January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yakanusha kuchelewa kutoa vibali uagizaji sukari

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

BODI ya Sukari Tanzania imekanusha taarifa za kuchelewa kutoa vibali vya uagizaji wa sukari nje unaofanywa na makampuni, badala yake baadhi ya kampuni zilichelewa zenyewe kuchukua vibali hivyo.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Bodi ya Sukari Tanzania, Profesa Kenneth Bengesi, alipokuwa akizungumza na waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam, kama njia ya kuelimisha jamii baada ya upotoshwaji wa makusudi uliofanywa na baadhi ya wadau wa sukari nchini hapa.

“Kampuni za wazalishaji zilipewa vibali kabla ya kampuni hizi wanazoziita kampuni za “vocha” ambazo zilipewa vibali baadae, tulipoona mwenendo wa uingizaji wa kampuni za wazalishaji sio mzuri.

Kampuni za wazalishaji zilipewa vibali vyake mapema mwezi Januari, wakati kampuni za wafanyabiashara zilipewa vibali mwisho mwa Januarina nyingine wakipewa vibali mwezi Aprili.

Alisema uamuzi wa Serikali kutoa vibali vya uagizaji wa sukari kwa kampuni nyingine za wafanyabiashara kulichangia kushusha bei ya sukari kwa kiasi kikubwa hali iliyoleta ahueni kubwa kwa wananchi.

“Ingawa kampuni hizi za wafanyabiashara zinadhihakiwa kuwa ni za vocha, hizi ndizo kampuni zilizoingiza sukari nchini kwa haraka katika kipindi kigumu cha upungufu mkubwa na kuifanya bei ya sukari ishuke,” alisema Profesa Bengesi.

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Sukari Tanzania inaonesha Kampuni za wafanya biashara zillifanikisha kuingizwa kwa sukari nyingi nchini ndani ya muda mfupi ikilinganishwa na kampuni za wazalishaji.

Ongezeko hilo lilifanikisha kushusha bei sukari nchini kutoka wastani wa sh. 7000 mwezi Februari hadi sh 2800 mwezi Juni.

Bodi ya Sukari iliamua kutolea ufafanuzi hoja za upotoshaji zilizotolewa na wadau wa sukari nchini Tanzania, kwa nia ya kuondoa hofu kwa wananchi na Watanzania kwa ujumla.