February 24, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali ya Kijiji Ilungu yawakatia bima za afya wananchi 1500

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

WANANCHI zaidi 1500 wa Kijiji  cha Mashese kata ya Ilungu katika Halmashauri ya Wilaya ya  Mbeya wamelipiwa bima za afya na serikali ya Kijiji hicho  ili kuwa na uhakika wa matibabu  na kujenga jamii imara.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kijiji cha  Ilungu ,Osia  Mwakalila  wakati Akizungumza na  Timesmajira katika Zahanati ya Kijiji hicho ambapo amesema kusudi la Serikali yake ya kijiji ni kuona inatoa bima za afya kwa watu  2000,wa kijiji hicho hata waishio nje ya kijiji kwa shughuli mbalimbali ikiwemo wanafunzi.

“Tulipokaa na uongozi wa Kijiji na kuangalia kutokana na vyanzo vyetu vya mapato ya kijiji tukaamua kuwakatia bima za afya wananchi na lengo letu ni wananchi wote wapate bima kwasababu wengi hawana kipato na tukatembelea wananchi huko tukaona wanaumwa halafu hawana fedha  za matibabu “amesema Mwenyekiti huyo.

Aidha Mwakalila ameomba wadau kusaidia  vifaa vya maabara  na kutembelea  Zahanati ya Ilungu ikiwemo wanaotaka Kijiji cha Mashese ili zoezi hilo liwe endelevu.

Akizungumzia bima hizo zilizotolewa kwa ajili ya wananchi  mganga mfawidhi wa Zahanati ya Ilungu ,Jafary Edward amesema bima za CHF zilizokatwa  kwa ajili ya wananchi hao ni kwa familia au kikundi cha watu sita kwa shilingi 30,000 na kusema  ni hatua muhimu katika kuhakikisha jamii inakuwa na watu wenye afya imara huku akiwatoa hofu wananchi wanaodhani wenye bima hawathaminiwi pindi wanapokwenda kupatiwa matibabu hospitalini.

“Hivyo tunaomba wananchi waone kuwa bima hii ni Muhimu kwao na waende hospitali kupatiwa matibabu wakiwa kifua mbele kabisa “amesema mganga mfawidhi huyo

Naye Mratibu wa bima ya CHF wilaya ya Mbeya Francisco Nguvila, amesema kilichofanywa na Serikali ya kijiji cha Mashese kuwakatia bima wananchi wake ni kitendo cha kuigwa na maeneo mengine katika kuhakikisha jamii inakuwa na afya imara na kuchochea maendeleo ya Taifa.

Aidha wananchi waliofikiwa na huduma hiyo wameishukuru Serikali yao kwa mpango huo ambao umetekelezwa kupitia raslimali za kijiji na  kuona zinarudi kwao (wananchi) kwa njia nyinginezo ikiwemo kujali afya za wananchi wake.