January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shime: Tunajiamini na tuna uwezo wa kufanya kitu kimataifa

Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KOCHA mkuu wa timu za Taifa za Wanawake za Tanzania, Bakari Shime ‘Mchawi Mweusi’ amesema michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) iliyomalizika mwishoni mwa wiki kwa timu ya Wasichana chini ya umri wa miaka 17 ‘Tanzanite Queens’ kutwaa ubingwa imewafanya kuamini kuwa wana uwezo wa kufanya mambo makubwa katika mashindano ya kimataifa.

Tanzanite ilitwaa ubingwa huo baada ya kuwafunga Zambia kwa mikwaju ya penalti 4-3 katika mchezo wa fainali uliochezwa kwenye uwanja wa Nelson Mandela Bay baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya goli 1-1.

Katika mchezo huo, Zambia walikuwa wa kwanza kupata goli lililofungwa dakika ya 19 na mshambuliaji Comfort Seleman ambaye alitumia vizuri makosa ya safu ya ulinzi ya Tanzania baada ya kuondoka na mpira kuanzia katikati ya uwanja hadi kwenye goli na kupiga shuti Tanzania na kupiga shuti ambalo lilimsinda golikipa Aisha Mrisho.

Lakini kipindi cha pili Tanzania ilisawazisha bao hilo kwa mkwaju wa penalti iliyopigwa na Koku Kipanga baada ya Aisha Masaka kuchezewa madhambi ndani ya eneo la 18 na mchezo huo kumalizika kwa sare ya goli 1-1.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ya mpira wa miguu ya wanawake wenye umri wa chini ya miaka 17 (U-17) wakiwa katika hafla iliyoandaliwa na Serikali kuwapongeza mabingwa wa michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika, (COSAFA) yaliyofanyika Afrika Kusini hivi karibuni. (Picha na Eleuteri Mangi, WHUSM)

Shime amesema kuwa, furaha yao ni kuona wamefanikiwa kuiwakilisha nchi vizuri kwani kwaoi ni jambo la kujivunia kwani wameonesha wanaweza kufanya kitu katika mashindano ya kimataifa.

Pamoja na matokeo mazuri lakini walikwenda katika mashindano hayo kuhakikisha kuwa wanajenga timu zao kwa kupata uzoefu zaidi katika mashindano ya kimataifa.

Kocha huyo amesema, yale waliyoyapata katika mashindano hayo ni muhimu zaidi kwani yataweza kutufanya kwenda katika fainali za Kombe la Mataifa Afrika kwa upande wa wanawake (AFCON) pamoja na yale ya kombe la Dunia.

Itakumbukwa kuwa Tanzania inakabiliwa na mchezo wa kuwania kufuzu kucheza Kombe la Dunia ‘African Qualifiers FIFA U 20 WWC’ dhidi ya Senegal na endapo itashinda mchezo huo itakuwa imefanikiwa kuingia raundi ya pili ambayo itakutana na mshindi kati ya Guinea Bissau na Ghana na ikifanya vizuri itaingia raundi ya tatu.

Ikiwa itaendelea kufanya vizuri basi itakuwa imefuzu kucheza Fainali za Kombe la Dunia na kuwa timu ya kwanza kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kushiriki Fainali za Dunia za Wanawake.

Tanzania ilifanikiwa kufuzu ikinga hatua hiyo baada ya kuwafunga Uganda kwa jumla ya goli 4-2 wakishinda nyumbani 2-1 na kisha kuwafunga Uganda 2-1 kwenye Uwanja wa Star Times jijini Kampala katika mchezo wa marudiano.

Kwa upande wake kocha Edna Lema ambaye ndiye aliyekuwa kocha mkuu wa Tanzanite katika mashindano hayo amesema kuwa, furaha yake ni kuona wamefanikiwa kutimiza ahadi yao kwa kurudi na kombe.

Amesema, toka ameanza kuzinoa timu za taifa huo ni ubingwa wake wa tano hivyo watahakikisha wanaendelea kutwaa makombe katika mashindano yatakayokuja mbele yao.