Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Babati
KATIBU wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, amesema uamuzi wa serikali kuwapanga vyema wafanyabiashara wadogo hauna lengo la kuwatia umasikini bali kuwajengea mazingira mazuri ya kujiongezea kipato.
Amesema kutokana na hilo ni vyema viongozi hususan wa Halmashauri za wilaya kuhakikisha hawapindishi lengo hilo kwa kuwawekea wamachinga mazingira magumu ya kufanyia biashara.
Shaka aliyasema hayo jana mjini Babati wakati akizungumza na wajasiriamali wadogo wanaofanya shughuli zao katika stendi ya zamani mjini Babati, mkoa wa Manyara ambao walilalamikia uamuzi wa kuwahamisha katika eneo hilo huku wakisema walikopelekwa kuna mazingira magumu ya biashara.
“Uamuzi wa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuwapanga wamachinga katika maeneo rasmi hauna maana ya kuwatengenezea umasikini, bali kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya biashara na kuongezea kipato,” alisema.
Shaka alitoa kauli hiyo baada ya kinamamma wanaofanyabiashara ndogodogo ikiwemo ya nyanya katika eneo hilo, kulalamikia changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo ikiwemo ya kusumbuliwa na mgambo wa Halmashauri.
More Stories
Makalla:Kupanga fujo ni dalili za kushindwa uchaguzi
Tanzania yapanda viwango Utawala wa Sheria Duniani
Rais Samia apeleka neema Tabora