November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaishukuru Canada kwa kuendelea kuipa misaada

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Tanzania imeishukuru Canada kwa misaada inayotoa kwa Serikali ambayo imekuwa ikiunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dr. Samia Suluhu Hassan.

Shukrani hizo zimetolewa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk (Mb) wakati wa kikao chake na Waziri wa Maendeleo wa Kimataifa wa Canada, Mhe Ahmed Hussein kilichofanyika katika Ofisi ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam leo Mei 15, 2024.

Balozi Mbarouk alisema kuwa Serikali ya Canada imekuwa mshirika mkubwa wa Tanzania katika sekta mbalimbali zikiwemo za afya, elimu, uwekezaji na biashara akitolea mfano wa msaada wa Dola milioni 15 uliotolewa na nchi hiyo kwa ajili ya uboreshwaji na uimarishwaji wa mifumo ya afya, hususan kuimarisha huduma za afya na vituo vya kutolea huduma za afya ya msingi nchini.

“Canada imekuwa mdau wetu mkubwa katika sekta ya afya nchini, imetupatia Dola za Canada zipatazo Milioni 15 kupitia mfuko wa bajeti ya afya, msaada huu unamaana kubwa kwa Tanzania, unasaidia sana kuboresha sekta ya afya nchini,” Balozi Mbarouk alisema.

Kwa Upande wa Waziri Hussein alimweleza Balozi Mbarouk kuwa Cadana imesaini mkataba wa Nishati safi katika Mkutano uliomalizika hivi karibuni nchini Ufaransa ikiwa ni ishara ya kuunga mkono nishati safi ya kupikia Afrika.

Aidha, alisema Canada inawekeza Dola milioni 20.5 katika Mpango wa Ustahimilivu wake, katika Sayari yetu kwa miaka sita.

Viongozi hao walihitimisha mazurngumzo yao kwa kuelezea kuridhishwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia uliopo baina ya nchi hizi mbili na kuahidi kuuimarisha zaidi kwa manufaa ya pande zote.