December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaufungua Mnada wa Magena

Na Mbaraka Kambona,Timesmajira. Mara

WAZIRI Nwa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki ameielekeza Halmashauri ya Mji wa Tarime kuufungua mnada wa mpakani wa Magena, uliofungwa kwa zaidi ya miaka 20 ili uanze kufanya kazi ya biashara ya mifugo kama ilivyokusudiwa awali.

Waziri Ndaki ametoa agizo hilo wakati wa ziara yake ya siku moja aliyoifanya mkoani Mara mwishoni mwa wiki, ambapo alitembelea kuona hali ya mnada huo na kuruhusu uanze kufanya kazi, baada ya kuelezwa na kujiridhisha kuwa zile sababu zilizosababisha mnada huo kufungwa hazipo tena.

Amesema serikali imedhamiria kuufanya mnada huo kuwa wa kimataifa na watahakikisha, wanaboresha miundombinu yote iliyochakaa ili iweze kutoa huduma nzuri na serikali ianze kukusanya mapato yake.

“Kwa kuanzia tumetenga sh. milioni 150 kwa ajili ya kuanza kuboresha miundombinu ya mnada huu na tutaendelea kuuboresha zaidi, ili uweze kuvutia watu wengi wakiwemo kutoka nchi za jirani kuja kufanya biashara hapa,” amesema.

Amewataka wananchi wa Wilaya ya Tarime, hususan wanaoishi katika Kijiji cha Magena kuhakikisha wanautunza mnada huo ili uweze kuwa na tija kwao pamoja na nchi kwa ujumla.

Waziri Ndaki amewaonya wenye tabia ya wizi wa mifugo, kuacha vitendo hivyo mara moja kwani ndiyo vilichangia hata mnada huo kufungwa, huku akisema serikali ipo imara na imejipanga kuhakikisha wanakomesha vitendo hivyo ili wafanyabiashara wa mifugo, waweze kuutumia mnada huo na kufanya shughuli zao kwa amani.

“Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kuboresha maisha ya wananchi wake, kufunguliwa kwa mnada huu ni katika jitihada za kuboresha maisha yenu ili kila mmoja aweze kupata maendeleo yake kupitia shughuli halali anazozifanya,” amefafanua.

Naye Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, ambaye pia ni Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara amesema kufunguliwa kwa mnada huo kutatoa fursa kwa wananchi wa Mkoa wa Mara kujiongezea kipato kupitia shughuli mbalimbali zitakazokuwa zinaendelea katika mnada huo.

“Mheshimiwa Waziri tunakushukuru kwa kutufungulia mnada huu, lakini nakuomba usiishie kuwa mnada wa mpakani tu ni muhimu tukauboresha kwa kujenga miundombinu ya kisasa kwa ajili uwe wa kimataifa ili serikali, iweze kukusanya mapato mazuri na wananchi pia waweze kufaidika kupitia rasilimali zao,” amesema Waitara.

Ameongeza kuwa ni muhimu sasa operesheni inayoendeshwa na Jeshi la Polisi nchini la kupambana na wizi, itumike pia kushughulika na wezi wa mifugo ili biashara hiyo iweze kwenda vizuri na kushamiri mkoani hapa.

Mnada huo wa Magena ulikuwa kati ya minada 10 ya mipakani na ulijengwa mwaka 1995 na kufunguliwa mwaka 1996, ambapo ulifanya kazi takribani mwaka mmoja kabla ya kufungwa kwa sababu zilizotajwa kukithiri wakati huo, ikiwemo wizi wa mifugo na sababu nyingine za kiusalama zilizosababisha Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa kuufunga Mei 14, 1997.