Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi Zanzibar Dkt Mngereza Mzee Miraji amesema wizara yake imeshakamilisha ramani ya mji wa Serikali kiutendaji kwa awamu ya kwanza ambapo maeneo sita yameshaainishwa kwaajili ya kujenga mji huo.
Akizungumza mara baada ya kumaliza kikao baina ya wizara yake na Taasisi ya Rais ufuatiliaji na Usimamizi wa utendaji Serikalini (PDB), kilichofanyika mwisho wa wiki katika hoteli ya Golden Tulip Kiembesamaki, Unguja, alisema ramani ya Mji wa Serikali imekamilika na muda sio mrefu Serikali itaamua wapi ujengwe mji huo.
Dkt Mngereza aliyataja baadhi ya maeneo ambayo wizara yake imependekeza kujenga mji wa Serikali ikiwemo, Fumba, Kisakasaka, Dunga na Tunguu ambapo maeneo hayo kwa unguja yameonekana yanafaa kujengwa Mji wa Serikali kutokana vigezo vinavyohitajika katika Mji wa Serikali.
“Ni kweli mwezi mmoja uliyopita tuliwaita watendaji wa wizara zote za Serikali tuliwaita wizarani watupe maoni yao ya mwisho ili tukafanye marekebisho katika dizaini (design) ya Mji wa Serikali iliyokuwepo, lakini leo maeneo yaliyoanishwa nitayataja matatu, Fumba, Kisakasaka, na Dunga. Naongeza na moja Tunguu“ Alisema Dkt Mngereza.
Alisema chanzo cha fedha za ujenzi wa Mji wa Serikali bado hakijafahamika lakini Serikali ikishaamua kujenga sehemu Fulani bila shaka kutakuwa na chanzo cha fedha na bajeti yake ambapo Ofisi ya Rais Fedha na Mipango itaeleza chanzo hicho na bajeti yake.
Pia alisema kupitia kikao hicho kunamajukumu wamekubaliana baina Wizara ya Ardhi na Taasisi ya PDB na majukumu hayo yametakiwa kukamilika kwa kipindi cha muda wa wiki moja.
Aidha Dkt Mngereza waliishukuru Taasisi ya Rais Ufuatiliaji wa Usimamizi Utendaji Serikalini (PDB) kwa kuanda kikao cha pamoja na Wizara yake kwa lengo la kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Ardhi Zanzibar.
Naye Mkurungenzi Mkuu Shirika la Nyumba (ZHC) Mwanaisha Ali Said alisema kikao hicho ni muhimu sana kwasababu ZHC bado inachangamoto ya kiutendaji ikiwemo fedha, jinsi ya kupata fedha na jinsi ya kuandika maandiko ya kupata fedha na vipaumbele mbali mbali.
“PDB imekua taasisi muhimu kwa ZHC kwa kutumia utaalamu wao katika sekta ya nyumba na sekta ya uendeshaji miradi wametusaidia kutuongoza kwani vipaumbele vya Mhe Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi ni vingi hata vipaumbele vya Shirika la Nyumba Zanzibar pia ni vingi” Alisema Mwanaisha.
Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha Mawasilino na Habari Kutoka Taasisi ya Rais Ufuatiliaji na Usimamizi wa Utendaji Serikalini (PDB) Dr. Mohamed Mansour Nassor alisema Taasisi yake imeweza kujua Shirika la Nyumba Zanzibar namna gani linavyofanya kazi, mikakati yake , mafanikio pamoja na changamoto.
Alisema kikao hicho ni muendelezo wa vikao vya PDB na Wizara mbali mbali za Serikali katika kufuatilia utekelezaji wa miradi ili waweze kujua ni changamoto zipi zinazoikabli miradi hiyo na kuipatia ufumbuzi ili kufikia malengo ambayo Mhe. Rais wa Zanzibar Dkt Hussein Ali Mwinyi anataka katika uongozi wake.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa