December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yasaini mkataba wa ujenzi wa umeme wa nguvu ya maji Kigoma wa megawati 49.5

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

SERIKALI imesaini mkataba na Kampuni ya Dongfang Electric International Corporation  ya Nchini China wa ujenzi wa mradi wa uzalishaji umeme wa Megawati 49.5 kwa nguvu ya maji katika mto Malagalasi mkoa wa Kigoma.

Mkataba huo umesainiwa jijini hapa leo,Februari 8,2024 na kushuhudiwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Dotto Biteko ambapo alisema Serikali itaendelea kuvijengea vyanzo vya Umeme nchini ili kuweza kukabiliana na Upungufu wa Umeme ambalo limekuwa ni mwiba kwa Taifa

Baada ya kusainiwa kwa  Mkataba  huo Dkt.Biteko alisema kuwa nchi ya Tanzania imekuwa na uhitaji mkubwa wa Nishati ya Umeme na mahitaji hayo yamekuwa yakiongezeka kila siku huku vyanzo vikibaki kuwa vile vile hali hiyo imekuwa ikipelekea Upungufu katika Vyanzo vya Umeme.

“Miradi inahitaji muda wa kuwekeza na kuitunza lakini pia Serikali inaweka msukumo mkubwa kuhakikisha suala la Nishati sio tatizo ndani ya nchi yetu, ” Amesema.

Alisema Mradi wa Malagarasi unahusisha ujenzi wa eneo la kufua umeme wa maji, njia za kupitisha maji, jumba la mitambo ya umeme, kituo cha kupokea na kusafirisha umeme, ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 132 ambayo itaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa kupitia kituo cha Kidahwe- Kigoma na  kuunganisha umeme kwenye vijiji 7 vitakavyopitiwa na mradi.

Aidha ameishukuru Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) kwa kutoa mkopo wa masharti nafuu wa kiasi cha Dola za Marekani milioni 140 ili kutekeleza mradi wa Malagarasi ambapo Serikali ya Tanzania imetoa  Dola za Marekani Milioni 4.14. Amesema Benki hiyo imeendelea kuiunga mkono Serikali katika miradi mbalimbali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Mkuu waShirikalaUmemeTanzania(TANESCO)Mhandisi Gissima Nyamuhonga amesema ujenzi wa mradi huo Utagharimu Dola  za Kimarekani 144.14 na utachukua miezi 42 hadi kumalizika .

Pia ameishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika  kwa  mkopo nafuu kwa kutoa Dolla za kimarekani Milioni 140 huku Serikali ya Tanzania kutia Dolla  Milioni 4.4.

Amesema mradi wa kufufua Umeme kwa nguvu ya maji wa Mto Malagalasi upo kilometa 100 kusini mwa Mji wa kigoma, kilometa 27 kusini mwa Barabara kuu ya Uvinza  – Kigoma katika Kara ya Kazuramimba  kijiji cha Igamba kwenye Mto Malagalasi wenye lengo kuu la kuboresha  usambazaji wa Umeme Magharibi mwa Tanzania ili kuchochea shughuli za kijamii na kiuchumi  katika mikoa ya Magharibi mwa nchi ikiwemo kigoma.

Alieleza kuwa Mradi huo utawezesha ongezeko la Umeme katika Gridi ya Taifa na kuwezesha biashara Umeme wa kanda na mradi wa Malagalasi unatarajiwa kuzalisha Umeme wa wastani wa Gigawati 181 kwa mwaka.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Nishati,amesema Mradi huo wa Mto Malagalasi ni miongoni mwa Miradi ambayo ilianza kwa Muda mrefu ambapo Serikali ilikuwa imeagiza Mikoa ambayo haijaunganishwa na Gridi ya Taifa iunganishwe kwa haraka ili kuharakisha Maendeleo.

Amesema kutokana na Mkoa huo kuunganishwa na vyanzo vinne Vya Umeme Unakwenda kuwa Tajiri wa umeme.

“Tunaimani baada ya Mkoa wa Kigoma Kupata Umeme, mipango ya Muda mrefu inakwenda kukamilishwa kutokana na Uwepo wa Nishati hiyo,”amesema 

Akizungumza kabla ya utiaji Saini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Ajira na Wenye Ulemavu,Profesa Joyce Ndalichako amesema mbali na uzalishaji wa megawati 49.5 kuongeza kiwango cha umeme katika gridi ya Taifa, pia hatua hiyo itachochea uanzishaji na ukuaji wa viwanda katika mkoa wa Kigoma.

Ameongeza kuwa kupitia hali hiyo, ajira zitaongezeka na kuwezesha wananchi kushiriki katika kukuza Uchumi wa Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Thobias Andengenye amesema maono na maelekezo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhusu uzalishaji wa nishati mkoani humo yameuheshimisha Mkoa wa Kigoma na Taifa kwa ujumla.

Amesema uzalishaji wa megawati 49.5 za umeme utapunguza gharama za uendeshaji ambapo kwa sasa zinatumika lita 28,000 za mafuta kwa siku kwa ajili ya kuzalisha umeme.