Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
SERIKALI imetunga Sera ya Taifa ya Kudhibiti na
Kupambana na Dawa za Kulevya ya Mwaka 2024 ili kuhakikisha kuwa wadau wote nchini wanashiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo,Mei 16,2024 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera,Bunge na Uratibu,Jenista Mhagama wakati akizungumza na waandishi wa habari,kuhusu kuwasilishwa kwa taarifa ya hali ya dawa za kulevya Bungeni ya mwaka 2023 ambapo amesema Sera hiyo itaimarisha udhibiti wa dawa za kulevya zinazozalishwa nchini kama vile bangi na mirungi.
Aidha amesema sera hiyo inatoa maelekezo ya kufanya utafiti wa mazao mbadala katika maeneo yaliyokithiri kwa kilimo cha mazao hayo ili wananchi wa maeneo husika wajihusishe na kilimo cha mazao halali badala ya kilimo cha bangi na mirungi.
Mhagama amesema Sera inaelekeza kuwajengea
uwezo wadau mbalimbali katika udhibiti wa dawa za kulevya ili ushiriki wao ulete tija katika mapambano haya.
Hata hivyo ameeleza kuwa mwaka 2023 umekuwa wa kipekee katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kwani wamefanikiwa kukamata kiasi kikubwa cha dawa za kulevya kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya mapambano ya dawa za
kulevya hapa nchini.
Amesema Mamlaka kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ilifanikisha ukamataji wa jumla ya kilogramu 1,965,340.52 zikihusisha watuhumiwa 10,522 (wanaume 9,701 na wanawake 821).
“Dawa za kulevya zilizokamatwa ni Heroin
Kilogramu 1,314.28, Cocaine kg 3.04, Methamphetamine Kg 2,410.82, Bangi Kg 1,758,453.58, Mirungi Kg 202,737.51, Skanka Kilogramu 423.54 na Dawa Tiba zenye Asili ya Kulevya gramu 1,956.9 na mililita 61,672. Aidha,
kiasi hiki cha dawa za kulevya kilogramu1,965,340.52
zilizokamatwa katika kipindi cha Januari – Desemba 2023, ni karibu mara tatu ya kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa nchini kuanzia mwaka 2012 hadi 2022, ambacho ni kilogramu 660,465.4.
“Aidha, dawa ngeni zilizoanza kuingizwa nchini hivi karibuni kama vile methamphetamine, skanka na biskuti zilizochanganywa na bangi pia zilikamatwa katika kipindi hicho.
Vilevile amesema serikali imeendelea kuboresha huduma za tiba kwa watu wenye uraibu wa dawa za kulevya ili kupunguza madhara yanayotokana
na matumizi ya dawa hizo.
“Hadi kufika Mwezi Desemba 2023,
Serikali ilikuwa na vituo 16 vya tiba saidizi na unasihi kwa waraibu wa dawa za kulevya (MAT Clinics), Vituo hivi viliwahudumia waraibu wa dawa za kulevya 15,912.
“Aidha, Katika kipindi hicho
kulikuwa na nyumba 56 za upataji nafuu (sober houses)zikihudumia waraibu 3,488,”amesema Mhagama.
Hata hivyo Waziri Mhagama amesema kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado kuna safari ndefu katika
kupambana na janga hilo kwani ni wazi kuwa bado dawa za kulevya zinaingia nchini kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika nchi zinazozalisha dawa hizo,kubadilika kwa teknologia za uzalishaji na usafirishaji pamoja na utandawazi.
“Idadi kubwa ya watumiaji wa dawa za kulevya nchini ni vijana kwa wastani wa asilimia 78, hivyo kuathiri nguvu kazi ya Taifa ambayo ni mhimu
kwa maendeleo ya Taifa letu.
“Napenda kutoa rai kwa jamii kuwa, suala la elimu ya kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya linapaswa kuanzia ngazi ya familia,Wazazi na walezi tuendelee kuwajengea misingi bora watoto wetu
ili wasijiingize kwenye vitendo viovu na makundi hatarishi yanayoweza kuwaingiza kwenye matumizi na biashara ya dawa za kulevya,”amesema Waziri Mhagama.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba