December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shilingi Trilioni 16 kujenga SGR awamu ya kwanza DSM -Mwanza

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma.

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania(TRC),Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa reli ya kisasa kwa awamu ya kwanza Dar es salaam hadi Mwanza wenye gharama ya Shilingi trilioni 16 umefikia hatua nzuri na mkandarasi tayari ameshalipwa kiasi cha Sh trilioni 6.4.

Pia amesema kwa kipande cha Morogoro mpaka makutupora  ujenzi  wa msongo wa kilovoti 220 ambao unaendelea una jumla  ya kilimeta  410 na mkataba wake  ni shilingi bilioni 160.2, na mpaka sasa  Wakandarasi wamelipwa  shilingi bilioni 29.4 na bilioni 48.5 Kila Moja.

Kadogosa amesema hayo jijini hapa leo na  wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya shirika hilo (TRC) 2021/22 na mikakati Kwa mwaka wa fedha 2022/23 ambapo amesema kuwa  usafiri wa treni ya kisasa unatarajiwa kuanza kati ya Januari au Februari mwaka 2023 pindi watakapokuwa wamepewa kibali na Mamlaka Udhibiti wa Usafiri Nchi Kavu (LATRA).

Pia amesema kukamilika kwa reli ya kisasa itasaidia kukuza uchumi wa Tanzania kwa kukomboa muda pamoja na kufungua milango ya uchumi kutoka nchi za Afrika Mashariki.

Vilevile Kadogosa amewatoa hofu Watanzania kuhusu kukatika kwa umeme katika usafiri wa reli ya kisasa na kubainisha kuwa treni zitakazotumia reli hiyo zinaweza kufua umeme wake na kusafiri zaidi ya dakika 48 bila umeme wa gridi ya Taifa.

Pamoja na hayo Kadogosa ameeleza kuwa TRC imelenga kutekeleza mipango ya kitaifa hususani uboreshaji na uendelezaji wa miundombinu kwa lengo la kurahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi  ikiwemo kukuza biashara ndani na nje ya Nchi.

Amesema pamoja na kuwa na  majukumu mengine pia shirika hilo kwa mwaka wa fedha  2021/22_2022/23  limejikita zaidi  katika kuongeza ufanisi wa  utendaji kazi ya shirika Kwa kujenga,kukarabati na kuboreshwa  miundombinu ya Reli  ununizi wa ukarabati na vitendea kazi .

Kadogosa amesema ili kufikia adhima,shirika litahakikisha linaboresha miundombinu ya Reli Kwa kujenga mtandao mpya  wa Reli wa kiwango Cha standard Gauge wenye jumla kilimeta 4,777 na ukarabati mtandao wa Reli iliyopo ya Meter Gauge Kwa kilimeta 2537.

Amesema ukarabati huo wa njia ambao utajumuisha kuinua uwezo wa njia  Kwa kuondoa reli nyepesi za paundi 45na 56 na kutandika Reli nzito za paundi 80,kuinua uwezo wa madaraja kutoka ekseli 13.5 kufikia  ekseli 18.5 pamoja  na kuboreshwa mfumo wa ishara na mawasiliano.

Akizungumzia  miradi mingine na amesema kuwa shirika hilo linatekeleza miradi  ya muda mfupi, muda wa kati  na mrefu ,pia muda mfupi inajumuisha  miradi ufufuaji wa njia za zamani ikiwemo  njia ya kaskazini ,miradi ya muda wa kati  inajumuisha ukarabati wa njia iliyopo ikiwemo uboreshaji wa njia ya kati ambao umefanyika kupitia  Mradi wa Tanzania Intermodal and tall Development project (TIRP) kutoka Dar es salaam hadi Isaka, Miradi ya muda mrefu ni pamoja na Mradi wa ujenzi wa Reli ya kisasa (SGR).

“Serikali inajenga mfumo wa umeme wa msongo  wa kilovoti 220 ambao unajitegemea (dedicated line) kwa ajili ya uendeshaji wa treni ili kupata umeme wa uhakika,Kwa kipande Cha Dar es salaam mpaka Morogoro mfumo huo una urefu  wa kilimeta 160 na umekamilika Kwa asilimia100,mkandarasi ameshalipwa kiasi Cha bilioni 70.6,”amesema.

Kwa Upande wake Msemaji mkuu wa Serikali Gerson Msigwa amesema ujenzi wa reli hiyo unaenda sambamba na Maboresho ya bandari zilizopo nchini kwa kuwa miundombinu hiyo ni mahsusi kwa ajili ya usafirishaji wa mizigo mizito.