Na Jackline Martin, TimesMajira Online
WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara ,Dkt Ashatu Kijaji amesema serikali itaendelea kuondoa vikwazo kwa wawekezaji kuanzia ngazi ya halmashauri ili kurahisisha uwekezaji nchini na kuongeza tija katika pato la Taifa.
Dkt. Kijaji alitoa kauli hiyo jana Jijini Dar es salaam katika mkutano uliowakutanisha wahariri wa vyombo vya habari, waandishi wa habari pamoja na watengeneza vipindi vya uwekezaji lengo ikiwa ni kupeana taarifa, kujengeana uwezo na kupeana elimu zaidi kuhusu mpango wa serikali wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.
“Kunasababu ya kudhibiti baadhi ya mambo lakini udhibiti huo uwe kwa lengo la kuendeleza sekta husika na uzalishaji usiwe na lengo la kukwamisha biashara, uwekezaji kwenye sekta husika hivyo tunadhibiti ili kuimarisha kumlinda mlaji na mtoa huduma ili waweze kufanya kazi zao wakiwa huru na wakiwa wanalindwa”Alisema.
Waziri Dkt. kijaji alisema serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi wataendelea kuainisha vikwazo kwa wawekezaji wanaotaka kuwekeza nchini na kuviondoa, hatua iliyotajwa kuleta uchechemuzi katika sekta ya uwekezaji.
“kumekuwa na malalamiko mengi huko nyuma, kumekuwa na mifumo isiyotabirika lakini msingi mmoja wapo wa utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara tuwe na mifumo inayotabirika , muwekezaji anapoingia nchini ajue ndani ya miaka mitano mpaka kumi, sera ya kodi ni hii lakini pia sera ya ushindani ni hii, isifike katikati ndani ya mwaka mmoja akabadilishiwa “Alisema.
Aidha Katika kuhakikisha kuwa mpango wa kuboresha biashara na uwekezaji unatekelezwa kwa ufanisi, Waziri Kijaji alisema serikali pia imefanikiwa kuanzisha idara ya viwanda , biashara na uwekezaji, kwenye mamlaka zote za serikali za mitaa, na mpango huu idara hizi zimeanza kutekeleza majukumu yake tangu Julai mosi mwaka huu.
“Uanzishwaji wa idara hizi dhamira yake ni kuendelea kuwa chachu ya kuboresha mazingira na maboresho mbalimbali yaliyoko kwenye serikali zetu za mitaa,” Alisema Dkt. Kijaji.
Mbali na hayo Dkt. Kijaji alizitaka taasisi zinazokusanya mapato ndani ya Taifa, zikusanye mapato kwa kutumia nyenzo rahisi na rafiki kwa kuweka vituo vya pamoja vya huduma au kuunganisha mifumo ya kuwahudumia wafanyabishara na wawekezaji nchini.
Aidha Waziri Dkt. Kijaji alitaka kukuzwa kwa ushindani wa kimkakati wenye usawa, tija na ubunifu kwa kupunguza Tozo na ada.”Ni lazima tuweze kukuza ushindani huwezi kuwa na mhudumu mmoja katika sekta husika ukasema kwamba hapa unaweza ukahudumia jamii katika ubora zaidi, lazima tukuze ushindani wenye tija wenye ubunifu ndani yake na usawa”,Alisema.
Waziri Kijaji alisema pia wameanzisha kitengo rasmi cha kuratibu na kuboresha mazingira nchini ambapo utekelezaji huo umeleta mafanikio mbalimbali hasa katika kukuza biashara, kuongeza ajira na kuboresha njia ya ukusanyaji mapato.
Pia Waziri Kijaji alisema kanuni zote zitakapotungwa zifanyiwe tathmini ya athari ya udhibiti kabla ya kuanza kutumika.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ally Gugu, alisema kikao hicho chenye lengo la kupeana taarifa , kujengeana uwezo na kupeana elimu zaidi kuhusu mpango wa serikali wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji na matokeo chanya ambayo yanapatikana au yanaweza kupatikana kufanya maboresho haya kitasaidia kuelimisha umma zaidi ili wafanyabishara na wawekezaji waweze kutumia fursa mbalimbali zinazojitokeza kulingana na maboresho hayo pamoja na kusisitiza Taasisi zinazotoa huduma za biashara na wananchi kwa ujumla kuendelea kuboresha ukuaji wa huduma hizo kwa wakati, ufanisi na tija zaidi.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi