Na Mwandishi wetu, Timesmajira Online
NAIBU Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknokojia Prof. Caroline Nombo ametembelea kiwanda cha uchapishaji wa maandishi ya Breli kwa ajili ya wanafunzi wasioona cha TET -Press B, kilichopo Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo Prof.Nombo ameipongeza TET kwa kazi nzuri inayofanywa kupitia kiwanda hicho kwa kuchapa na kusambaza vitabu vya Breli kwa wanafunzi wasioona wa Elimu ya Msingi na Sekondari.
Aidha, aliwaongoza wafanyakazi kiwandani hapo kumtakia kheri ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia S. Hassan, kwa kumshukuru na kumpongeza Rais.
“Namshukuru sana Rais kwa kutoa kipaumbele kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum kwa kutoa fedha za kuchapa na kusambaza vitabu vya kiada vya sekondari vya wanafunzi wenye uoni hafifu na wasioona, kazi iliyofanywa na kiwanda hiki” amesema Prof.Nombo.Aidha,
Prof.Nombo alipongeza TET kwa kazi kubwa na nzuri ya uandaaji wa mitaala na vitabu, ameahidi kuwa serikali itaisaidia TET kukarabati kiwanda hicho ambacho ni kiwanda pekee nchini chenye kuchapa vitabu vya Breli.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu Fixon Mtelesi ameeleza kuwa pamoja na mafanikio mengi ya kiwanda hicho zipo baadhi ya changamoto zinazokikabili kiwanda hicho ambazo ni uchakavu wa miundombinu na upungufu wa watumishi.
Naye Mkurugenzi wa Utafiti, Habari na Machapisho-TET Kwangu M.Zabrone alimjulisha Prof.Nombo kuwa kiwanda hicho sasa kinakamilisha uzalishaji wa nakala 5460 za vitabu vya kiada vya Elimu ya Awali kwa maandishi ya Breli kwa ajili ya watoto 904 wasioona wa Elimu ya Awali ili kurahisisha ujifunzaji wao sawa na wenzao wasiokuwa na changamoto ya uoni.
Vile vile, Mkuu wa Kiwanda cha Press B Kibanda alieleza kuhusu mitambo ya kiwanda hicho alisema, anamshukuru Rais na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa kuwezesha ununuaji wa mitambo miwili ya kuchapa vitabu vya Breli iliyosaidia kutekeleza kazi katika kiwanda hicho.
More Stories
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba
TRA kuongeza idadi ya waendesha uchumi walioidhinishwa
TRA Tanga wajivunia ukusanyaji mapato