December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yawatengea fidia wakazi wa Kipunguni

Na Agnes Alcardo,TimesmajiraOnline,Dar

MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo amesema, Serikali imetenga fedha ya fidia kwa ajili ya wakazi wa Kipunguni waliobomolewa nyumba zao kupisha upanuzi wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere (JNIA)

Mkuu huyo wa wilaya ameyasema hayo leo Septemba 13, 2024 Jijini Dar es Salaam, kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vilivyopo maeneo ya Ukonga Banana, mkutano uliozikutanisha Kata tatu za Kipawa, Kipunguni na Minazi Mirefu, lengo likiwa ni kusikiliza na tutatua kero za wananchi hao.

Akijibu kero za wananchi wa Kata hizo, Mpogolo amesema, anatambua kero mbalimbali walizo nazo wananchi katika maeneo hayo, huku akiwaondoa hofu wakazi wa maeneo ya Kifunguni kuendelea kuwa na subira kwani suala lao la kulipwa fidia litaenda kukamilika hivi karibuni.

Aidha, Mpogolo aliwapa pole wananchi wa mtaa huo na kuwapongeza kwa kuwa wavumilivu kubwa na kusema kuwa ni kweli zoezi hilo limekuwa la muda mrefu “Christapen tulikutana nae hadi kwa Waziri Mwigulu lakini wakapenya upande wa pili hadi kwa Waziri Mkuu kama mlivyomsikia kwa kuwa walitumia haki yao ya msingi ya kuwatumia viongozi wao,” amesema Mpogolo.

Ameongeza kuwa, ili kuwathibithishia kuwa suala la kuanza taratibu za malipo ameitaka kamati ya siasa katika kata hiyo kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Wilaya hiyo siku ya jumanne ili kuweza kuwapa uhakika wa kujua ni kitu gani kinaendelea.

Sambamba na hilo amewaahidi wananchi wa Kata ya Kiwalani kuwa, atatenga muda wa kutembelea kwa ajili ya kuangalia namna wanaweza kujenga kivuko ili wananchi waache kupita kwenye karavati la reli iliyopita katika kata hiyo.