Na Mwandishi wetu;- Dar es Salaam
Serikali imeitaka Idara ya Uhamiaji kuendelea kuimarisha Misako na Doria za kuwabaini Wahamiaji wanaoshindwa kufuata sheria za nchi pamoja na uhalifu unaovuka mipaka.
Hayo yamesemwa leo Julai 5, 2024 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo wakati akizungumza katika Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Kamishna Jenerali wa Uhamiaji na Maafisa Waandamizi kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Baraza la Maaskofu Jijini Dar es Salaam.
Mhe. Sillo amewasihi kuzidisha nguvu katika udhibiti kwa kuongeza Misako, Doria na ikiwezekana kuwepo na doria maalum ambazo zitashirikisha wadau mbalimbali na Vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama ili kuwaongezea nguvu kwani nchi ikiwa salama dhidi ya uhalifu itaendelea kuvutia uwekezaji na kuendelea kuwa kivutio kwa wageni.
“Kama tunavyofahamu nchi yetu inaelekea katika kipindi cha uchaguzi wa Serikali za mitaa pamoja na uchaguzi mkuu ni vema kuimarisha usalama katika vituo vyetu vyote vya kuingia na kutoka hapa nchini na tuhakikishe tunafanya ukaguzi wa mara kwa mara wa taasisi ambazo zimeajiri wageni hapa nchini ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa salama kabla na baada ya uchaguzi. Kwa kufanya hivyo nchi hii itaendelea kulinda heshima na nafasi yake katika tasnia ya kimataifa” Alisema
Aidha, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuitangaza nchi kwani matunda yake yameonekana hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha anatoa huduma nzuri katika vituo vyote vya kuingilia na kutokea wageni wote waliokidhi vigezo jukumu hilo litafanywa vyema na Idara ya Uhamiaji kutokana na kuwa na nafasi kubwa katika uimarishaji wa uingiaji wa wageni pamoja na uwekezaji nchini.
Awali Kamishna Jenerali wa Uhamiaji Tanzania CGI Dkt. Anna Makakala akisoma taarifa yake mbele ya Mgeni Rasmi wakati wa Ufunguzi wa Kikao Kazi chenye lengo la kupokea taarifa na kujadili masuala mbalimbali ya utendaji kazi pamoja na kuweka mikakati ya kuongeza ufanisi alimshukuru kwa dhati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwateuwa na kuwapandisha vyeo jumla ya Maafisa Waandamizi takribani 50 huku akiahidi kuendelea kusimamia vema maelekezo yote yanayotolewa na Serikali katika kuhakikisha mipaka ya nchi inakuwa salama.
Idara ya Uhamiaji itaendelea kusimamia misingi ya Sheria na kutoa Huduma Bora kwa Wananchi na Wageni ili kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais kwa kuimarisha Uchumi wa nchi yetu kupitia sekta ya Utalii na Uwekezaji.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Makamishna wa Uhamiaji, Maafisa Wandamizi kutoka Vitengo mbalimbali Makao Makuu, Maafisa Uhamiaji Mikoa yote Tanzania Bara na Visiwani sambamba na Maafisa kutoka katika Vituo vya kuingia na kutoka nchini.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria