November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Shahada 5 za Heshima za Falsafa kwa Samia somo kubwa kwa vizazi vijavyo

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Korea

TANGU Rais Samia Suluhu Hassan, aingie madarakani miaka mitatu iliyopita amezidi kujizolea umaarufu duniani kwa uongozi wake mahiri duniani.

Ipo mifano mingi ya wazo ya mambo ambayo Rais Samia ameweza kufanya nchini na sina sababu ya kuyarudia, kwani kila mwenye macho hawezi kuambiwa tazama.

Ingawa hapa kwetu wapo wanaojifanya hawaoni mambo makubwa na mazuri ambayo yamefanywa na Rais Samia akiwa Rais wa kwanza mwanamke nchini, lakini Dunia inaona na inasema wazi.

Majarida mengine makubwa yanayosomwa duniani kote kama The Time na Forbes ya Marekani yanamuweka Rais Samia kwenye orodha ya wanawake 100 wenye nguvu ulimwenguni.

Lakini pia jarida maarufu duniani la Avance Media la Ghana hivi karibuni limemtaja Rais Samia, kama mmoja wa wanawake 100 wa Afrika wenye nguvu na ushawishi mkubwa Barani Afrika.

Aidha, Chama cha Waandishi wa Habari za Miundombinu na Fedha Afrika (MIFA) kimchagua na kumpa Tuzo Rais Samia kama Rais aliyefanya mapinduzi makubwa zaidi kwenye miundombinu Barani Afrika kwa mwaka 2022.

Kwa kudhihirisha umahiri wa uongozi wake, ndani ya miaka mitatu Rais Samia ametunukiwa Shahada tano za Heshima (Honoris Causa).

Shahada ya Heshima ya Falsafa ni Shahada ya Juu sana katika elimu inayotolewa na Taasisi ya Elimu ya Juu (Chuo Kikuu) bila ya kumhitaji Mtunukiwa wa Shahada hiyo kufuata utaratibu wa kawaida na uliozoeleka wa kupata Shahada.

Utaratibu wa kawaida kupata Shahada ni mtu kuingia darasani kwa muda wa miaka fulani akisoma na kupikwa na baadae akifaulu hutunukiwa Shahada hiyo. Lakini, Shahada hii haimhitaji Mtunukiwa kuingia darasani.

Hii ni Shahada inayotunukiwa ama kutolewa kwa mtu aliyefanya jambo kubwa, la muhimu na lililoacha alama na kubadilisha maisha ya watu kwenye jamii ama Taifa.

Jambo hilo linaweza kuwa kwenye sekta ya elimu, kutumia maarifa yake kutatua changamoto kwenye jamii, kulinda na kupigania haki za binadamu.

Tamaduni na asili ya kutoa Shahada hii ya Heshima ilianza miaka ya 1470 kwenye kipindi cha kati cha zama za ‘Enlightenment’ Barani Ulaya na Marekani kwa Vyuo Vikuu mbalimbali kama Chuo Kikuu cha Oxford na Cambridge kuanza kuandaa utaratibu wa kuwatunuku watu mbalimbali waliokuwa na mchango mkubwa wa kuleta mageuzi katika Jamii.

Mtu wa kwanza kutunukiwa Shahada hii alikuwa Lionel Woodville ambaye alisifika kwa uhodari wake wa kutangaza neno la Mungu na kuuasa ulimwengu kuachana na maasi. Kuanzia hapo hadi sasa, ikawa ndiyo mwanzo wa Shahada hii ya Heshima.

Shahada hii ya Heshima haitolewi tu kienyeji kwa matakwa ya mtu fulani iwe kwa cheo chake ama nguvu ya kifedha, bali hufuata utaratibu mrefu wa majadiliano ya kina na jopo la Viongozi wa Chuo husika na Mabaraza yao (Deans).

Ni mpaka Maprofesa, Wasomi na Wanazuoni wakubaliane kumtunuku mtu Shahada hii ni lazima kweli mtu huyo awe amefanya kazi kubwa inayotambulika na kuacha alama kwenye jamii, iliyoleta mapinduzi makubwa ya kiuchumi, kijamii, kielimu, kisiasa, kitamaduni.

Kwa Rais Samia Hii ni rekodi na jambo ya kujivunia ndani ya nchi yetu. Kilianza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) ambacho Novemba 30, 2022 kilimtunuku Shahada ya Juu ya Heshima kwenye Humanitia na Sayansi Jamii (Social sciences).

Oktoba 10, 2023 kikafuatia Chuo Kikuu cha Jawaharlal Nehru cha nchini India.

Chuo Kikuu cha Jawaharlal NehruKwa kina heshima kubwa duniani, ambapo Rais Samia aliandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kutunukiwa Shahada ya Heshima na Chuo hicho na Rais wa tatu pekee baada ya Rais wa Urusi, Vladimir Putin pamoja ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa Japan Hayati Shinzo Abe kutunukiwa na Chuo hicho.

Na Desemba 28, 2023 Chuo Kikuu cha Zanzibar (SUZA) kilimtunuku Shahada nyingine ya Uzamivu ya Usimamizi wa Utalii na Masoko (Doctor of Philosophy in Tourism Management and Marketing- Honors Causa).

Aidha, Chuo Kikuu kikubwa cha Ankara cha nchini Uturuki kina kilimtunuku tena Rais Samia Udaktari wa Heshima. Aidha Wiki hii

Wiki hii Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea (KAU) kimemtunuku Shahada nyingine kutokana na mchango wake katika sekta ya usafiri wa anga.

Rais wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea, Hee Young Hurr, anasema chuo hicho kina historia ya miaka 72 na kimekuwa na ushirikiano na Tanzania hasa kwenye udhamini wa masomo ya shahada ya umahiri.

Anasema huo ni mwanzo mzuri wa ushirikiano kati ya Tanzania na Korea. “Uongozi wako unavutia na tumeamua kukutunukia shahada ya udaktari katika usimamizi wa usafiri wa anga,” anasema Hurr.

Mwenyekiti wa Bodi ya KAU, Amidi wa Shule Kuu, Soo Chang Hwang anasema kama kiongozi mwanamke, anatoa somo kubwa kwa vizazi vijavyo.

Anasema uongozi wake katika sekta ya anga ni wa kipekee na umekuwa na manufaa makubwa ikiwemo kuongezeka kwa idadi ya ndege zinazotua nchini, kuongezeka kwa idadi ya ndege za ATCL pamoja na mapato.

Anasema kwa kwa niaba ya Bodi ya KAU, tunakupongeza na shahada hii ni ishara ya heshima kwako kwa kile unachokifanya na tunatarajia utaendelea kuwa na ushirikiano na Chuo chetu,” alisema Hwang.

***Amefanya nini katika sekta ya anga?

Akizungumza baada ya kutunukiwa udaktari wa heshima, Rais Samia anashukuru Chuo hicho na kueleza kwamba sekta ya usafiri wa anga imekuwa na umuhimu mkubwa katika maendeleo ya nchi.

Kutokana na umuhimu huo, Rais Samia anasema ana nia ya kujenga chuo cha masuala ya anga nchini kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Anga cha Korea.

Anasema ilikuwa ni muhimu kulihuisha Shirika la ATCL na tangu hatua hizo zilipoanza kuchukuliwa, mapato ya ATCL yameongezeka kutoka sh. bilioni 33 mwaka 2016/17 hadi kufikia Dola za Marekani bilioni 308.4 mwaka 2023.

Kwa mujibu wa Rais Samia safari za ndege za kimataifa pia zimeongezeka kutoka 26 mwaka 2016/17 hadi kufikia 33 mwaka 2021 na hivyo kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini hadi kufikia karibu watalii milioni mbili wanaotembelea Tanzania.

“Ni muhimu kutambua kwamba waendeshaji wa ndani na wasafiri wamekuwa sehemu ya sekta hii kwani takwimu zinaonyesha pia idadi ya wasafiri imeongezeka kwa asilimia 25.6 kutoka abiria milioni tatu kabla a mlipuko wa Uviko-19 hadi abiria milioni 3.8 kufikia mwaka 2023,” anasema.

Rais Samia anasema mwaka 2006, Tanzania ilikuwa na ndege moja pekee, lakini hadi sasa ina ndege 14 za abiria pamoja na ndege moja ya mizigo. Pia, anasema imeweza kupanua masafa yake kutoka mataifa manne hadi kufikia mataifa 24.

Pia soko la shirika la ATCL la safari za ndani limefika asilimia 53 asilimia kutoka asilimia 2.4 tu mwaka 2022/23, huku idadi ya abiria imeongezeka kwa asilimia 42 kutoka milioni 4.8 mwaka 2015 hadi milioni 6.8 mwaka 2024.

Mbali na hapo, idadi ya marubani waliosajiliwa na wahandisi wa ndege imeongezeka kufikia 604 ikiwa ni ongezeko la asilimia 21 na wahandisi kufikia 76 ambalo ni ongezeko la asilimia 181 mpaka mwisho wa mwaka 2023.