Na Penina Malundo,Timesmajira
WAZIRI wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,Jerry Silaa amesema serikali itaendelea kuimarisha uchumi wa kidijitali kukuza biashara mtandao na kuleta ajira nyingi kwa vijana hususan madereva wa pikipiki(bodaboda) kupitia mfumo wa usafirishaji wa vifurushi,mizigo na abiria.
Waziri Silaa aliyasema hayo leo Januari 24,2025 wakati akizindua mfumo wa usafirishaji wa Vifurushi,Mizigo na Abiria ujulikanao kwa jina la ”Swifpack”.
Amesema kupitia huduma hiyo itatoa fursa za kipato cha uhakika na kuifanya kazi ya bodaboda kuwa sawa na kazi nyingine za usafirishaji wa vifurushi,mizigo na abiria.
”Leo tunashuhudia hatua nyingine muhimu kwa Shirika la Posta Tanzania kupitia huduma ya Swifpack ambayo itawezesha upatikanaji wa huduma za usafirishaji wa vifurushi,mizigo na abiria kwa kasi ufanisi na gharama nafuu,”amesema na kuongeza
”Teknolojia inabadilisha namna ya tunavyofanya kazi na kuwasiliana na huu ni mfano bora wa jinsi taasisi za umma zinavyoweza kutumia ubunifu wa teknolojia kutibu mahitaji ya soko na kuboresha huduma kwa wananchi,”amesisitiza.
Aidha Waziri Silaa alieleza kuwa serikali inamatarajio makubwa na kwamba huduma hii itachangia kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu kazi za bodaboda ambazo mara nyingi zimekuwa zikipata sifa mbaya mitandaoni na kutajwa kwa changamoto mbalimbali za kijamii.
Waziri Silaa aliliagiza Shirika la Posta kuhakikisha kuwa linaimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa mizigo na vifurushi unafanya kazi kikamilifu,kutoa taarifa sahihi kwa wateja na kuongeza ushirikiano na sekta binafsi ili kuhakikisha huduma ili inahudumia wananchi wengi na inafika maeneo mengi zaidi nchini.
Awali akitoa salamu za Shirika la Posta Tanzania,Postamasta Mkuu,Macrie Mbodo alisema kuwa shirika hilo limeendelea kutekeleza mkakati wake wa nane wa biashara wenye dhamira ya kuifanya posta ya Tanzania kuwa posta ya Kidijitali kwa biashara endelevu.
”Moja ya mafanikio tuliyoyapata kupitia utekelezaji wa mkakati huu,tumefanikiwa kuunganisha huduma na biashara zetu kwenye programu tumizi inayojulikana kama posta kiganjani inayopatikana playstore na Apple Store ambapo kwa sasa kupitia programu hii mwananchi yeyote mwenye simu janja anaweza kufurahia huduma zetu za posta kiganjani mwake ikiwemo kufuatilia mzigo wake(tracking)kuomba na kufanya malipo ya huduma zetu mbalimbali,”amesema Mbodo.
More Stories
Kambi ya wanasheria Katavi kuwajengea uwezo wananchi
RAS Tanga aipongeza Lushoto DC kuvuka lengo mapato ya ndani
Baraza la Wafanyakazi Ofisi ya Mwanasheria Mkuu latakiwa kutoa huduma bora za kisheria