November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yamaliza mgogoro wa ardhi baina ya wananchi na NARCO Kigoma

Na Mbaraka Kambona,TimesMajira online,Kigoma

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi,Mashimba Ndaki ameielekeza Kampuni ya Ranchi za Taifa (NARCO) kutenga Ekari 15000 na wazigawe kwa wananchi wa vijiji viwili vya Mpeta na Chakulu vilivyopo wilayani Uvinza,mkoani Kigoma ili kutatua mgogoro wa ardhi wa muda mrefu baina ya wananchi hao na kampuni hiyo.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki akiongea na wananchi wa Kijiji cha Mpeta ambapo alieleleza kuwa zaidi ya Ekari 14000 zitegwe kutoka katika Ranchi ya Uvinza na zigawiwe kwa wananchi wanaoishi katika eneo la Mwandulubhantu na Kazaroho ili wazitumie kwa makazi na shughuli nyingine za kimaendeleo.

Ndaki ametoa maelekezo hayo jana katika ziara yake Wilayani Uvinza, Mkoani Kigoma kwa lengo kutatua mgogoro huo ardhi kufuatia wananchi wa vijiji hivyo kuvamia maeneo ya Ranchi ya Uvinza na kuishi humo kinyume na taratibu.

Akiongea na wananchi wa vijiji hivyo kwa nyakati tofauti, Waziri Ndaki amesema kuwa Serikali imeamua kufikia maamuzi hayo ili wananchi hao waweze kujikita katika shughuli za maendeleo na kuachana na migogoro ya kila siku ambayo haina tija yoyote.

“Hatupendi tuendelee na migogoro kwenye maeneo yetu, tunataka tumalize migogoro ili tuanze kufanya shughuli za maendeleo, kila mwananchi afanye shughuli yake bila bughudha yoyote,” amesema Ndaki.

Wananchi wa Kijiji cha Mpeta wakiagana kwa furaha na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki (katikati kulia) muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkutano wa Waziri huyo na Wananchi wa Kijiji cha Mpeta uliofanyika Wilayani Uvinza Mkoani Kigoma Aprili 25, 2021

Ameongeza kuwa baada ya ugawaji wa maeneo hayo kukamilika Mkuu wa Wilaya ya Uvinza na timu yake watakwenda kufanya tathmini katika maeneo hayo na kuyafanyia mchakato wa kuyarasimisha ili kuwa Kijiji au Kitongozi.

Amesisitiza kuwa pamoja na wananchi hao kuvunja Sheria, Serikali imeangalia maslahi mapana na ndio maana imeamua kutoa sehemu ya eneo katika ranchi hiyo ili wananchi hao waweze kuishi kwa utulivu na kuendelea na shughuli zao huku akiwaonya kuwa wasijaribu tena kuingia katika ranchi hiyo baada ya kugawa ekari hizo na atakayefanya hivyo anatafuta kesi.

“Ranchi ni eneo la kufugia mifugo na sio eneo la kuishi watu au kulima humo, atakayejaribu kuingia tena ananitafuta kesi, tumewapa maeneo hayo ili mkae humo, atakayetaka kufuga aje sisi tutampa eneo la kukodisha kwa bei ya Serikali ili aweze kufuga kisasa, kulima malisho na kuongeza tija ya mifugo yake,” alisisitiza Ndaki

Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mwanamvua Mrindoko baada ya kumshukuru Waziri Ndaki kwa uamuzi huo naye amewasisitiza wananchi hao kutoendelea kuvamia maeneo ya ranchi hiyo ili kuepukana na migogoro isiyo na tija na badala yake watumie maeneo hayo waliyopewa kujiletea maendeleo yao.