji
Tanzania Mwenyeji wa Mkutano wa nchi zinazozalisha kahawa Afrika
Watatu mbaroni kwa tuhuma za mauaji wakigombania shamba