Na Tiganya Vincent,TimesMajira Online, Tabora
NAIBU Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amemwagiza Katibu Tawala Mkoa wa Tabora Msalika Makungu kuwaondoa watumishi wote wa Manispaa ya Tabora ambao wamejimilikisha mashamba katika mradi wa Umwagiliaji wa Inala.
Amesema wamechukua maeneo hayo na kusababisha wananchi wanaozunguka mradi huo kukosa mashamba kwa ajili ya kulima kilimo cha mpunga.
Bashe ametoa kauli hiyo jana wakati wa kufungua maadhimisho ya sherehe za siku ya Ushirika Duniani (SUD) ambapo Kitaifa inafanyika Mkoani Tabora na kilele kitakuwa tarehe 3 Julai mwaka huu.
Amesema licha ya Serikali kutumia fedha nyingi kujenga Bwawa hilo bado mradi huo haufanyikazi vizuri kama ulivyokusudiwa kwa sababu ya watumishi wa Manispaa ya Tabora kujimilikisha mashamba ambayo hawayalimi.
Katika hatua nyingine Naibu Waziri huyo amemwagiza Mrajis wa Vyama Vya ushirika Nchini Dkt. Benson Ndiege kufanya miaka mitatu mfululizo maadhimisho ya sherehe za siku ya Ushirika Duniani (SUD) katika Mkoa mmoja badala ya kila mwaka kuanga katika eneo jipya.
Amesema hali hiyo itasaidia kuleta matokeo chanya kutokana na Washirika kujifunza katika eneo mmoja kwa kipindi cha miaka mitatu.
Wakati huo Naibu Waziri amewataka vijana kujiunga na ushirika ili kuondoa dhana potofu kuwa Ushirika na wazee na watu waliochoka.
Amesema ushirika ndio silaha pekee itakayowasaidia wakulima kupanga katika masoko na kupata bei nzuri itakayowasaidia kuondoa katika umaskini.
Bashe amesema Serikali itaendelea kuunga mkono Ushirika ili hatimaye uweze kuwa msaada mkubwa kwa wakulima kuchangia katika pato la Taifa kutoka la sasa la asilimia 26 na kuongezeka Zaidi.
Amesema kilimo ndio Sekta inayotoa ajira kwa wananchi wengi ni vema ikachangia kwa kiasi kikubwa katika pato la Taifa.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku ya ushirika Duniani mwaka huu ni Ushirika pamoja tujijenge uya kwa ubora na tija.
More Stories
Benki ya Equity Tanzania yasaini mkataba wa kuwawezesha wanawake kiuchumi
Rais Samia alivyoguswa kifo cha msanii Grace Mapunda
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta