Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Mary Maganga amesema Serikali imeandaa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira ambao utatekelezwa kwa kipindi cha miaka 10 na kuainisha changamoto za kimazingira na mikakati ya kukabiliana nazo kwa kuzingatia utofauti wa maeneo mbalimbali.
Bi, Maganga ameyasema haya leo 13 oktoba, 2022 katika Mkutano kati ya Ofisi ya Makamu wa Rais na Washirika wa Maendeleo katika kikao kilichofanyika katika Ukumbi wa Benki ya Tanzania, jijini Dar es salaam.
“Ofisi ya Makamu wa Rais imeona ni busara kuitisha mkutano huu kwa nia ya kushirikisha wadau hawa maendeleo jitihada ambazo Serikali inafanya na kuainisha maeneo ambayo tunahitaji kushirikiana nao kwa karibu zaidi hasa katika maeneo yenye changamoto za mazingira kwa kutumia Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira” Alisisitiza Bi. Maganga
Amesema mkutano huo utatumika kuweka mikakati ya kupanga, kufadhili na kutekeleza afua za kimkakati ili kutatua changamoto zilizoainishwa na kuendeleza ushirikiano wa muda mrefu katika maeneo ya uhifadhi na usimamizi wa mazingira kati ya Serikali na wadau wa Maendeleo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Khamis Shaban alipongeza Ofisi ya Makamu wa Rais kwa jitihada zake katika kusimamia uhifadhi wa mazingira.
Alisema kuzinduliwa kwa Mpango Kabambe wa Mazingira ni hatua ambayo itachochea katika kupata fedha za kusaidia katika hifadhi ya mazingira.
“Hata hivyo, Serikali inaendelea kujipanga kuhakikisha changamato za kimazingira zinatatuliwa kwa kupanga bajeti kupitia wizara zake,” alisema Naibu katibu Amina.
Kwa upande mwingine Bw. Zlatan Milisic, Mwakilishi mkazi wa Umoja wa Mataifa na Mwenyekiti wa Kundi la washirika wa Maendeleo nchini (Development Partners Group on Environment, DPG) amesema kwa kushirikiana na wadau wenzake wako tayari kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha utekelezaji wa Mpango Kabambe wa Kitaifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022-2023)
Mpango Kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira Mpango kabambe umeainisha changamoto 12 za mazingira zinazoikabili nchi ikiwa ni pamoja na uharibifu wa ardhi; uharibifu wa vyanzo vya maji; athari za mabadiliko ya tabianchi; uchafuzi wa mazingira; ukataji ovyo wa miti na uharibifu wa misitu.
Changamoto zingine ni upotevu wa makazi ya wanyamapori na bioanuai; uharibifu wa mfumo-ikolojia ya pwani na baharini; uharibifu wa ardhi oevu; usimamizi hafifu wa taka; kuenea kwa viumbe vamizi; na changamoto za mazingira katika miji.
Ili kupata ufumbuzi wa changamoto hizo Mpango Kambambe umeainisha hatua za kimkakati na mahsusi kwa kuzingatia jiografia na mifumo ikolojia ya maeneo husika.
More Stories
Rehema Simfukwe atoboa siri sababu kuimba wimbo wa Chanzo
Tanzania ipo tayari kupokea wakuu wa nchi,mkutano wa nishati-Dkt.Kazungu
Chunya yafikiwa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano