December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yagawa vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi katika Mikoa mitano

Na Hadija Bagasha, TimesMajira Online, Tanga

Serikali kupitia wizara ya afya na ofisi ya Rais Tamisemi imeandaa zoezi la kugawa vyandarua vyenye viuatilifu kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa Mikoa mitano ikiwemo Mkoa wa Tanga ili kuhakikisha kiwango cha maambukizi ya malaria kinapungua hadi kufikia asilimia sifuri ifikapo mwaka 2030.

Vyandarua hivyo vitatolewa kwa watoto wote wa shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba bila malipo.

Akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa zoezi la ugawaji wa vyandarua kwa wanafunzi wa shule za msingi 1083 zilizopo katika Mkoa Tanga, Mkuu wa Mkoa Tanga Omari Mgumba amesema kwamba jumla ya vyandarua 529,641 vinatarajiwa kugawiwa kwa wanafunzi.

Mgumba amesema hali ya kiwango cha ugonjwa wa malaria katika Mkoa Tanga ni asilimia 12.4% kikilinganishwa na Mikoa mingine nchini.

“Viwango vya maambukizi katika Mkoa vimetofautiana kati ya Halmashauri ambapo zipo Halmashauri zenye maambukizi yanayofikia asilimia 35.5% Handeni DC na TC na nyingine chini ya asilimia 1 (Lushoto na Bumbuli) kwahiyo bado tunalo jukumu kubwa kwa kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti ugonjwa wa malaria hadi kutokomeza kabisa kabla ya mwaka 2030,”alisema Mgumba.

Aidha kupitia ugawaji huo wa vyandarua Mgumba ametoa onyo kwa watu wanaotumia vibaya vyandarua vinavyogawiwa na serikali kwa matumizi yasiyokusudiwa ikiwemo kufugia kuku, kuvulia samaki na dagaa katika bahari na kueleza kuwa atakayebainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake licha ya kwamba vyandarua hivyo vimetolewa bure.

Mgumba pia amewaagiza viongozi wote wa kiserikali, dini na kijamii kusimamia ipasavyo matumizi sahihi ya vyandarua hivyo ili kuepuka matumizi yasiyotarajiwa kwa vyandarua yaliyopita.

Kwa upande wake Meneja wa bohari ya dawa MSD Mkoa wa Tanga Siti Abdulrahman amesema kuwa vyandarua hivyo vinatolewa kwa wanafunzi wote wa shule za msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba bila malipo.

Meneja Siti amesema lengo la kufanya hivyo ni kuhakikisha kiwango cha maambukizi ya ugonjwa wa malaria kinapungua hadi kufikia asilimia 0 ifikapo 2030.

Hashim Mgandilwa ni Mkuu wa wilaya ya Tanga amesema takwimu za Malaria katika wilaya ya Tanga zimekuwa zikishuka kila mwaka kwani takwimu zilizopita walikuwa na wastani wa asilimia 17.3 ambapo hivi sasa wastani umeshuka na kufikia asilimia 14.7.

Mgandilwa ameahidi kupita nyumba kwa nyumba ili kukagua matumizi halisi ya vyandarua vilivyogawiwa.

“Tutapita nyumba nyumba kwa nyumba maana Mkuu wa wilaya kwa nafasi yake ana uwezo wa kuingia popote tutaingia mpaka vyumbani kukagua kama hivi vyandarua vinatumika na nikuhakikishie tu Mkuu wa Mkoa kwamba nitakwenda kulitekeleza hili, “alisisitiza Mgandilwa.

Usambazaji wa vyandarua hivyo utafanyika katika Halmashauri 11 ndani ya siku 45 kazi ambayo itafanywa na bohari ya dawa kwa kushirikiana na Halmashauri husika.

Usambazaji huo umeanza katika jiji la Tanga na utaendelea katika Halmashauri za Korogwe, Muheza, Mkinga, Pangani, Handeni, Kilindi, Lishoto na Bumbuli.