December 28, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaendelea kubuni mikakati kuinua uchumi kwa vijana

Na Jackline Martin, TimesMajira Online

Serikali ya Tanzania imeendelea kubuni mikakati mbalimbali ambayo itaiwezesha nchi kutumia fursa ya kiteknolojia zilizopo katika kuinua uchumi wa nchi ambapo imetoa fursa ya mafunzo ya ujuzi wa kujiajiri au kuajiriwa kwa vijana 118,415

Imeelezwa kuwa, tangu kuanza kwa programu hiyo ya Taifa ya kukuza ujuzi, vijana katika fani mbalimbali wamenufaika kupitia mafunzo hayo ambayo ni ya uanangezi , ufugaji wa samaki na viumbe maji, kilimo cha kisasa na ukarimu.

Hayo ameyasema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati akizindua Mradi wa Kuwezesha Vijana Kielimu na Kiuchumi kupitia KCB 2jiari wa KCB Foundation na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ) katika ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere, leo jijini Dar es Salaam.

“Tunatambua kuwa ajira ni changamoto iliyopo duniani kote lakini kila nchi ina mkakati wake, Tanzania moja ya mkakati ni huu wa kuwapa ujuzi vijana kila mmoja aweze kushiriki katika ahughuli za kujiletea uchumi ili iwe sehemu ya ajira”

waziri Mkuu Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia amekuwa kinara katika mkakati wa kupambana na changamoto za ajira, ameendelea kutoa wito wa uwekezaji nchini ambapo wanatarajia kupata wawekezaji watakaojenga viwanda, watakaoshiriki uchimbaji wa madini, watakaoshiriki kwenye kilimo cha mashamba makubwa na wazalishaji kutoka ndani ya nchi.

Kutokana na hivyo, Waziri Mkuu Majaliwa ametoa wito kwa wawekezaji wote ndani na nje ya nchi kuendelea kutumia fursa zilizopo ndani ya nchi ili kuwekeza na kutumia nguvukazi za watanzani ambayo moja ya nguvu kazi hiyo ni mradi huo wa kusaidia vijana katika Maendeleo endelevu.

“Suala la uwezeshwaji kwa vijana ni muhimu sana katika kukuza uchumi , hii inatokana na ukweli kwamba vijana ndiyo nguvu kazi wa Taifa hili”

“Serikali tuna matumaini makubwa kwa mkakati huu mlionao ndani ya Benki na kutafuta wadau kuongeza nguvu yenu ili muwafikie vijana wote nchini” Amesema Waziri Mkuu Majaliwa

Pia amesema hadi sasa serikali imejenga vyuo vya ufundi (VETA) kila wilaya ambapo wameanza kwa Wilaya 28 na wanatarajia kujenga zaidi ya 28 lengo ikiwa ni kuweza kufikia halmashauri zote 183 ili kila wilaya kuwe na chuo cha ufundi kitakachowawezesha vijana kupata elimu ya ufundi.

Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali itaboresha huduma za utafiti na mafunzo taaluma ya mifugo pamoja kuanzisha kuendeleza vituo atamizi Vya wawekezaji kwenye maeneo ya mifugo.

Kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana, Waziri Mkuu Majaliwa amesema serikali imeendelea kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 1.88.

Aidha, Waziri Majaliwa amewataka vijana waendelee kujitokeza kwa wingi na kuchangamkia fursa za uwepo wa mradi mbalimbali ya kuinua vijana kiujuzi na kiuchumi.

Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Prof. Joyce Ndalichako amesema kuwa mradi huo ni muhimu kwa kuwa unagusa moja kwa moja vijana ambao ni moja ya nguzo muhimu ya maendeleo ya Taifa.

“Mradi huu wa kuwainua vijana kiuchumi na kiujuzi tukiutekeleza ipasavyo, tutakuwa tumeinua Taifa kimaendeleo na kuimarisha uchumi wa Taifa letu”

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Benki ya KCB, Paul Russo amesema
Benki ya KCB, kupitia Taasisi yake inafuraha kuungana na GIZ ili kutoa mchango wa kudumu katika maendeleo ya uchumi wa Tanzania kupitia vijana katika sekta ya ujenzi.

“Hii ni kwa sababu wanatambua nafasi ya vijana katika kuleta mabadiliko ya uchumi na jinsi sekta ya ujenzi ilivyo muhimu katika kukuza ukuaji wa Tanzania kupitia athari zake za kuzidisha sekta nyingine.”

Amesema Benki pia inatoa msaada mbalimbali kwa jamii katika sekta za afya, elimu, mazingira, na watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na vituo vya watoto yatima.

” Maeneo mengine ya msaada ni majanga ya kitaifa kama vile msiba wa MV Nyerere katika Ziwa Victoria mwaka 2018, ambapo benki hiyo ilitoa TZS 125 milioni.”

“Kiuchumi, Benki ya KCB Tanzania inashiriki kikamilifu katika uboreshaji wa miundombinu ya nchi kwa kufadhili miradi ya Serikali kupitia wateja wake wanaokopa.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB, Cosmas Kimario amesema lengo la mradi huo wa ‘2Jiajiri’ ulioanzishwa mwaka 2000 ni kuboresha ajira na biashara kwa wanawake na vijana nchini na kupunguza mawazo ya vijana kuajiriwa.

“Kupitia mradi huu vijana na wanawake, 1,780 wamenufaika na kwa mwaka huu tunatarajia kufikia vijana takriban 5,000,” amesema.

Pia amesema Programu hiyo ya 2jiajiri imekua na mabadiliko chanya mwaka hadi mwaka ambapo mwaka 2019 – 2018, wanawake 315 wamiliki wa biashara ndogondogo walifaidika kwa kupatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa siku tano mfululizo darasani na baada ya hapo, KCB iliwapatia maafisa watuta wa benki akiwemo afisa masoko, akauntanti na mwanasheria kuwapa mafunzo elekezi ndani ya biashara zao ili kuhakikisha walichofundishwa darasani wanakitumia kwenye biashara zao.

Aidha amesema Mwaka 2019 – 2020, vijana 163 (118 walihitumu vizuri) walipewa ufadhali wa 100% kusoma kozi mbalimbali katika chuo cha VETA, na baadae kusimamaiwa kuanzisha na kuendesha biashara zao ambapo hadi leo KCB Bank Tanzania ni mlezi wa hawa vijana.

Pia amesema Mwaka 2021, vijana 304, walipatiwa mafunzo ya ujasiriamali kwa ushirikiano wa KCB Bank Tanzania na baraza la uwezeshaji la taifa (NEEC).

“Mwaka 2021 -2023 vijana 960 wamenufaika kwa kwa ushirikiano kati ya KCB Bank Tanzania kupitia KCB Foundation na GIZ kupitia mpango wa 2jiajiri/E4D ambapo
Mwaka 2023, KCB Bank itawezesha vijana 5000 kwa kuwasomesha kozi mbalimbali kupitia VETA.” Alisema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania, John Ulanga amesema kwa sasa KCB Bank inashirikiana na katibu tawala wa mikoa mbalimbali katika kuona jinsi gani wanaweza kushirikiana katika kuwaendeleza vijana hao zaidi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza wakati wa uzinduzi mradi wa Kuwawezesha Vijana Kielimu na Kiuchumi kupitia KCB Foundation na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ), katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Aprili 16, 2023.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipewa maelezo na Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Benki ya KCB, Christina Manyenye kuhusu vifaa vilivyotolewa kwa ajili ya vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi kupitia mradi wa kuwawezesha vijana Kielimu na Kiuchumi kupitia KCB Foundation na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ), kwenye uzinduzi wa mradi huo uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Aprili 16, 2023.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Swaumu Bakari vifaa vya ujenzi baada ya kuhitimu mafunzo ya ufundi kupitia mradi wa kuwawezesha vijana Kielimu na Kiuchumi unaofadhiliwa na KCB Foundation na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ), wenye uzinduzi wa mradi huo uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Aprili 16, 2023.
 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akimkabidhi Frank Ferdinand vifaa vya ujenzi baada ya kuhitimu mafunzo ya ufundi  kupitia mradi wa kuwawezesha vijana Kielimu na Kiuchumi unaofadhiliwa na KCB Foundation na Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Ujerumani (GIZ), wenye uzinduzi wa mradi huo uliofanyika katika ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere, Aprili 16, 2023.