September 20, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatenga Bil.70 ruzuku kwenye gesi

Na Moses Ng’wat, Songwe.

SERIKALI ipo katika hatua ya maandalizi ya kuanzishwa kwa mfuko wa nishati safi ya kupikia, utakaosaidia kuweka ruzuku ili kupunguza gharama za ununuzi wa mitungi yenye gesi ya kupikia.

Hatua hiyo imelenga kufanikisha mkakati wa serikali wa kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na matumizi ya kuni na mkaa hapa nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na matumizi ya kuni na mkaa kwa Tanzania.

Hayo yamebainishwa leo Septemba 19,2024 na Kamishina wa Wizara ya Nishati, Styden Rwebangira, wakati wa kongamano la kutoa elimu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia katika Mkoa wa Songwe iliyowahusisha wakuu wa wilaya,wakuu wa taasisi, walimu wa shule za msingi na sekondari, watendaji wa kata ,viongozi wa dini, mila na wananchi.

“Tunatarajia mfuko huo utakuwa kama wakala wa usambazaji umeme vijijini (REA) ambayo itakuwa na teknolojia ya matumizi ya gesi kulingana na fedha ambayo mtumiaji utaweka kama tunavyonunua luku kwenye umeme ikiisha unanunua tena,” amesema Rwebangira.

Naye, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira, Christina Mndeme, amesema serikali imetenga kiasi cha zaidi ya Sh. bilioni 70 kama fedha za ruzuku kwenye ununuzi wa mitugi ya gesi ya kupikia itakayotumiwa na watanzania ambapo fedha hizo zitasaidia ununuzi wa mitungi laki nne (4,000,00), huku baadhi ya taaisi zikinufaika ikiwepo magereza.

Mndeme amesema utafiti uliofanyika mwaka 2021 ulibaini asilimia 6 ya watanzania ndio wanatumia nishati safi hali iliyopelekea Mei 8,2024 Rais Samia kuzindua mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Ameongeza kuwa, lengo la serikali ni kufikia mwaka 2034 asilimia 80 ya watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia ikiwa ni pamoja na kupunguza vifo vitokanavyo na matumizi ya kuni na mkaa kwa Tanzania.

“Takribani watanzania 33000 hufariki kila mwaka kutokana na matumizi ya nishati isiyo safi ambayo ni kuni na mkaa ambayo waathirika wakubwa ni wanawaake ambao hutumia mda mwingi kupika majikoni,” amesema Mndeme.

Amesema serikali ipo katika mazungumzo na wawekezaji wa ndani na nje watakaowekeza nchini kwa lengo la kupunguza gharama za ununuzi wa mitungi ya gesi na kumrahisishia mwananchi wa kawaida kumudu gharama ili kampeni ya nishati safi ya kupikia iwe endelevu kupunguza uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wake, akisoma taarifa juu ya matumizi ya nishati safi ya kupikia Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Happiness Seneda, amesema asilimia 90 ya wananchi wa mkoani huo hutumia kuni na mkaa kama nishati ya kupikia ikiwepo kwenye taasisi ambazo shule,magereza na hospitali.