February 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shaka:Uimara wa Rais Samia ni matokeo chanya unaojali kesho ya nchi

Na Mwandishi wetu Morogoro

Mkuu wa Wilaya ya Kilosa Shaka Hamdu Shaka amesema uimara wa Rais Samia Suluhu Hassan katika uongozi wake ni wenye matokeo chanya unaojali kesho ya Nchi yetu (vizazi vya leo na kesho) kwa kukamilisha mradi wa kimkakati wa SGR kutoka Dar – Morogoro – Dodoma.

Amefahamisha kuwa kukamilika kwa mradi huo kumerahisisha usafiri miongoni mwa wananchi morogoro na mikoa jirani, kumechochea biashara na shughuli nyingine za kiuchumi na kijamii.

Ameyasema hayo katika kituo cha SGR (Jakaya Mrisho Kikwete Station) wakati akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Morogoro katika uzinduzi wa Duka la 456 la. Huduma kwa wateja kupitia kampuni ya simu ya Vodacom katika kituo hicho.

‘Ufanisi wa mradi huu ni matokeo ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa Bwawa la Mwl Nyerere ambao umekamilishwa na Rais Samia. Mradi huo umetupa uhakika wa umeme kwa ajili ya uendeshaji wa mradi huu wa SGR huu ni ukumbozi mkubwa katika sekta ya usafiri na usafiri haji sambamba na upatikanaji wa nishati ya umeme kwa uhakika,”amesema

Amebainisha kuwa watanzania katika wameendelea kushuhudia mapinduzi makubwa katika sekta ya mawasiliano ya simu na intaneti nchini ambapo serikali ya Rais Samia imeendelea kujenga mazingira rafiki na wezeshi kwa makampuni ya mawasiliano kama Vodacom na wengine kuwekeza na kutoa huduma kwa wananchi kwa ufanisi.

“Tusione vyaelea vimeundwa na muundaji mwenyewe ni Jemedari Rais Samia Suluhu Hassan. Matokeo makubwa ya utendaji kazi wake katika kipindi cha miaka minne ya usimamizi wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020 – 2025 yanawapa wapinga maendeleo kiwewe”

“Niwaambie vitendo vina sauti kuliko maneno matupu. Matokeo ya kazi kubwa na nzuri ya maendeleo na uimarishaji wa huduma kwa wananchi yanamfanya Rais Samia aishi kwenye mioyo na akili za watanzania walio wengi na hiyo ndio sababu wapinga maendeleo wanapata hofu kabla ya muda, watulie Rais Samia bado ana kazi ya kukamilisha” amesema

Hata hivyo Shaka ameipongeza kampuni ya Vodacom kwa uamuzi wa kutumia fursa hiyo ya kuwahudumia watanzania na wageni mbalimbali watakaosafiri na SGR pamoja na wananchi wa maeneo ya jirani, hatua inayotoa nafasi pia kwa Watanzania kuwa sehemu ya mabadiliko ya kidijitali.

George Rugata Mkurugenzi wa Mauzo na Usambazaji vodacom amesema kuwa vodacom itaendelea kutoa huduma za kisiasa ambazo sio tu kuwarahisihia wananchi kupata huduma kwa urahisi lakini pia kuinua maisha ya wananchi na kuimarisha uchumi nchini ambapo jumla vituo 456 vimefunguliwa katika mikoa mbali mbali nchini.