December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yatangaza kibano zaidi watoroshaji wa mbolea ya ruzuku

-Nao wabadili mbinu, Hiace, Bajaji na Bodaboda zatumika.

-Mifuko 182 yakamatwa ikitoroshewa Malawi na Zambia.

Na Moses Ng’wat, Songwe.

SERIKALI kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imetangaza hatua kali zaidi zinazolenga kudhibiti tatizo la utoroshaji wa mbolea ya ruzuku kwenda nje ya nchi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari leo, Agosti 15, 2024, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kwa kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Joshua Ng’ondya, amesema TFRA imeajiri wataalam katika maeneo ya mipakani watakaohusika moja kwa moja katika kudhibiti utoroshwaji wa mbolea kwenda nje ya nchi kunakofanywa na baadhi ya watu na wafanyabiashara wasio waaminifu.

Alitaja mkakati mwingine ambao utatumika kudhibiti tatizo hilo ni Mamlaka hiyo kuingia makubaliano ya kimkataba (MoU) na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu (TPHPA) ili kudhibiti mipaka rasmi.

Ng’ondya amesema mikakati hiyo pia inaenda sanjari na operesheni mbalimbali za kushtukiza zitakazoendelea kufanywa kwa ushirikiano kati ya Mamlaka hiyo na vyombo vya ulinzi na usalama, ikiwemo kufuatilia wafanyabiashara wanaotiliwa mashaka katika mfumo wa mauzo ya mbolea ili kujiridhisha na mwenendo wa mauzo yao.

” TFRA tunakemea kwa nguvu zote vitendo vya hujuma kwa Taifa na tumejipanga kweli kweli kuhakikisha kwamba yeyote atakayejiingiza katika hujuma za utoroshaji wa mbolea anachukuliwa hatua kali ili iwe fundisho kwa watu wengine ” amesema Ng’ondya.

Katika hatua nyingine, Mamlaka hiyo imesema licha ya serikali kufanya opereshani mbalimbali za kudhibiti utoroshwaji wa mbolea hiyo ya ruzuku kwenda nje ya nchi, baadhi ya watu wanaofanya vitendo hivyo vya kuhujumu Taifa wamebadili mbinu za usafirishaji kutoka kusafirisha Malori na sasa husafirisha mbolea hiyo kwa kutumia magari madogo ya abiria (Hiace), Bajaji na Bodaboda.

Meneja huyo wa TFRA kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Ng’ondya amesema kuwa Agosti 5, 2024 Mamlaka hiyo ilifanikiwa kumkamata mfanyabiashara, Furaha Mwakalengela, akiwa na mifuko 128 ya mbolea aina ya Urea aliyokuwa akiitoroshea nchi jirani ya Malawi kwa kutumia Hiace yenye namba za usajili T 706 BMK.

Ng’ondya ameongeza kuwa, mnamo Agosti 12, 2024, TFRA kwa kushirikiana na jeshi la polisi lilikamata Hiace nyingine yenye namba za usajili T 168 CRS ikiwa na mifuko 44 ya mbolea ikitoroshwa kwenda nje ya nchi, pamoja na bajaji zenye namba MC 681 EHR na MC 532 DRN zikiwa na mifuko mitano kila moja na kwa watuhumiwa na vyombo vyote vinashikiliwa katika kituo cha polisi Tunduma.

Katika operesheni iliyofanyika hivi karibuni jumla ya wafanyabiashara wanane walikamatwa na kufikishwa mahakamani ambako kesi zao zipo katika hatua mbalimbali katika mahakama za Mkoa wa Songwe.