January 20, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yadhamiria kutekeleza Mradi wa Liganga na Mchuchuma

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb.)ameihakikishia Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuwa Serikali imedhamiria kutekeleza Mradi wa Kimkakati wa Liganga na Mchuchuma kwa manufaa ya Taifa kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Kijaji amewahakikishia wajumbe hao kuwa Serikali imekamilisha kuhakiki ardhi na mali za wananchi watakaopisha Mradi na imejipanga kulipa fidia kwa wakazi wa maeneo ya mradi huo ili kurahisisha utekelezaji wa mradi huo kuanza.

Dkt. Kijaji ameyasema hayo wakati wa Semina ya kuwaelimisha Wajumbe wa Kamati hiyo kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Liganga na Mchuchuma, Februari 09, 2023, Bungeni, Jijini Dodoma.

Wakichangia kwa nyakati tofauti Wajumbe wa Kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati, Mhe. David Mwakiposya Kihenzile wamesema Mradi huo wa Kimkakati unapaswa kuanza kutekelezwa mapema iwezekanavyo ili kuleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Vilevile, Wajumbe wa Kamati hiyo walitoa maoni na mapendekezo mbalimbali yaliyolenga kusaidia jitihada za kukamilisha taratibu za kuanza kutekeleza Mradi huo kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.

Naye, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Dkt. Hashil Abdallah aliieleza Kamati hiyo kuwa utekelezaji wa Mradi huo wa Kimkakati utafuata taratibu na Sheria zinazosimamia Uwekezaji, Madini, Kodi na Raslimali za nchi zilizopo ili kuhakikisha Mradi huo unaleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.

Naye, Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) Dkt. Nicolaus Shombe akitoa elimu kwa wajumbe hao amesema NDC inatekeleza miradi ya kielelezo (Flagship projects) na miradi ya
kimkakati ikiwemo Mradi unganishi wa Mchuchuma na Liganga, Mradi wa chuma ghafi wa Maganga Matitu na Makaa ya Mawe Katewaka na Ngaka iliyopo pamoja na miradi mingine iliyopo nchini.

WAZIRI wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ,akizungumza wakati wa Semina ya kuwaelimisha Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira kuhusu utekelezaji wa Mradi wa Kimkakati wa Liganga na Mchuchuma, iliyofanyika leo Februari 09, 2023, Bungeni, Jijini Dodoma.