Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema mwelekeo wa Serikali kwa sasa ni kusisitiza utoaji elimu yenye ujuzi ili kuhakikisha wahitimu hasa wa Maendeleo ya Jamii wanapata stadi za kazi.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo wakati akiwatunuku wahitimu 1604 wa fani ya Maendeleo ya Jamii katika ngazi mbalimbali, wakati wa Mahafali ya 12 ya Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Desemba 16, 2022.
Amesisitiza kuwa, Serikali na hata Sekta binafsi hazina uwezo wa kuajiri wahitimu wote wa elimu ya juu, hivyo dhana ya uanagenzi, ubunifu na ushirikishwaji jamii katika mitaala ni suluhisho la ukosefu wa ajira kwa kuwa wahitimu wanapata ujuzi wanaoweza kutumia kujiajiri na hata kuajiri wengine.
“Nitoe Rai kwa Wadau wa mahala pa kazi ikiwemo Mamlaka za Serikali, Asasi za kiraia, Mashirika na Makampuni kutenga nafasi za uanagenzi kwa wanafunzi wa Taasisi ili kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa wahitimu wetu” alisema Gwajima.
Ameongeza kuwa, Taaluma ya Maendeleo ya Jamii ni muhimu kwani inawezesha sekta nyingine kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi kwa sababu inashughulika na watu moja kwa moja.
Aidha amewataka wahitimu hao kuwa na fikra chanya na ubunifu kwa sababu wamehitimu kipindi ambacho Serikali imefanya kazi kubwa ya kuvutia wawekezaji wa ndani na nje, kujenga uchumi imara na kuongeza mzunguko wa fedha.
“Ninyi ni mawakala wa mabadiliko, kiuhalisia huwezi badili fikra mpya na chanya kwa Jamii zetu kwa ajili ya kuleta mwamko na hamasa ya maendeleo” aliongeza Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima ameihakikishia Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru kuwa Wizara itaendelea kutatua changamoto zinazikabili Taasisi hiyo ambayo inaelekea kutimiza miaka 60 tangu kuanzisha kwake.
Wakati huo huo, Taasisi hiyo ya Maendeleo ya Jamii Tengeru imemtunuku Waziri Dkt. Gwajima tuzo ya Kinara wa kupambana na ukatili wa kijinsia nchini.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya uendeshaji wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru Dkt. Rosemarie Mwaipopo amemshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuipatia Fedha Taasisi hiyo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya Maendeleo ambapo, mwaka 2022/23 Taasisi imepokea Shillingi bilioni 1.6 kwa ajili ya samani katika majengo ya hosteli ya wasichana na kumbi pacha za mihadhara.
Kwa upande wake Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Dkt. Bakari George amesema Taasisi kwa mwaka huu imeadhimisha wiki ya Maendeleo ya Jamii kwa shughuli mbalimbali kwa lengo la kujikumbusha kwa vitendo shughuli za msingi za fani ya Maendeleo ya Jamii.
Akitaja shughuli hizo Dkt. Bakari amesema ni Kongamano la kitaaluma kubadilishana mawazo kuhusu muelekeo na Maendeleo ya Jamii, upandaji miti, matembezi ya kuhamasisha lishe Bora, mashindano ya uandishi wa maandiko ya miradi, elimu juu ya mapambano ya Vitendo vya ukatili na kuchangia damu salama.
More Stories
‘Ni Wasira ‘Makamu Mwenyekiti CCM Bara
15 mbaroni tuhuma wizi wa shehena ya unga wa sembe
Wacheza rafu Uchaguzi Mkuu ujao waonywa