Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
WIZARA ya Mifugo na Uvuvi imesema Serikali imenunua jumla ya hereni za kidijitali 36,323,300 kwa ajili ya utambuzi wa ng’ombe 19,099,100, Mbuzi na Kondoo 17,224,200 watakaochanjwa.
Imesema lengo kuu la utambuzi wa mifugo ni hiyo ni kukidhi matakwa ya soko la kikanda na kimataifa linalohitaji kila mnyama na mazao yake kuwa na alama ya utambuzi.
Hayo yamesemwa jijini hapa leo Mei 6,2025 na Waziri wa Wizara hiyo Dkt.Ashatu Kijaji wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita.
Ambapo amesema kuwa alama hizo za utambuzi zitawezesha wafugaji kupata mikopo na bima,kudhibiti wizi wa mifugo,kurahisisha ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya wanyama na
kuwezesha Serikali na wadau kuweka mipango ya kuhudumia mifugo kwa kuwa
idadi yao inajulikana.

Aidha Dkt.Kijaji amesema kuwa katika miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita, Wizara imeendelea kuimarisha biashara ya nyama kwenda nje ya nchi, ambapo mauzo yameongezeka kutoka tani 1,774 zenye thamani ya shilingi 9,867,000,000 kwa mwaka 2020/2021 na kufikia tani 13,745.38, zenye thamani ya shilingi 147,133,388,688 kwa mwaka 2024/2025.
Hivyo, kufanya jumla ya tani 40,635 zilizouzwa nje ya nchi zenye thamani ya shilingi 414,378,447,756.
“Ongezeko hili linatokana na
jitihada zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuongeza ushirikiano na fursa za kibiashara nje ya nchi na hivyo, kuongezeka kwa masoko ya
nyama hadi kufikia nchi 12 ambazo ni Bahrain, Comoro, Hong Kong, Jordan, Kenya, Kuwait, Oman, Qatar, Rwanda, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Vietnam.
Akizungumzia Sekta ya Uvuvi Dkt.Kijaji amesema ni miongoni mwa Sekta za uzalishaji ambayo inatoa ajira za moja kwa moja kwa wavuvi 201,661, wakuzaji viumbe maji 49,084 na takriban watanzania milioni 6 wanajishughulisha na kazi mbalimbali zinazohusiana na uvuvi katika mnyororo wa thamani.
Aidha,amesema ukuaji wa Sekta ya Uvuvi ni asilimia 1.4 ambapo unachangia Pato la Taifa kwa asilimia 1.7 katika mwaka 2023,huku hali ya uzalishaji wa mazao ya uvuvi ukiongezeka kutoka tani 477,018.84, zenye thamani ya shilingi
2,775,798,531.30 katika mwaka 2021, hadi kufikia tani 522,788.33, zenye thamani
ya shilingi 4,352,735,640.54, katika mwaka 2024.

“Aidha, katika kipindi cha kuanzia mwaka 2021 hadi 2024, jumla ya tani 1,951,296.33 za mazao ya uvuvi, zenye thamani ya shilingi 13,647,504,498.08, zilizalishwa kutoka katika maji ya asili,”amesema Dkt.Kijaji.
Kwa upande wa Mauzo ya Mazao ya Uvuvi na Samaki Hai wa Mapambo Nje ya Nchi,Dkt.Kijaji amesema Serikali imeendelea kuimarisha biashara ya mazao ya uvuvi katika soko la ndani na
nje ya nchi ambapo, mauzo ya mazao ya uvuvi na samaki hai wa mapambo
yameongezeka kutoka tani 42,302.03 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa
mapambo 181,268 zenye thamani ya dola za Marekani 457,817,845,082 kwa
mwaka 2021 hadi kufikia tani 59,746.41 za mazao ya uvuvi na samaki hai wa
mapambo 148,041 zenye thamani ya shilingi 752,969,498,996 mwaka 2024.Hivyo,
kufanya mauzo ya mazao ya uvuvi kuongezeka hadi kufikia tani 181,655.7 na samaki hai wa mapambo 729,413 yenye thamani ya shilingi 2,282,092,677,530.
“Ongezeko hili limetokana na kuboreshwa kwa mazingira ya biashara ikiwa ni pamoja na kupungua kwa baadhi ya tozo na kuimarika kwa masoko ya mazao nje ya nchi. Aidha, ongezeko la thamani ya samaki hai wa mapambo limetokana na kuimarika kwa soko la samaki hai nchi za nje zikiwemo nchi za Poland, Denmark, Ujerumani,Marekani na Uswisi,”amesema.
Pamoja na hayo Dkt.Kijaji amezungumzia Program ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT)ambapo amesema kupitia maono ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wizara imetekeleza Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) inayolenga kuwajengea uwezo vijana na wanawake kujiajiri na kuajiri wengine katika shughuli za ufugaji, uvuvi na ukuzaji viumbe maji nchini.
Amesema kupitia Programu hiyo,
katika kipindi cha miaka miwili, Wizara imewezesha vijana 235 katika vituo nane kupata mafunzo kwa vitendo ya unenepeshaji wa mifugo.

“Baada ya mafunzo hayo,
vikundi 20 vyenye vijana 106 vimepatiwa ekari 1,761 katika Ranchi ya Kagoma na
kupewa mkopo usio na riba wa jumla ya shilingi 934,231,000 kupitia Benki ya
Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa ajili ya kuendesha shughuli za
unenepeshaji ng’ombe.
“Pia Serikali imeboresha miundombinu katika Ranchi hiyo kwa kuweka umeme wa jua kwenye makazi ya vijana hao na kujenga mazizi kwa ajili ya shughuli za unenepeshaji wa mifugo,”amesema.
Ameeleza kuwa hadi kufika Machi, 2025 jumla ya ng’ombe 583 wamenunuliwa. Kati ya ng’ombe hao 416 ambao wana thamani ya shilingi 299,520,000 wamenenepeshwa na kuuzwa kwa jumla ya shilingi
370,240,000 ambapo kwa wastani kila ng’ombe mmoja amegharimu shilingi 720,000 na kuuzwa kwa wastani wa bei ya shilingi 890,000. Hivyo, faida ikiwa ni wastani wa shilingi 170,000 kwa kila ng’ombe.
“Kwa upande wa Sekta ya Uvuvi, jumla ya
wanufaika 500 (wanawake na vijana) waliwezeshwa kwa kupatiwa mafunzo kwa
vitendo kupitia vituo 15 vilivyopo katika Ukanza wa Ziwa Victoria (10) na Ukanda wa Pwani (4) na Zanzibar (1) katika mwaka 2023/2024,”amesema Dkt.Kijaji.
More Stories
UAE yamtunuku Rais Samia Medali ya juu kabisa
Rais Samia amteua Mkurugenzi Mtendaji TANESCO
RMO,DMO waagizwa kumsimamia Mkurugenzi ununuzi vifaa ,vifaa tiba