April 30, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaombwa kusambaza umeme kwa kasi na kuboresha huduma vijijini

Na Joyce Kasiki, Timesmajira online,Dodoma

BUNGE limepitisha bajeti ya Wizara ya Nishati ya zaidi ya shilingi Trilioni mbili huku Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko akiwahakikishia Wabunge kuwa maono na ushauri waliotoa vinafanyiwa kazi kwa haraka Ili kuboresha sekta ya Nishati nchini.

Akijibu hoja za wabunge wakati akihitimisha hoja ya bajeti yake,Dkt.Biteko amesema michango yao yote waliyoitia itazingatiwa kwani Serikali peke yake haiwezi kuendesha sekta hiyo.

Amesema Moja ya hoja ambayo Wabunge wameizungumza sana ni kuhusu mradi wa LNG ambapo amesema pamoja na mradi huo kuanza muda mrefu kujadiliwa lakini

“Tunatamani mradi huo uwepo lakini majadiliano haya lazima yalete tija,,,mtakumbuka huko nyuma Mheshimiwa SpikaSerikali baada ya kukamilisha majadiliano ya awamu ya kwanza ilirudisha majadiliano hayo kwa ajili ya kupata maoni,

“Baada ya kupita kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ,ukweli ni kwamba yapo mambo mengi ambayo yalikuwa yanahitaji kufanyiwa kazi zaidi Ili kupata mkataba mzuri zaidi,

“Leo tinaweza kusmea mradi huo uanze,lakini mkataba uliopo mzuri Leo ,kesho unaweza kuwa mbaya,,,Nchi hii Ina historia ya kupita kwenye mikaraba inayolalamikiwa na tumejigfunza mengi lakini yapo mambo ambayo ni lazima yafanyiwe kazi kabla ya mkataba huo kusainiwa.

Amesema Serikali pamoja na wawekezaji timu kinaendelea na majadiliano Ili kuondoa changamoto zilizopo ambazo zimebaki chache sana ,tunatarajia kuwa ndani ya mwaka huu 2025 kama tutakuwa tumemaliza mambo matatu yaliyosalia nataka nikihakikishie kuwa mkataba utasainiwa na mradi huo uanze mara Moja

Ametoa wito kwa Wabunge waipe muda Wizara Ili ifanyie kazi mambo hayo kwa maslahi mapana kwa Taifa.

Mapema wakichangia bajeti hiyo  Wabunge wameiomba Serikali kuongeza kasi ya kusambaza umeme katika vitongoji mbalimbali nchini, sambamba na kuboresha hali ya umeme maeneo ambayo bado yanakumbwa na changamoto ya kukatika mara kwa mara.

 Wabunge hao wamesema hayo wakichangia bajeti ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo waliipongeza Serikali kwa hatua kubwa zilizofikiwa lakini wakasisitiza bado kuna kazi ya ziada inayopaswa kufanyika.

Mbunge wa Viti Maalum, Sophia Mwakagenda, alieleza kuwa licha ya kuwepo kwa miradi mikubwa kama ule wa kufua umeme wa Julius Nyerere, bado kuna changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara katika baadhi ya maeneo. 

Alibainisha kuwa Tanzania ina zaidi ya vitongoji 32,000 lakini ni 927 tu ndivyo vilivyopata umeme hadi sasa, hali ambayo inaonesha uwiano mdogo wa usambazaji wa nishati hiyo muhimu.

Mwakagenda alisisitiza kuwa Serikali inapaswa kuongeza kasi ya usambazaji umeme hasa katika maeneo ya vijijini ambako ndiko wananchi walio wengi wanaishi huku akitaja baadhi ya mikoa kama Rukwa, Katavi, Lindi na Mtwara kuwa bado haijaunganishwa kikamilifu katika gridi ya Taifa, jambo linalosababisha huduma ya umeme kutokuwa ya uhakika.

Katika mchango wake, alieleza pia changamoto za kibajeti zinazoikumba Wizara ya Nishati, ambapo baadhi ya fedha zinazotegemewa kutoka kwa wafadhili hazijawasilishwa kwa wakati. 

Alitolea mfano wa zaidi ya shilingi bilioni 52 ambazo zilitakiwa kutolewa na wadau lakini hadi sasa hazijafika huku akisema hali hii, inasababisha kuchelewa kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Aidha, Mwakagenda alizungumzia umuhimu wa Shirika la TANOIL ambalo ni chombo cha Serikali kusimamia mafuta nchini, lakini akatahadharisha kuhusu deni la zaidi ya shilingi bilioni 21 linalolikabili shirika hilo.

 Alimwomba Waziri wa Nishati, Doto Biteko, kuhakikisha fedha hizo zinarejeshwa haraka kwenye mfuko wa Serikali ili kuimarisha uendeshaji wa sekta ya nishati.

Wabunge pia waligusia tofauti kubwa ya gharama za kuunganishiwa umeme kati ya maeneo ya vijijini na mijini. Ilielezwa kuwa wakati wananchi wa vijijini hulipia shilingi 27,000 kwa mita 30, katika maeneo mengine gharama hiyo huweza kufika hadi shilingi 626,000 kwa mita 120,000. Hali hii imeleta malalamiko ya kuwepo kwa matabaka ya kimapato baina ya wananchi wa mijini na vijijini.

Kuhusu matumizi ya nishati safi, Mwakagenda alisema jitihada zimeanza kuzaa matunda ambapo wananchi wengi wameanza kuelewa umuhimu wa kutumia majiko ya gesi na kuni mbadala. Alieleza kuwa baadhi ya majiko yamegawiwa kwa wabunge ili wayasambaze kwa wananchi, huku gesi yenye ruzuku ikipunguza gharama kutoka shilingi 48,000 hadi kati ya shilingi 18,000 hadi 20,000.

Hata hivyo, aliomba Serikali kuongeza idadi ya majiko hayo, akitolea mfano wa Wilaya ya Rungwe iliyopokea majiko 300,000, akisisitiza kuwa bado mahitaji ni makubwa. Pia aliomba mitungi ya gesi ilindwe kutokana na baadhi ya wananchi kuitupa baada ya gesi kuisha, jambo linalosababisha hasara na uchafuzi wa mazingira.

Mbunge huyo alielezea umuhimu wa mradi wa umeme wa Runakali utakaozalisha megawati 222 kwa gharama ya trilioni 1.58. Mradi huo utatekelezwa katika wilaya za Makete na Busokelo na una manufaa makubwa kwa taifa, lakini alieleza kuwa wananchi walioko katika maeneo yatakayopitiwa na mradi huo bado hawajalipwa fidia walizoahidiwa tangu mwaka 2019.

Mwakagenda alitaja kata za Rufilio, Itete, Ruangwa, Isange, Mpombo na Kandete kuwa miongoni mwa maeneo ambayo wananchi wake wamesubiri fidia kwa muda mrefu. Alisema fidia hiyo ingewezesha wananchi kuanzisha maisha mapya katika maeneo mengine, hivyo aliomba Serikali kuwapa kipaumbele katika malipo hayo.

Akizungumzia mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 15 vya mikoa ya Mbeya na Tanga, Mwakagenda alisema mkandarasi alichelewa kupatikana, hali iliyoathiri utekelezaji wa mradi huo. Alieleza kuwa ni hadi wiki iliyopita tu ndipo kandarasi ilisainiwa, hivyo aliiomba REA kusimamia kwa karibu utekelezaji huo.

Mbunge huyo pia alishauri Serikali kupeleka umeme kwa wananchi hata kabla ya malipo kamili, akisema utaratibu wa wananchi kulipia kidogo kidogo unaweza kuongeza mapato ya Serikali huku ukiwaondolea adha wananchi wa maeneo ya vijijini.

Kuhusu nishati jadidifu, Mwakagenda alisema eneo la Busokelo limebarikiwa kuwa na umeme wa jotoardhi na visima tayari vimechimbwa na vinaonyesha uwepo wa maji ya moto kwa kasi kubwa. Aliiomba Wizara ya Nishati kutenga fedha ili miradi ya Mbaka, Kejo na Mambo ianze kutumika haraka.

Katika mchango wake, Mbunge wa Viti Maalum Christine Ishengoma aliiomba Serikali kulitatua tatizo la kukatika kwa umeme ambalo linaathiri vifaa vya umeme vya wananchi kama televisheni, friji na redio. Alisema tatizo hilo linaathiri maisha ya kila siku ya wananchi.

Naye Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro, aliipongeza Serikali kwa maboresho makubwa yaliyofanyika kupitia TANESCO ambapo sasa wananchi hupata taarifa mapema endapo kutatokea hitilafu ya umeme. Alisema licha ya kukatika kwa umeme bado kuendelea, tofauti kubwa imeonekana ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Alisisitiza kuwa matumizi ya umeme vijijini bado ni madogo na akaiomba Serikali kuhakikisha mwaka wa fedha 2025/2026 unatumika kuongeza upatikanaji wa umeme katika vitongoji vyote nchini. Alisema azma kubwa inapaswa kuwa kuhakikisha asilimia kubwa ya vitongoji vya Tanzania vinapata umeme ifikapo mwaka 2030.

Naye Mbunge wa Jimbo la Busokelo,  Atupele Mwakibete, ameishauri Serikali kuimarisha gridi ya Taifa pamoja na miundombinu ya kusambaza umeme nchini huku akisema, licha ya Tanzania kuzalisha zaidi ya megawati 4000 za umeme, bado kuna changamoto kubwa ya usambazaji kwa wananchi, hivyo ni muhimu Serikali kuongeza kasi ya kupeleka huduma hiyo muhimu kwa Watanzania wote.

 Mwakibete ameeleza kuwa katika maeneo ya jimbo lake la Busokelo, mvua hunyesha kwa takriban miezi 10 hadi 11 kwa mwaka, hivyo nguzo za mbao zinazotumika kwa usambazaji wa umeme huharibika kwa haraka. Kutokana na hali hiyo, ameshauri Serikali kusambaza nguzo za zege katika maeneo yenye unyevunyevu ili kuhakikisha uimara na uendelevu wa miundombinu hiyo ya umeme.

Katika kuchangia hoja kuhusu miradi ya kimkakati, Mbunge huyo ametolea mfano wa mradi wa umeme wa Runakali, ambao unatarajiwa kuzalisha megawati 222 na kugharimu takriban shilingi trilioni 1.58. Ameeleza kuwa mradi huu wa muda mrefu unatarajiwa kuwa na manufaa makubwa kwa taifa, hasa ukizingatia kuwa unatekelezwa katika mikoa ya Mbeya na Njombe, ndani ya wilaya za Makete na Busokelo.

Aidha, Mwakibete ameikumbusha Serikali kuhusu fidia ambayo wananchi wa kata za Rufilio, Itete, Ruangwa, Isange, Mpombo na Kandete waliahidiwa tangu mwaka 2018/2019.

 Ametoa wito fidia hiyo ya takriban shilingi bilioni 264 itolewe haraka ili kuwawezesha wananchi hao kuendelea na maisha yao katika maeneo mengine baada ya kupisha mradi wa umeme mkubwa.

Kuhusu mpango wa kusambaza umeme vijijini kupitia REA, Mbunge huyo amesema kuwa katika mradi wa kusambaza umeme kwa vitongoji 15 vya mikoa ya Mbeya na Tanga, kumekuwa na ucheleweshaji wa kuwapata wakandarasi. Hata hivyo, amefarijika kusikia kuwa wiki iliyopita mikataba ilisainiwa, na sasa anaiomba REA kusimamia utekelezaji wa haraka wa mradi huo.

Pia ameshauri Serikali kurahisisha upatikanaji wa umeme kwa wananchi kwa kuwawezesha kulipia kwa awamu ndogondogo. Ameeleza kuwa mfumo huu utawawezesha wananchi wengi kupata huduma hiyo huku Serikali ikiendelea kukusanya mapato kwa utaratibu wa kudumu na endelevu.

Vilevile,  Mwakibete amezungumzia fursa ya umeme jadidifu, hususan jotoardhi katika maeneo ya Mbaka, Kejo na Mambo ndani ya Busokelo. Ametoa ombi kwa Wizara ya Nishati kutenga fedha kwa ajili ya kuanza kutumia umeme huo ambao tayari visima vya maji vya joto vimeshachorongwa kwa mafanikio kupitia kampuni tanzu ya TANESCO. Mwisho, amegusia ongezeko la vituo vya mafuta nchini na kuiomba Serikali kuhakikisha usalama wa maeneo hayo, ili kuepusha athari iwapo ajali zitatokea.