January 4, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yagawa injini za boti kwa vyama vya wavuvi

Na Mbaraka Kambona,TimesMajira Online,Kagera

KATIKA kuhakikisha shughuli za wavuvi zinaboreshwa ili kukuza kipato chao, Serikali imegawa Injini za Boti nne (4) aina ya Yamaha zenye thamani ya shilingi milioni 35 kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi vinne vinavyofanya shughuli zao katika Ukanda wa Ziwa Victoria.

Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi(Uvuvi), Dkt.Rashid Tamatamah (kulia) akikabidhi injini ya boti kwa Kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika wa Wavuvi, Zilagula, Agness Mbasha katika hafla fupi ya kugawa Injini za boti kwa Vyama vya Ushirika vya Wavuvi Kanda ya Ziwa Victoria iliyofanyika katika Wilaya ya Muleba, Mkoani Kagera

Wakati akikabidhi Injini hizo kwa Wavuvi Wilayani Muleba Mkoani Kagera jana, Katibu Mkuu,Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi),Dkt.Rashid Tamatamah alisema kuwa ugawaji wa injini hizo ni katika kutekeleza moja ya majukumu ya Wizara ya kuhakikisha wanawezesha upatikanaji wa utaalamu,rasilimali fedha na vitendea kazi ili kuwasaidia Wavuvi kuboresha kazi zao na kuendeleza sekta ya uvuvi kwa ujumla.

Dkt.Tamatamah alisema kuwa katika kuhakikisha Vyama vya Wavuvi vinawezeshwa, mwaka wa fedha 2020/ 2021 Wizara ya Mifugo na Uvuvi imetenga shilingi milioni mia mbili (200,000,000) kwa ajili ya kuviwezesha vyama vya Ushirika vya Uvuvi na Ukuzaji Viumbe maji.

“Rai yangu kwa Vyama hivi vya Ushirika wazitumie injini hizi kwa kufanya uvuvi endelevu na kuachana na uvuvi haramu”, alisema Dkt. Tamatamah.

“Nawahamasisha pia wavuvi wajiunge katika vikundi vya ushirika ili iwe rahisi kuwezeshwa kwa mikopo na vitendea kazi ili waweze kujikwamua kiuchumi”,aliongeza Dkt.Tamatamah.

Kuhusu mwitikio wa Wavuvi kujiunga na vyama vya ushirika,Dkt.Tamatamah alisema kuwa muitikio ni mzuri na Wilaya ya Muleba imekuwa kinara wa kuanzisha vyama hivyo.

Akiongea baada ya kupokea Injini ya Boti,Mwakilishi wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi,Izigo, Wilayani Muleba, Naziru Kassanga alisema kuwa Injini hiyo ya Boti waliyopatiwa itawasaidia sana wao kama wavuvi wadogo wadogo kufanya uvuvi wa kisasa utakaowasaidia kuboresha maisha yao.

“Injini hii itatusaidia sisi wavuvi wadogo kwenda kuvua katika kina kirefu kwa urahisi na kuondokana na uvuvi wa kienyeji ambao tija yake ni ndogo”, alisema Kassanga.

Naye, kaimu Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika cha Wavuvi cha Zilagula, Wilayani Buchosa,Agnes Mbasha aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwakabidhi boti ambayo anasema itawasaidia kufanya doria ya kulinda nyavu zao dhidi ya wezi.

“Nitumie nafasi hii pia kuwahamasisha wanawake wenzangu kujiunga na Vyama hivi vya Ushirika kwani vinasaidia sana kujikwamua kimaisha”,alisema Mbasha
Kuhusu vyama vya ushirika kuunganishwa na taasisi za fedha, Dkt.Tamatamah alisema mikopo iliyoombwa na kupitishwa kwa ajili ya vyama vya ushirika ni shilingi bilioni 2.6 na ambayo tayari imeshatolewa ni shilingi milioni 873.8 na vyama 14 viko katika hatua za mwisho kupatiwa mikopo.

“Wizara imeihamasisha Benki ya Posta Tanzania (TPB) kuzindua akaunti ya Wavuvi (Wavuvi account) kwa ajili ya mikopo na bima mahususi kwa Wavuvi hususani wavuvi wadogo”,alifafanua Dkt. Tamatamah
Mwisho.