Na Allan Kitwe, TimesMajira Online, Tabora
BARAZA la Mashehe Mkoani Tabora limemsimamisha kazi Shehe wa Kata ya Kidatu katika Halmashauri ya Manispaa Tabora, Bakari Sikonge, kwa kukiuka maadili ya dini kwa mujibu wa katiba inayoongoza Baraza hilo.
Akitoa maamuzi hayo jana Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye ni Shekhe wa Mkoa huo Alhaj Ibrahim Mavumbi amesema kuwa mbali na kusimamishwa pia wataendelea kufuatilia mienendo yake ili kujiridhisha kama amebadilika au la.
Amebainisha kuwa baada ya kupokea malalamiko dhidi yake, aliitwa na Uongozi wa Baraza na kutakiwa kutoa maelezo ya tuhuma zinazomkabili lakini hakuzingatia kile alichoelekezwa badala yake alienda kwenye vyombo vya habari.
Shehe Mavumbi ametaja tuhuma kubwa inayomkabili kuwa ni kumfungisha ndoa mwanamke ambaye yupo kwenye ndoa nyingine kwa lengo la kunufaika na fedha kutoka kwenye taasisi moja iliyokuwa inatoa fedha kwa wanandoa wapya.
Amefafanua kuwa Shehe huyo alimhadaa Shehe Mkuu na Mufti wa Tanzania, Alhaj Abubakar Zuberi Bin Ali ambaye ndiye Kiongozi wa dini kwa kufungisha ndoa isivyo halali huku akijua kabisa kuwa ni kosa kufanya hivyo.
‘Kwa mujibu wa taratibu za Baraza la Mashehe na dini ya kiislamu hakuna ndoa juu ya ndoa, hii ni hadaa, ni ndoa feki, ingekuwa ndoa sahihi kama mwolewaji angekuwa ameachika lakini wawili hao walishaoana na wanaishi pamoja’, amesema.
Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kata anayesimamia masuala ya dini katika Kata hiyo Suleiman Salumu naye amepewa onyo kali kwa kuhusika na tukio hilo ikiwemo kuitisha vyombo vya habari ili kuzungumzia tukio hilo.
Amebainisha kuwa kitendo hicho ni kinyume na taratibu za baraza na dini, kwa kuwa masuala ya dini yote yanayofanyika katika Mkoa msemaji ni Shehe wa Mkoa au Shehe wa Wilaya na sio muumini au Kiongozi wa ngazi za chini.
Amesisitiza kuwa Baraza litaendelea kufuatilia mienendo yao na kama itabainika kuwa wana mambo mengine wanayoyafanya kinyume na maelekezo ya Baraza, hatua kali zaidi za kinidhamu zitatuchukuliwa dhidi yao.
More Stories
Jokate awapa tano vijana UVCCM maandalizi Mkutano Mkuu wa CCM
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto