Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania imewasisitiza Watanzania kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni mbalimbali kuhusu sheria ambazo wanaona zina mapungufu na zinahitaji marekebisho ili tume hiyo iweze kuzipitia na kuzifanyia tafiti kwa ajili ya kuzirekebisha kabla ya mapendekezo hayo kupelekwa Serikalini.
Katibu Mtendaji wa Tume hiyo George Mandepo, amesema hayo mara baada ya kutembelea banda la Tume hiyo katika Maonesho ya Kimataifa ya Nane Nane yanayofanyika katika Viwanja vya Nzuguni Jijini Dodoma.
Mandego amesema wajibu mkubwa wa Tume hiyo ni kupendekeza marekebisho ya sheria, kufutwa kwa sheria au kuboresha mifumo ya usimamizi wa sheria ambazo zipo Serikalini ili ziweze kutenda haki kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
“Tume kabla ya kurekebisha sheria inafanya utafiti kwa uhakika kuhusu sheria husika kwa kuangalia mazingira ya sasa na mazingira yajayo kwa sababu sheria inaishi”, Amesisitiza Mandego.
Katibu Mtendaji huyo wa Tume ya kurekebisha Sheria Tanzania amesema pamoja na Tume kufanya mapitio ya sheria na kuzirekebisha pia ina wajibu wa kuangalia iwapo sheria inayotungwa kama inaweza inaweza kuleta madhara ya kijamii, kiuchumi na kisiasa.
Amebainisha kuwa mchakato mzima wa kurekebisha sheria unashirikisha kikamilifu wadau wa sekta husika ikiwemo wananchi ili kuhakikisha sheria inayotungwa inakuwa bora kwa ajili ya maslahi ya mapana ya pande zote Mbili.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato