November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yasikia kilio cha wakazi wa Rulenge

Na Allan Vicent, TimesMajira Online, Ngara

SERIKALI ya awamu ya 6 inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan imetoa zaidi ya sh mil 51 kwa ajili ya ujenzi wa daraja la Mto Murumuna litakalohudumia wakazi wa kata za Rulenge, Keza na Nyakisasa Wilayani Ngara Mkoani Kagera.

Daraja hilo linalounganisha Vitongoji vya Murumuna na Mtakuja katika Mamlaka ya Mji Mdogo Rulenge ni kiungo muhimu sana kwa wakazi wa eneo hilo kutokana na adha kubwa wanayopata ikiwemo kushindwa kuvuka wakati wa masika.

Akizungumza na gazeti hili jana Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini Wilayani hapa Mhandisi Christopher Masunzu alisema ujenzi wa daraja hilo umeanza na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi ujao.

Aliongeza kuwa mbali na ujenzi wa daraja hilo serikali pia imewapatia kiasi cha sh mil 130 kwa ajili ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa km 4.1 ambayo inaunganisha Vitongoji hivyo 2 kupitia daraja hilo, ujenzi wa barabara hizo umekamilika.‘Eneo hili ni hatarishi sana kwa akinamama, wanafunzi, wazee na jamii kwa ujumla, wakati wa masika maji hufurika hivyo kutopitika kirahisi, hali inayokwamisha shughuli za kiuchumi za wananchi’, alisema.

Mhandisi Masunzu aliishukuru serikali ya awamu ya 6 kwa kuwapatia fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati, kufungua barabara mpya na kuzifanyia matengenezo barabara zote zinazounganisha Vijiji na Kata katika wilaya hiyo.

Akielezea adha ya kukosa daraja katika eneo hilo, Mwanafunzi Hafidhi Hussein (12) wa shule ya msingi Rulenge alisema barabara hiyo ni fupi lakini walikuwa wanachelewa shule au kutokwenda kabisa kutokana na maji kujaa.

Bi.Mwanne Ruheta (46) mkazi wa kitongoji cha Mtakuja alisema akinamama wanapata shida sana kupeleka watoto wao kliniki hivyo akaomba mafundi wanaojenga daraja hilo kuharakisha kazi hiyo ili kumaliza kero hiyo.

Naye Mzee Haruna Muwachu (70) mkazi wa kata jirani ya Keza alisema mto huo umeshachukua roho za ndugu zake 2 ambao walijaribu kuvuka na baskeli lakini maji yakawazidi nguvu na kuwasomba na walipowatafuta walikuta wameshafariki.

Alimshukuru Rais Samia kwa kujali wananchi wa Rulenge hivyo akaomba ujenzi wa daraja hilo uharakishwe kwa sababu kipindi hiki cha mvua wanapata shida sana kuvuka mto huo.

Wakazi wa Vitongoji 2 vya Mtakuja, Murumuma na kata za Rulenge, Keza na Nyakisasa wakipita kwa taabu katika daraja la muda la Mto Murumuna lililopo katika Mamlaka ya Mji Mdogo Rulenge Wilayani Ngara Mkoani Kagera mahali linapojengwa daraja jipya, wa kwanza kushoto ni Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mjini (TARURA) Wilayani Ngara Mhandisi Christopher Masunzu. Picha na Allan Vicent.