January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yataka changamoto za ushirika zitatuliwe

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Tabora

SERIKALI imemwagiza Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Vyama vya Ushirika kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) kuangalia namna ya kusaidia vyama vya ushirika nchini ili kumaliza changamoto zinazovikabili.

Agizo hilo limetolewa jana na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi David Silinde alipokuwa akifungua maadhimisho ya siku ya ushirika duniani yanayofanyika Kitaifa Mjini Tabora.

Alisema Shirikisho la Vyama vya Ushirika kwa kushirikiana na Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini wanafanya kazi nzuri kusimamia na kuhamasisha shughuli za wakulima jambo lililopelekea idadi ya wanachama kuongezeka zaidi.

Alibainisha kuwa kati ya mwezi Desemba 2012 na Machi 2023 wanachama wameongezeka kutoka mil 6.9 hadi mil 8.3 hivyo kupanua kwa kiasi kikubwa wigo wa uzalishaji mazao mbalimbali nchini.

Naibu Waziri aliongeza kuwa hadi kufikia Machi 2023 jumla ya kilo bilioni 1.8 za mazao mbalimbali sawa na tani milioni 1.85 zenye thamani ya sh trilioni 1.72 zimevunwa hivyo kuwezesha wakulima kunufaika zaidi na jasho lao.

Alitaja baadhi ya mazao hayo kuwa ni tumbaku, pamba, alizeti, korosho, zabibu, maharage, choroko, miwa, ufuta na mengineyo na kubainisha kuwa serikali ya awamu ya 6 chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuwainua zaidi.

Alitoa wito kwa vijana na wanawake kote nchini kujiunga na vyama vya maendeleo ya ushirika ili kunufaika na fursa zilizopo na mipango mbalimbali inayoendelea kufanywa na serikali katika kuinua juhudi za wakulima.

Aidha alielekeza Shirikisho la Vyama Vya Ushirika (TFC), COASCO na Tume ya Maendeleo ya Ushirika (TCBC) kusaidia vyama vya ushirika kuimarisha mfumo wao wa utunzaji taarifa kidigitali, kudhibiti mapato na kuwapa mafunzo watendaji wa vyama vya ushirika ili kuongeza ufanisi wao.

Mrajis na Mtendaji Mkuu wa Vyama vya Ushirika Benson Ndiege alisema kwa kutambua kuwa ushirika ni biashara wamejiwekea mikakati thabiti ya kuelimisha watendaji wa vyama vyote ili kupanua wigo wa uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao ya wakulima.

Alibainisha kuwa kwa sasa wapo katika mchakato wa kuanzisha Benki ya Ushirika Tanzania itakayokuwa ya kitaifa ili kuunganisha wana ushirika wote nchini, na lengo lao kwa sasa ni kubadilisha benki ya sasa ya Kilimanjaro Cooperative Bank Ltd (KCBL) na kuitwa National Cooperative Bank Ltd (NCBL).

Akiongeakwa niaba ya Mkuu wa Mkuu huo, Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Dkt Rashid Chuachua alisema hadi sasa Mkoa huo una vyama vikuu vya ushirika 3 ambavyo ni WETCU 2008 Ltd, Milambo na Igembensabo na hadi sasa wana vyama vya msingi (Amcos) 428 na SACCOS zipatazo 14.

Alipongeza serikali kwa kuwapatia kiasi cha sh mil 161 kwa ajili ya ujenzi wa majosho 7 katika wilaya ya Uyui na kiasi cha sh mil 27.2 kwa ajili ya uanzishwaji mashamba darasa na maeneo ya malisho katika wilaya mbalimbali.