Na Penina Malundo,Timesmajiraonline,Dar
MEI Mosi ni Siku ya Wafanyakazi Duniani. Ni tarehe ambayo inaadhimishwa na wafanyakazi kukumbushana mapambano ya kihistoria na maendeleo yaliyofanywa na wafanyakazi kote ulimwenguni kudai haki zao.
Kila mwaka,ifikapo siku hiyo vyama vya wafanyakazi vya umma na binafsi udhimisha kwa njia mbalimbali ikiwemo kutumia maandamano kudai kudai haki zao, ikiwemo na mazingira bora ya kazi.
Hivyo Mei Mosi ni siku ya kutambua mchango wa wafanyakazi katika kuleta mabadiliko na kuboresha mazingira ya kazi ulimwenguni na kuhakikisha wanaenziwa kwa kuwaunga mkono na kuwaenzi na kuwaunga mkono wafanyakazi katika harakati zao za kutetea haki zao.
Nchini Tanzania maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika mkoani Arusha na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali, viongozi wa dini, Serikali na Taasisi na vyama vya Wafanyakazi.
Mbali na hao pia maadhimisho hayo yamehudhuriwa na Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ambaye alimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, ambapo pamoja na mambo mengine amewatoa amewatoa hofu wafanyakazi nchini kwa kuwahakikishia mazingira bora ya kazi kwa wafanyakazi kama Mikataba ya Shirika ya Kazi Duniani inavyosema.
Anasema Serikali itaendelea kuhuisha viwango vya mshahara kwa kuzingatia uwezo wa kiuchumi na kibajeti pamoja na ujuzi na utendaji wa waajiriwa ili kuepuka kuchochea mfumuko wa bei, kuhatarisha uhimilivu wa deni la Taifa na athari nyingine kwenye utulivu wa uchumi wa Taifa kwa ujumla.
Dkt. Mpango anasema changamoto mbalimbali ambazo zimeikumba dunia ikiwemo vita na majanga ya asili zimeendela kuathiri uchumi wa Taifa kutokana na kuvurugika kwa mfumo wa ugavi na kupanda kwa bei za mafuta, mbolea, chuma na chakula.
Anasema pamoja na changamoto hizo tathmini ya Serikali na ya Taasisi za kimataifa ikiwemo IMF, Benki ya Dunia, AfDB, Moody’s, Fitch,zimeonesha kuwa uchumi wa Taifa umekuwa stahimilivu kwa kiasi cha kuridhisha hivyo hali hiyo itakapoendelea kudumu wafanyakazi wawe tayari kunufaika.
“Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa namna mbalimbali, ikiwemo kwa kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara ambapo Mwaka 2023/24 kiasi cha shilingi bilioni 153.9 kililipwa na kwa mwaka 2024/25,”anasema na kuongeza
”Serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 150.8 kwa ajili hiyo na pia imeendelea kuwapandisha vyeo watumishi mbalimbali, ambapo mwaka 2023/24 jumla ya watumishi 81,515 walipandishwa vyeo na mwaka 2024/25,”anasema.
Anasema serikali imetenga kiasi cha sh. bilioni 252.7 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 219,924 na pia inathamini na kupokea hoja ya kuboresha Kanuni ya ukokotoaji wa mafao ambapo suala hilo ni la sayansi ya Watakwimu-bima ambalo litashauriwa kwa kuzingatia uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Halikadhalika katika risala yake,Dkt. Mpango anasema likizo ya uzazi ni haki ya mfanyakazi na iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto njiti, kipindi cha uangalizi maalumu hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi.
Anasema vilevile mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha.
”Serikali ipo katika hatua ya kuifanyia marekebisho Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini, Sura 366 ili likizo ya uzazi ianze pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum kadri madaktari watakavyothibitisha,”anasema na kuongeza
”Anatoa wito kwa wafanyakazi nchini kuendelea kutekeleza majukumu kwa bidii, maarifa, uadilifu kwa kutanguliza maslahi ya Taifa mbele kwa kuongeza tija katika utendaji kazi,”anasema.
Pia anavisihi vyama vya wafanyakazi kushirikiana na Serikali na Waajiri kuhakikisha tija inaongezwa kwenye maeneo ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe.
Anasema wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kudai risiti kila wanaponunua bidhaa na kuhakikisha risiti wanazopewa zimeandikwa gharama halisi ili kuiwezesha Serikali kupata mapato zaidi na kupelekea wigo mpana zaidi wa kuboresha maslahi ya wafanyakazi.
*** Bodi ya kima cha chini cha mshahara
Anasema Serikali inashukuru kwa ushauri huo kutoka TUCTA lakini kwa upande wa bodi ya kima cha chini cha mshahara kwa utumishi wa umma bodi iliitwa mwaka 2016 na kumaliza muda wake 2023 na tayari bodi mpya imeundwa na kuendelea na majukumu yake.
Aidha anasema kwa upande wa bodi hiyo kwa upande wa sekta binafsi iliundwa Aprili 2022 na bado ipo hai na mchango wake ni mkubwa kufikia uamuzi wa kima cha chini ya mshahara sekta binafsi kilichotangazwa kupitia tangazo la serikali namba 687 Novemba 2022na kuanza kutumika Januari 2023.
Anasema sheria inataka bodi hiyo kutekeleza majukumu yake kwa kipindi cha miaka mitano ,kima cha chini cha mshahara ufanyiwa mapitio ndani ya kipindi hicho kwa kuzingatia.
***Kuhusu matakwa ya kisheria.
Anasema tayari tumeanza utafiti wa kina wa kima cha chini cha mshahara cha sekta binafsi ambao utajumuisha sekta ndogo ndogo kwa upana zaidi.
Anatoa wito wa wajumbe wa bodi kutoka TUCTA kwa kushiriki kikamilifu katika mchakato huo ili tufikie uamuzi shirikishi utakaosadifu mazingira ya wakati uliopo.
*** Akizungumzia hoja ya watumishi waliopo katika serikali za mitaa kulipwa mishahara kupitia mfuko mkuu wa serikali.
Anasemakuanzia mwezi julai 2024,watumishi 473 kutoka halmashauri 101 ambazo zilibainika kutokuwa na uwezo wa kulipa mishahara watumishi wake kwa kutumia mapato ya ndani.
”Sasa tutawalipa kupitia mfuko mkuu wa serikali,kiasi cha sh. Bilioni 3.8 zimetengwa kwaajili hiyo serikali itaendelea kufanya tathimini za mara kwa mara ili kubaini uwezo wa kifedha za halmashauri husika na kufanya uamuzi kadri inavyoonekana inafaa.
”Matarajio ya serikali halmashauri husika zitasimamia vizuri fedha zavyanzo vya mapato ya ndani na kuboreshaa huduma za kijamii,”anasema.
Anasema ni lazima halmashauri ziendelee kuongeza ubunifu ili kupata vyanzo vipya vya mapato na kusimamia kikamilifu matumizi yake.
Kwa upande wake,Waziri Mkuu Kassim Majaliwa anasema siku ya Wafanyakazi Duniani (MEI MOSI) ambayo huadhimishwa kila mwaka ni siku maalum kwa ajili ya wafanyakazi kutafakari na kutathmini namna walivyotekeleza malengo waliyojiwekea katika mwaka husika.
Anasema kuwa siku hiyo inatoa fursa kwa wafanyakazi wote duniani kuweka mipango kwa ajili ya mwaka unaofuata na ndiyo maana inafanyika kipindi ambacho nchini nyingi duniani zinakuwa katika maandalizi ya Bajeti.
“siku hii ni muhimu sana na inatukumbusha wajibu wetu wafanyakazi wa kujadiliana kwa pamoja changamoto zilizopo katika utendaji wetu wa kazi na kuzitafutia ufumbuzi kwa pamoja na hatimaye kuleta tija katika maeneo ya kazi”anasema.
Aidha,Majaliwa amewapongeza watumishi wote kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuwaletea watanzania maendeleo. “Sisi sote ni mashahidi wa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitatu kiuchumi, kisiasa, kidiplomasia na kijamii”anasema.
Katika maadhimisho hayo ambayo yamebeba kauli mbiu ya “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora na Kinga Dhidi ya Hali Ngumu ya Maisha”.
*** Hoja ya kikokotoo
Kuhusu madai ya kutaka kubadilishwa kikokotoo anasema Serikali imepokea hoja hiyo ya wafanyakazi.
“Hata hivyo, uamuzi wa kubadilisha Kikokotoo ni lazima utokane na tathmini ya kina ya kisayansi ya Watakwimu-bima. Ni matumaini ya Serikali kwamba, TUCTA itashiriki kikamilifu katika zoezi hilo na kuwasilisha maoni yatakayoimarisha zaidi mifuko.”
Hayo yamesemwa jana na Makamu wa Rais Dkt. Phili Mpango kwenye maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Mei Mosi, yaliyofanyika mkoani Arusha.
Dkt. Mpango amesema Serikali inategemea wataalam wake waishauri kuhusu suala la kikokotoo, kwani Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali yake wanawahakikishia wafanyakazi kwamba hakuna mtu ambaye angependa kuona watu walioitumikia nchi hii, wakiathirika kwa kukosa kiinua mgongo stahiki au pensheni zao.
“Kuhusu hoja ya kuboresha Kanuni ya ukokotoaji wa mafao, Serikali imepokea ushauri uliotolewa. Hata hivyo, ni muhimu kuzingatia kwamba uendeshaji na usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii ni suala la sayansi ya Watakwimu-bima.
Hivyo, tunawategemea wataalam wetu watushauri kuhusu suala hili la uhimilivu na uendelevu wa mifuko ya hifadhi ya jamii,” amesema Dkt. Mpango.
Amesisitiza kwamba Rais na Serikali yake wanawahakikishia wafanyakazi kwamba hakuna mtu ambaye angependa kuona watu walioitumikia nchi hii, wakiathirika kwa kukosa kiinua mgongo stahiki au pensheni zao.
“Kutokana na hali hiyo, ndiyo maana Serikali iliposhauriwa na wataalam husika, Serikali ya Awamu ya Sita ilichukua uamuzi mkubwa wa kulipa deni la mifuko ya Hifadhi ya Jamii kiasi cha sh.trilioni 2.147, hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imeimarisha mifuko hiyo.
Vilevile, tumeendelea kuimarisha utendaji kwenye mifuko hiyo na kupunguza ucheleweshaji wa malipo ya wastaafu.”
Kuhusu hoja ya kodi kwenye mapato yasiyo ya mshahara, naomba nieleze kwamba, kodi katika mapato ya wafanyakazi inatozwa kwa mujibu wa Sheria na utaratibu wa ukokotoaji, na ukusanyaji unazingatia kanuni za msingi za utozaji kodi ikiwemo kuweka usawa kwa watu wenye kipato kinachofanana.
Amesema utaratibu huo pia unawezesha udhibiti wa vitendo vya baadhi ya waajiri wasio waaminifu, kufanya udanganyifu kwa kupunguza kiasi cha msingi cha mishahara na kuainisha kwenye mahesabu yao kiasi kikubwa cha posho na marupurupu ili kukwepa wajibu wa kulipa kodi na michango ya pensheni za wafanyakazi wao, ambazo ni haki ya msingi kwa ajili ya kuwawezesha kupata kipato cha kujikimu baada ya kustaafu.
Kama sehemu ya kaulimbiu ya mwaka huu isemavyo, “Nyongeza ya Mishahara ni Msingi wa Mafao Bora….”. Kwa wale waajiri wanaoficha mishahara katika posho, watambue kuwa licha ya kuikosesha Serikali mapato, pia wanawakosesha wafanyakazi wao mafao bora baada ya kustaafu.
Kwa muktadha huo, Serikali itaendelea kusimamia Sheria ya Kodi ili kulinda haki za wafanyakazi.
Hata hivyo alitumia fursa hiyo kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi katika ulipaji wa kodi.
Kimsingi, wafanyakazi ni miongoni mwa walipaji wazuri wa kodi, na mnayo kila sababu ya kujipongeza kwa mchango wenu adhimu kwa Taifa. Kupitia sherehe hizi za Mei Mosi, naomba niendelee kuyasihi makundi mengine katika jamii, kutimiza wajibu wao wa kisheria wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.
***Majibu ya hoja za wafanyakazi
Aidha, Dkt. Mpango anasema Serikali imepokea ushauri wa TUCTA kuhusu kuridhia Mikataba yote muhimu inayogusa masuala ya wafanyakazi nchini na kukamilisha uridhiaji wa Mikataba 6 ya ILO iliyoanza kushughulikiwa.
Amesema Serikali inatambua umuhimu wa kuridhia Mikataba ya ILO inayogusa maslahi ya wafanyakazi.
Amesema Mpaka sasa, baada ya kupitia na kujiridhisha kuhusu yaliyomo ndani, Serikali imeridhia Mikataba minane kati ya 10 ya Msingi (Core Conventions).
Aidha, Serikali imeshaanza mchakato wa kuridhia Mikataba Sita ya Shirika la Kazi Duniani ambayo inajumuisha Mikataba miwili ya Msingi iliyobaki.
Serikali inapenda kusisitiza kwamba, kuridhiwa kwa mikataba ya kimataifa kutafanyika baada ya kujiridhisha na masuala ya msingi kama vile mila, tamaduni, desturi na maslahi mapana ya nchi yetu kwa ujumla. Kwa sasa tunaendelea na michakato ya ndani ya Serikali, na baada ya hatua hiyo, mapendekezo yatawasilishwa Bungeni kwa hatua zaidi.
Kuhusu mifumo ya utatuzi wa migogoro ya kikazi, Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 Marejeo ya Mwaka 2019, imeainisha utaratibu wa kufuata katika kushughulikia migogoro ya kikazi katika Utumishi wa Umma.
Aidha, Sheria inawataka watumishi wa Umma kutumia njia zote za kurekebisha (remedies) zilizoainishwa katika Sheria ya Utumishi wa Umma kwa kutumia Sheria nyingine ikiwemo Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini, Sura 366.
Aidha, Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha utendaji wa Tume ya Utumishi wa Umma ikiwemo kuongeza idadi ya siku za mikutano ya Tume kutoka siku 10 hadi 15 ili kushughulikia rufaa na malalamiko mengi zaidi, kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye Wizara na Taasisi za Umma kwa lengo la kuangalia uzingatiwaji wa Sheria katika usimamizi wa rasilimaliwatu na hivyo kupunguza rufaa na malalamiko ya watumishi, kuwajengea uwezo watumishi wa Tume na kuweka Mfumo wa Kielektroiniki wa kushughulikia rufaa na malalamiko.
Serikali imepokea pia ushauri kuhusu kuiongezea Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) watumishi na vitendea kazi ili kuiwezesha kufanya kazi kwa ufanisi.
Aidha, Dkt. Mpango amesema kwa kuzingatia umuhimu huo, Serikali itaendelea kuboresha utoaji wa huduma za CMA kwa kuipatia vitendea kazi ikiwemo magari na kuongeza idadi ya watumishi kulingana na uwezo wa kibajeti. Mfano, kwa mwaka wa fedha wa 2021/22 Serikali ilitoa kibali kwa Tume cha kuajiri watumishi 8, mwaka 2022/23 watumishi 16 na 2024/25 nafasi 24 zimetengwa kwa ajili ya ajira mpya.
Aidha, Serikali inaendelea kusimika Mifumo ya Kielektroniki ya usajili, utatuzi na usimamizi wa migogoro ya kazi. Mifumo hii itawezesha Wafanyakazi na Waajiri popote walipo kusajili migogoro ya kazi ikiwemo kutumia simu-janja pasipo kulazimika kuzifuata Ofisi za CMA. Utaratibu huu ni kama inavyofanyika katika Mahakama kote nchini.
***Vibali vya ajira
Kuhusu utaratibu wa kupata Vibali vya Ajira katika Utumishi wa Umma kwa makundi mbalimbali, alisema huo ni utaratibu wa kawaida uliowekwa kwa mujibu wa Sheria.
“Napenda nitumie fursa hii kusisitiza kwamba, watumishi wa taasisi za serikali ambazo zimeundwa kwa sheria mbalimbali wote ni watumishi wa umma. Hivyo, ni lazima kufuata sheria, kanuni na taratibu zinazoongoza ajira katika utumishi wa umma.
Utaratibu huu unalenga kuimarisha udhibiti katika eneo la ajira ambalo linapaswa kuzingatia sifa, uwezo wa kibajeti na vipaumbele vya Serikali katika kulitekeleza. Hata hivyo, Serikali itaendelea kuhakikisha kwamba eneo hili linaendelea kuwa na ufanisi ili kuharakisha utoaji wa Vibali vya Ajira kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Miongozo iliyopo.
Kuhusu Bima ya Afya, katika kuhakikisha kuwa wananchi wanapata huduma bora za matibabu nchini, alisema Serikali imefanya maboresho katika Orodha ya Taifa ya Dawa Muhimu (NEMLIT) pamoja na Miongozo mbalimbali ya Tiba (STG).
***Bima ya Afya
“Hivyo, kutokana na maboresho hayo, Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umefanya maboresho katika Kitita chake ili kwenda sambamba na Miongozo hiyo kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma bora kwa wanachama wake.
Hata hivyo, kutokana na changamoto zilizojitokeza baada ya kuanza utekelezaji wa Kitita hicho, Serikali iliunda Kamati huru ya Wataalam ili kupitia hoja za wadau na kupata suluhu ya changamoto zilizojitokeza,” amesema Dkt. Mpango.
Alisema kwa kuwa zoezi la mapitio ya Kitita bado linaendelea, Serikali itahakikisha wadau wote muhimu wanashirikishwa kikamilifu katika zoezi hilo na kutatua changamoto zilizojitokeza.
Alisema Uhai na uendelevu wa Mifuko ya Bima ya Afya Duniani kote unategemea uwasilishaji wa michango ya Wafanyakazi kwa wakati kutoka kwa Waajiri.
“Sheria ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya, Sura 395, inataka kila Mwajiri kuwasilisha mchango wa bima ya afya ndani ya siku 30 tangu tarehe ya malipo ya mshahara wa Mfanyakazi. Kwa kutambua jukumu hilo, Serikali imekuwa ikiwasilisha michango ya Watumishi wa Umma kwa wakati.
Ili kuepusha usumbufu kwa Wafanyakazi, Waajiri wote wanaojiunga kwa hiari katika Mfuko wanakumbushwa kuwasilisha kwa wakati michango ya Wafanyakazi wao,” alisema.
***Likizo ya uzazi
Kuhusu likizo ya uzazi kwa wafanyakazi wanawake wanaojifungua mtoto/watoto njiti. Alisema iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto kabla ya muda wake, mtoto au watoto husika huwekwa katika chumba na mashine maalum (incubator) chini ya uangalizi wa madaktari na wahudumu wengine wa afya hadi pale wataalam hao wanapojiridhisha kuwa afya ya mtoto/watoto hao imeimarika.
Hivyo, iwapo mfanyakazi atajifungua mtoto au watoto njiti, kipindi cha uangalizi maalumu hakitahesabiwa kama likizo ya uzazi. Likizo ya uzazi itaanza pale mtoto atakapomaliza kipindi cha uangalizi maalum kadri madaktari watakavyothibitisha.
Vilevile, mfanyakazi husika ataruhusiwa kutoka kazini saa 7:30 kila siku kwa muda wa miezi sita baada ya kumalizika kwa likizo ya uzazi ili kumpa fursa ya kwenda kunyonyesha.
***Maboresho ya maslahi ya wafanyakazi
Dkt. Mpango anasema Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya watumishi kwa namna nyingine mbalimbali, ikiwemo kwa kulipa nyongeza ya mwaka ya mshahara (annual salary increment), ambapo Mwaka 2023/24 kiasi cha sh. 153,926,496,703.68 kililipwa; na kwa mwaka 2024/25, Serikali imetenga sh. 150,873,245,100.00 kwa ajili hiyo.
“Kama mlivyosema kwenye risala yenu, kabla ya mwaka jana, nyongeza ya mshahara ilikuwa imesimama kwa muda mrefu, lakini sasa tunajitahidi kuitekeleza.
Kwa upande mwingine, Serikali imeendelea kuwapandisha vyeo watumishi mbalimbali, ambapo Mwaka 2023/24 jumla ya watumishi 81,515 walipandishwa vyeo na mwaka 2024/25 Serikali imetenga kiasi cha 252,703,717,483.72 kwa ajili ya kuwapandisha vyeo watumishi 219,924,” amesema Dkt. Mpango.
Amewapongeza wafanyakazi wote nchini kwa kuadhimisha sikukuu hii, na nawashukuru tena kwa mchango wenu adhimu katika ujenzi wa Taifa letu. Kama yalivyo makundi mengine kwenye jamii, kundi la wafanyakazi lina mchango mkubwa sana katika ujenzi wa nchi yetu. Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya kazi ikiwemo kuboresha maslahi ya wafanyakazi kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.
“Wito wangu kwenu wafanyakazi, ni kuendelea kutekeleza majukumu yenu kwa bidii, maarifa, uadilifu na kwa moyo wote, huku mkitanguliza maslahi ya Taifa mbele.
Nawaomba pia muendelee kuongeza tija katika utendaji kazi. Navisihi vyama vya wafanyakazi tushirikiane na Serikali na Waajiri kuhakikisha tunaongeza tija kwenye maeneo yetu ya kazi kwa manufaa ya Taifa na wafanyakazi wenyewe, sambamba na kupaza sauti kuhusu madai ya wafanyakazi,” amesema Rais Samia.
More Stories
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini
Rais Dk. Samia alivyowezesha Tanzania kuwa kinara usambazaji umeme Afrika