December 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaonyesha juhudi katika kukuza sekta ya mifugo

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi Tixon Nzunda amesema mpango wa Serikali ni kuwekeza ng’ombe wazazi na ng’ombe wa maziwa zaidi ya 2000 katika mashamba ya mifugo  ya Sao Hill,Ngerengere,Ngaramo ,kitulo na Narco ili kuongeza uzalishaji wa ng’ombe bora na wenye tija hapa nchini.

Aidha amesema,baada ya uzalishaji ng’ombe hao watauzwa  kwa bei ya kurudisha  sehemu ya gharama ambazo serikali imetumia na siyo kibiashara ili kuongeza wigo wa usambazaji mifugo.

Katibu Mkuu huyo ameyasema hayo leo wakati akifungua kikao cha wadau wa mifugo kilichoketi jiji Dodoma kwa ajili ya kujadili mazingira ya ufanyaji biashara kwenye sekta ya mifugo .

“Katika kuhakikisha mashamba hayo yanapata mifugo,matumaini ya Serikali ni Sao hili kuwa na ng’ombe wazazi 500,Ngerengere ng’ombe 200,Ngaramo ng’ombe 200 ,lakini pia shamba la Kitulo ng’ombe wa maziwa  160 ,ili tuweze kupata ng’ombe wazazi watakaoweza kuongeza uzalishaji .amesema na kuongeza kuwa

“ Kwa hiyo Serikali inajielekeza katika eneo hilo lakini pia ndani ya mwaka huu wa fedha tunategemea Narco wanunue ng’ombe 1000 ambao pia serikali itatoa fedha ili ng’ombe 500 wapelekwe Kongwa .”

“Kwa hiyo ndugu wadau tunajaribu kuonyesha juhudi hizi za serikali ni kwa sababu tunataka watu wanaotaka kufuga kisasa,kibiashara na wanaoweza kusaidia kuleta tija na siyo wafugaji wa kuzurura,najua haya maneno yanawakera sana wale wanaofuga kwa kuzurura kutoka Kaskazini hadi Kusini ,

“Lakini siogopi kuwaambia hatuwezi kuendelea kufuga kwa kuzurura ,tunataka au hatutaki ni lazima twende kwenye kufuga kisasa,ufuge kulingana na eneo ulilonalo sasa hayo ndiyo mazingira sahihi ya ufugaji wa kisasa lakini siyo kufuga tu, unaamka asubuhi hujui unapokwenda yamepitwa na wakati.”amesisitiza Nzunda

 Ametumia nafasi hiyo kuwaasa wanasiasa kuacha kuwapotosha wananchi kwa makusudi kuhusu ufugaji wa kuzurura hali ambayo amesema inadumaza sekta ya mifugo.

“Ni  lazima tuwambie maana tunajua katika eneo hilo kuna wanasiasa wapotoshaji, wanapotosha kwa makusudi ili kudumaza sekta ,sisi tumeamua tutafanya mabadiliko bila kujali kama mabadiliko hayo yatakuwa machungu lakini tunataka ibadilike ili iweze kuwa na mchango katika uchumi wa nchi.”amesema

Amezungumzia kuhusu malisho ya mifugo ambapo amesema,Serikali imeamua kuanza na mashamba darasa 100 kwa ajili ya kuwaonyesha wafugaji wadogo namna ya kulima malisho ya mifugo ili kusiwe na visingizo kwamba hawajui.

“Lazima tuwekeze katika eneo hilo kwa sababu hakuna mtu mwingine wa kusaidia kuwekeza katika hilo ,lazima wewe mwenyewe uwajibike uandae fedha,uuze sehemu ya mifugo uwekeze uweze ili uweze pamoja na mambo mengine pia uweze kupata malisho.”amesisitiza Katibu Mkuu huyo