January 7, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shaka:CCM itabaki kuwa mtetezi maslahi ya umma

Na Mwandishi Wetu, Rukwa

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakitaacha kutetea maslahi ya umma, kupigania maendeleo ya kisekta au kutofuatilia ahadi zilozotolewa wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 kwani masuala hayo yameahidiwa na hayana budi kutekelezwa kwa muda muafaka ili kuimarisha ustawi wa maisha ya wananchi.

Aidha, chama hicho kimeapa kufuatilia utelelezaji wa kazi zote zilizoahidiwa na chama kupitia ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2020-2025 na mtendaji yeyote atakayezembea katika utekelezaji wake atachukuliwa hatua za kinidhamu.

Msimamo huo umetolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi,Shaka Hamdu Shaka kwa nyakati tofauti wakati akizungumza na wazee, wenyeviti wa mashina, viongozi na wanachama wa chama hicho Wilaya ya Sumbawanga Vijijini akiwa katika ziara ya siku mbili inayoongozwa na Katibu Mkuu wa CCM,Daniel Chongolo mkoani Rukwa.

Amesema, kazi ya CCM tokea enzi za TANU na ASP ni kushughulika na maisha ya watu, shida, kero zao lakini pia kutazama kwa kina iwapo mikakati ya kimaendeleo iliyobuniwa kisera katika maeneo husika inafanyiwa utekelezaji na hatimaye utelelezaji huo utoe matokeo chanya.

Shaka amebainisha kuwa,CCM kazi yake kubwa ni kutazama iwapo mipango na mikakati ya kisera inabeba uhalisia wa utekelezaji katika kutoa majawabu ya kero za wananchi na kuharakisha maendeleo na pale itakavyokuwa vinginevyo hakitakaa kimya aidha kwa kuogopa muhali au kwa kumuonea mtu aibu na pia kumuonea mtu badala yake kitatimiza wajibu wake kwa kuisimamia, kuielekeza na kukishauri serikali kuchukua hatua ili kufikia malengo kusudiwa.

“Lengo la wenzetu (upinzani) ni kutaka kutuondoa kwenye reli ya utelelezaji wa majukumu ya msingi na ya kisera ambayo hata wao wanajua tuliyoyaahidi kwa wananchi, hatutagombana nao wao waendelee kupiga mayowe, sisi tuendeleze ajenda yetu ya kuwatumikia wananchi kwa kuangalia maisha ya watu kwa kutatua shida, kero na chamgamoto zinazokwamisha maendeleo yao na nchi kwa ujumla,”ameeleza Shaka.

Hata hivyo, Shaka amesema katika ushindani wowote kila upande huomba washindani wao wadhoofike ili upande wa pili upate sababu za kuweleza wananchi kwamba mliowapa dhamana wameshindwa kutekeleza hili na lile hivyo watataka wao waaminiwe na wananchi kushika madaraka ya utawala jambo ambalo kwa CCM hawawezifanikiwa kutokana na umakini wake.

“Havijatokea vyama vya siasa makini na mbadala wa CCM vyenye uwezo na misuli ya kushika madaraka ya utawala. Kazi ya kuendesha nchi ni nzito na ngumu mno. Kazi ya utawala si mchezo au mahali pa kufanyia majaribio kama mpo maabara kwa sasa kazi hii CCM bado inaimudu vyema chini ya Rais Samia hivyo watanzania waendelee kutuamini,”amesema Shaka.