Na Mwandishi wetu,Timesmajiraonline
SERIKALI kupitia Wizara ya Afya, imewahakikishia wananchi kuwa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV),haziuzwi na kwamba zipo za Kutosha.
Taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari na Mkuu wa Kiitengo cha Mawasiliano Serikali Wizara ya Afya,Roida Andusamile amesema watumiaji wa dawa hizi, hawana sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu upatikanaji wa dawa hizi.
“Wizara ya Afya imebaini uwepo wa taarifa kwenye mitandao ya kijamii pamoja na vyombo vingine vya habari zikielezea uhaba wa dawa za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI (ARV),na kwamba sasa watumiaji wanalazimika kununua dawa hizo,”amesema.
Amesema taarifa hizi ni za upotoshaji na zimeleta hofu miongoni mwa wananchi na kusababisha baadhi ya wagonjwa kuomba kupewa dawa za muda mrefu kwa ajili ya akiba, jambo ambalo si sahihi na linaweza kuathiri utunzaji na matumizi sahihi ya dawa.
Amesema Serikali kupitia Wizara inaendelea kuweka mikakati thabiti na stahiki ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kama kawaida.
Aidha, Wizara inatoa rai kwa wananchi kupuuza taarifa hizi na kuendelea kutumia dawa kwa usahihi kama wanavyoelekezwa na wataalam wa afya ili kuzuia usugu wa vimelea vya magonjwa haya dhidi ya dawa.
More Stories
Tanzania kuendeleza mipango ya kidemokrasia kukomesha mzozo na machafuko Congo
Wawili mbaroni kwa tuhuma za wizi waya wa TANESCO
Madiwani Lushoto wameridhia bajeti ya bil 54.6 mwaka 2025/26