Na Judith Ferdinand,TimesMajira Online,Misungwi
WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki ameagiza eneo la shamba la uzalishaji mifugo lililopo wilayani Misungwi mkoani Mwanza kulindwa na Suma JKT,Polisi pamoja na kujengewa fensi( uzio),ili kuimarisha ulinzi na usalama wa eneo hilo.
Hii ni baada ya Waziri huyo kufanya ziara jana ya kutembelea shamba la Mabuki pamoja na taasisi zilizomo ndani yake ambapo alielezwa kuwepo kwa uchungaji haramu na uchomaji moto pamoja na tishio la usalama kwa wanafunzi na watumishi katika shamaba hilo.
Ndaki amesema,eneo hilo ni kubwa na lipo wazi kwa hali hiyo siyo salama kila mtu anaweza kuingia na kufanya jambo lolote hivyo waangalie uwezekano wa kuweka fensi ili mtu atakaye bomoa na kuingia itakuwa rahisi kumdhibiti.
Amesema,eneo hilo linapaswa kulindwa na Suma JKT,hivyo alimuagiza Mkurugenzi wa Utafiti ,Mafunzo na Ugani kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt.Angello Mwilawa pamoja na uongozi wa kituo hicho kukaa pamoja na kuangalia ni walinzi wa ngapi wanahitajika kwa ajili ya ulinzi wa shamba hilo.
Pia amesema katika suala la kuwalipa Suma JKT ni la wote Wizara na kituo hicho ambapo wanapaswa kuangalia namna ambayo watakuwa wanawalipa.
Aidha katika kuimarisha zaidi ulinzi wa eneo hilo amemuomba Mkuu wa Wilaya ya Misungwi awapatie Askari Polisi ambao watakuwa wanafanya kazi angalau siku mbili kwa wiki kwa ajili ya kuzungukia eneo hilo.
“Hatuwezi kuangalia wanafunzi na watumishi wapo hatarini,halfu sisi tunanyoosha mikono na kusema Mungu tusaidie na vitendo vya waangalizi wa ng’ombe,wanafunzi na watumishi kupigwa siyo sawa hivyo,tutafute pesa popote fensi ijengwe kama mwanzo,eneo hili lilindwe na Suma JKT na Polisi ili wavamizi wajue kuwa linalindwa,” amesema Ndaki.
Awali Kaimu Meneja wa Wakala wa Mafunzo ya Mifugo(LITA) kampasi ya Mabuki Joel Ngogo,akisoma taarifa kwa Waziri huyo, amesema Juni 9,2020 wanafunzi wao wakiwa shambani kukata fito za kujengea uzio wa ng’ombe walivamiwa,walipigwa na jaribio la kutaka kubakwa mwanafunzi mmoja wa kike ambaye aliokolewa na watu waliopita eneo hilo.
Ngogo amesema, Aprili 23,mwaka huu matukio ya wanafunzi kuvamiwa na kupigwa kwa kombeo wakiwa eneo la kantini( mgahawa) wakipata chakula yalirudiwa na wavamizi wanaodhaniwa kutumwa na wafugaji ambao mifugo yao ilikamatwa na uongozi wa shamba hilo.
Amesema katika kutatua changamoto hiyo alimuomba Waziri kusaidia kuoata ulinzi thabiti kwa kutumia makampuni ya ulinzi kwa kushirikiana na jeshi la Polisi.
Kwa upande wake Meneja wa shamba la uzalishaji mifugo Mabuki Lini Andey Mwalla,amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya uchungaji haramu wa mifugo ya wananchi kutoka sehemu mbalimbali.
Hali hiyo imekuwa ikivuruga malengo yaliyokusudiwa na serikali na kusababisha athari ikiwemo kueneza magonjwa ya virusi na yaenezwayo na kupe hivyo kusababisha vifo vingi vya mifugo vitokanavyo na magonjwa kama ndigana kali na mengineyo.
Pia amesema,suala la uchomaji moto hususani kipindi cha kiangazi kinachofanywa na watu ambao bado hawajawabaini kutokana na mbinu wanazotumia wahusika limekuwa likisababisha uharibifu wa mazingira na hivyo mifugo kukosa malisho.
More Stories
Kongamano la Uwekezaji kati ya Tanzania na Ubelgiji lafanyika Dar
CCM kuhitimisha kampeni kwa kishindo
Walimu elimu ya lazima watatakiwa kuwa wabobezi kwenye masomo wanayofundisha