Na David John,Timesmajiraonline
SERIKALI imepokea Gawio la sh. bilioni 2.5 kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Kuhifadhi Mafuta (TIPER) Tanzania, fedha hizo zitasaidia kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akizungumza katika hafla fupi ya kupokea gawio hilo, jijini Dar es Salaam, leo Julai 27 ,2023 Msajili wa Hazina Nehemiah Mchechu amesema lengo la uwekezaji wa kampuni hiyo ni kuongeza mchango kwa maendeleo ya taifa.
“Nawapongeza sana TIPER kwani walichofanya ni kiitu kikubwa, tunazihimiza kampuni nyingine kutoa gawio kwani fedha hizo ndizo ambazo zinakwenda kuinua uchumi wa nchi na kutekeleza miradi ya maendeleo,”amesema.
Amefafanua kuwa kuna baadhi ya kampuni ambazo mwaka ujao wa fedha zitafutwa kutokana na kupitwa na wakati au huduma zake na nyingine zitaunganishwa kutokana na shughuli zake kushabihiana ambapo zikiunganishwa na kufanya kazi pamoja zitaleta tija zaidi.
“Kuna timu inaendelea kufanya uchambuzi zaidi na mwezi wa nane mwaka huu ripoti itapokelewa na kutangazwa ni kampuni gani zitaunganishwa au kufutwa kwani wakati mwingine kampuni hufanya vibaya sababu ni uongozi hivyo lazima wapewe muda kwa kuwavumilia na kuangalia uongozi wao,” amesema.
Mkurugenzi Mtendaji wa TIPER Tanzania, Mohamed Mohamed,amesema kuwa sekta ya mafuta ni moja ya maeneo muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani na ina mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi.
Amesema sekta hiyo ina mchango mkubwa katika usafirishaji, kilimo na miundombinu kwa sababu mafuta yanatumika kwa matumizi mbalimbali, hivyo imeendelea kuwa mhimili muhimu kwa maendeleo ya uchumi.
“Kuwekeza katika rasilimali watu ni jambo muhimu hususan kwa kampuni ambayo inaendelea kukua na inapenda kujipqmbqnua kuwa kampuni yenye nmchango mkubwa katika jamii,”amesema.
Akizungumzia uwekezaji ambao wanataka kuufanya nchini,amesema kuwa uwekezaji umekuwa ukifanyika kipindi cha miaka 10 iliyopita na wamendelea kuwekeza, hivyo ni jambo endelevu.
Amesema TIPER imejipanga kuongeza ufanisi,tija na faida na kwamba wanaimani mwaka unaokuja wanaweza kutoa gawio kubwa zaidi huenda likawa mara mbili ya walilotoa mwaka huu.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato