January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaandaa mpango kabambe wa kitaifa wa hifadhi na usimamizi wa mazingira

Na Mwandishi wetu,timesmajira

Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais imeandaa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2032) kwa lengo la kutoa mwongozo wa hatua za kuchukua ili kutatua changamoto za mazingira nchini kwa kuzingatia upekee wa changamoto katika sehemu husika na hatua mahsusi zinazopaswa kuchukuliwa.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira),Khamis Hamza Khamis leo wakati wa mjadala ulioandaliwa na Benki ya Dunia kuhusu jitihada za Tanzania katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi ikiwa ni sehemu ya mijadala katika Mkutano wa 27 wa Nchi Wanachama wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea Sharm El-Sheikh, Misri.

Amesema mpango kambambe huo unaonesha changamoto za mazingira zinazoikabili Tanzania ikiwa ni pamoja na uharibifu wa ardhi; uharibifu wa vyanzo vya maji; athari za mabadiliko ya tabianchi; uchafuzi wa mazingira; ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu; upotevu wa makazi ya wanyamapori na bioanuai.

“Uharibifu wa mfumo-ikolojia ya pwani na baharini; uharibifu wa ardhi oevu; usimamizi hafifu wa taka; kuenea kwa viumbe vamizi; na changamoto za mazingira katika miji zimeanishwa katika Mpango huo,” amesisitiza Naibu Waziri Khamis.

Amesema Mpango Kambambe unatoa hatua za kimkakati na mahsusi kwa kuzingatia jiografia na mifumo ikolojia ya maeneo husika.

Hatua hizo zinazingatia utofauti wa mtawanyiko wa changamoto za mazingira na hatua muafaka zinazopaswa kuchukuliwa na kutoa mwongozo kuhusu usimamizi wa mazingira.
Naibu Waziri Khamis amesema kupitia ufadhili wa shirika la Umoja wa Mataifa la Mfuko wa Uendelezaji Mitaji (LoCAL), serikali imeanza kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika  halmashauri tatu za Kondoa, Chamwino na Mpwapwa pamoja na kujenga uwezo wa kitaasisi wa kuhuisha masuala ya mabadiliko ya tabianchi.
 
Ametoa wito kwa jamii kuhakikisha zinaendelea kutunza na kuhifadhi mazingira kwa kuwa Mabadiliko ya Tabianchi ni halisi na kusisitiza utekelezaji wa Sera na Mikakati kwa pamoja kwa kesho iliyo bora kwa kizazi cha sasa na kijacho. Aidha, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi nchini.

Itakumbukwa Mpango Kabambe wa Hifadhi ya Mazingira ulizinduliwa Juni 5, 2022 na Waziri Mkuu wa Tanzania,Kassim Majaliwa kwa niaba ya Makamu wa Rais wa Tanzania,Dkt. Philip Isdor Mpango.