Na Mwandishi wetu,Timesmajira
SERIKALI kupitia Wizara ya Nishati imeziagiza taasisi za serikali kuanzia ngazi za chini pamoja na wadau mbalimbali kuongeza kasi ya kuhamaisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia ili kutimiza lengo la kufikia asilimia 80 ya matumizi hayo ifikapo 2030 ambapo kutasaidia kutunza mazingira pamoja na kulinda afya kwa jamii.
Waziri wa Nishati,Deogratius Ndejembi amesema hayo jana mkoani Morogoro wakati akizungumza katika Kongamano la Wadau wa Nishati,ambalo limelenga kujadili kuimarisha matumizi ya Nishati safi ya kupikia kwa maendeleo endelevu ya Tanzania,ambalo liliandaliwa na Taasisi ya Uongozi(Uongozi Institute)kwa kushirikiana na Wizara ya Nishati.
Akizungumza katika kongamano hilo,Waziri Ndejembi amesema kuwa Tanzania imefanya jitihada kubwa katika kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kuweza kufikia asilimia 23 katika kipindi cha miaka miwili huku akisema kuwa bado suala hilo linakabiliwa na changamoto kwa jamii kuendelea kutumia kuni na mkaa kunakosababisha uharibifu wa mazingira pamojana kuhatarisha afya zao.

“Napenda kusisitiza na kutoa maelekezo mahsusi kwa taasisi zote za serikali,Mamlaka za serikali za mitaa,sekta binabifsi na wadau wa maendeleo kuongeza kasi ya utekelezaji wa mipango ya kuhamasisha na kuwezesha matumizi ya Nishati safi ya kupikia hapa nchini”amesema Waziri Ndejembi
Aidha Waziri Ndejembi amesema kuwa upo umuhimu wa kuendelea kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa sera na programu ili kupanua miundombinu ya usambazaji wa umeme na gesi,kubuni mifumo rafiki ya kifedha kwa kaya zenye kipato cha chini,na kuendeleza kampeni za kitaifa za kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Akizungumza katika kongamano hilo,Afisa Mtendaji mkuu wa Taasisi ya Uongozi bwana Kadari Singo amesema kuwa Matumizi ya nishati safi ya kupikia yanamchango mkubwa katika kulinda afya na mazingira,ambapo kupitia jukwaa hilo walijadili mada mbalimbali ambazo zitaweza kusaidia jamii pamoja na serikali kwa ujumla kupiga hatua katika matumizi ya nishati safi ya kupikia.
“Kongamano hili lina malengo makuu matatu la kwanza ni kukuza uelewa wa wakiafya,Kimazingira na Kiuchumi na teknolojia ya Nishati safi ya kupikia,lapili kuhamasisha ushirikiano baina ya serikali,sekta binafsi na asasi za kiraia ili kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia”amesema Kadari Singo,Afisa Mtendaaji Mkuu wa Uongozi Institute.

Kwa upande wake mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Adamu Malima ametumia fursa hiyo kuiomba serikali kuangalia namna ya kuviwezesha vikundi vya wajasiriamali ambavyo vinajishughulisha na utengenezaji wa mkaa mbadala kwa kutumia mapumba ya mpunga,ombi ambalo limepatiwa majibu na Waziri wa Nishati ambae ameagiza jambo hilo kufanyiwa kazi mara moja.
Kongamano kuhusu kuboresha matumizi ya nishati safi ya kupikia kwa maendeleo endelevu Nchini Tanzania yanalenga katika kuhakikisha kuwa asilimia 80ya Watanzania wanatunia nishati safi yakupikia ifikapo mwaka 2034.




More Stories
TANESCO yazindua ndege nyuki kuboresha ukaguzi miundombinu ya umeme nchini
Dkt.Tulia awagusa waislam wasiojiweza kuelekea Idd
Kamati ya Bunge ya Miundombinu yaipongeza TTCL,Kituo cha ukusanyaji wa data kwa utendaji kazi wake