January 8, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Serikali kupitia TANROADS Mkoa wa Manyara inatekeleza miradi mbalimbali ya Maendeleo ya barabara ikiwemo mitatu mikubwa ya Kitaifa yenye lengo la kurahisisha na kupunguza gharama za usafiri, kuunganisha mkoa huo na maeneo ya Jirani pamoja na kupendezesha Mji huo kwa kuweka taa za barabarani.

Miradi inayotekelezwa mkoa wa Manyara ni pamoja na Sehemu ya kwanza (Lot 1) Mbulu – Garbabi km 25 katika barabara ya Karatu – Mbulu- Haydom, Sehemu ya pili (Lot 2) Labay –Haydom km 25 barabara ya Karatu – Mbulu – Haydom na sehemu ya kwanza (Lot 1) Dareda Centre –Dareda Mission km 8 katika barabara ya Dareda – Dongobesh.

Akitoa taarifa kwa umma kuhusu miradi inayotekelezwa katika mkoa wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Manyara Eng: Dutu John Masele amesema katika mkoa huo pia kuna miradi mitatu mikubwa ya ujenzi wa barabara inayotekelezwa kwa utaratibu wa EPC + Financing ambayo ni Arusha –Kibaya-Kongwa Junction km 493, Handeni –Kiberashi –Kijungu –Njoro –Olbolot –Mrijo Chini –Dalai –Bicha –Chambolo –Chemba –Kwa Mtoro –Singida km 460 pamoja na Karatu –Mbulu –Haydom –Sibiti River –Lalago –Maswa km 389.

Amesema katika mradi wa barabara ya Arusha – Kibaya –Kongwa km 493 mkoa wa Manyara una Jumla ya km 332.1 kati ya Losinyai na Dosidosi katika Wilaya ya Simanjiro na Kiteto Mtawalia, Mradi wa Handeni- –Kiberashi –Kijungu –Njoro –Olbolot –Mrijo Chini –Dalai –Bicha –Chambolo –Chemba –Kwa Mtoro –Singida km 460, Mkoa wa Manyara una km 120 kuanzia Kiberashi (Mpakani na Tanga) hadi Olbolot (Mpakani na Dodoma).

Mradi wa barabara ya Karatu – Mbulu –Haydom –Sibiti River –Lalago –Maswa km 389, mkoa wa Manyara una km 113 ukipunguza km 50 zinazotekelezwa kwa kutumia fedha za ndani, kipande cha Mbulu –Garbabi na Labay –Haydom, nyingine zote zinatekelezwa kwa utaratibu wa EPP+ Financing.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa Fedha 2022/2023 TANROADS mkoa wa Manyara imepangiwa kutekeleza kazi za matengenezo ya barabara km 1,657, matengenezo madogo ya madaraja 121 na ujenzi wa madaraja 7 kwa makisio ya Shilingi milioni 13.929.

Eng: ametaja kazi zilizopangwa kufanyika, ni kuweka taa za barabarani maeneo ya Mjini, Kuendeleza upanuzi wa barabara katika eneo la Mlima Dabii km 1.7 barabara ya Dareda –Dongobesh, Kuboresha eneo la Mizani Mdori, kuongeza midomo mitatu daraja la Sunya, Kuongeza Midomo miwili, daraja la Losinyai, kuongeza tabaka la lami sehemu zilizochakaa barabara ya Babati – Singida pamoja na kuchonga na kuziwekea Changarawe barabara Mbalimbali za Mkoa.

Aidha TANROADS Mkoa wa Manyara inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa km 1, 657 kati ya hizo km 207 ni barabara kuu na km 1450 ni barabara za mkoa.