Na Jackline Martin, TimesMajira Online
Serikali imejipanga kuweka mazingira wezeshi kwa maendeleo ya Uwekezaji, Viwanda na Bishara kwa kufanyia kazi changamoto za wafanyabiashara kupitia Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara hasa katika kuimarisha upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika na kwa bei nafuu, kujenga barabara, reli, bandari, viwanja vya ndege na miundombinu mingine ya uchukuzi.
Hayo ameyasema Waziri wa Biashara na maendeleo ya viwanda serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Omar Said Shaban wakati wa ufunguzi wa maonesho ya saba ya bidhaa za viwanda vya Tanzania yaliyofanyika jana Novemba 4, 2022 katika uwanja wa maonesho wa Mwl. J.K Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri Omar amewataka wananchi kutumia malighafi zilizoanzishwa nchini ili viwanda viweze kuongeza ajira kwa watanzania na hata kuchangia katika uchumi wa nchi.
“Nawaasa Watanzania waliopo nchini na wanaoishi nje kuwekeza katika Viwanda ambavyo vitatumia malighafi zinazozalishwa nchini na kuziongezea thamani, ili kuendeleza viwanda, kuongeza ajira kwa watanzania na hata kuchangia katika uchumi wa nchi yetu”
Aidha Waziri Omar aliwataka wasomi na watafiti kufanya tafiti zitakazo saidia Viwanda nchini kuimarika kwa kutumia mazingira halisi ya Tanzania.
Pia Waziri huyo amewahakikishia wafanyabishara nchini kuwa wataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuhakikisha wanatenga maeneo ya kimkakati katika uwekezaji na viwanda.
” Wizara itaendelea kushirikiana na Wakuu wa Mikoa kupitia Idara za Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuhakikisha wanatenga maeneo ya Kimkakati katika Uwekezaji na Viwanda kwa ajili ya Viwanda vidogo na vya Kati (SMEs) katika kila Mkoa na Wilaya, kuweka miundombinu wezeshi ya Viwanda ikiwa ni pamoja na kutatua changamoto ya ardhi kwa ajili ya kuendeleza viwanda nchini.”
Vilevile Waziri Omar amesema Tanzania ipo katika nafasi nzuri zaidi kiushindani katika masoko mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kutokana na uwepo wa fursa za soko la pamoja ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Soko huru la Afrika (AfCFTA), Ushirikiano wa nchi za Kusini mwa Afrika, Soko la Ulaya, Marekani, China, India na nchi za Asia kati na mashariki ya mbali.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzanzia (TANTRADE) Latifa Mohamed amesema katika kuhakikisha taarifa za biashara zinawafikia Wadau kwa wakati, TanTrade imesanifu Mfumo wa Taarifa za biashara (TanTrade Mobile App) utakowezesha upatikanaji wa taarifa muhimu zikiwemo bei za bidhaa, mwenendo wa masoko, wauzaji wa bidhaa na watoa huduma kutoka sekta mbalimbali za kibiashara kama vile wasafirishaji na mawakala.
“Uzinduzi wa Mfumo huu unatarajia kufanyika tarehe 5 Desemba, 2022 katika Ukumbi huu wa DOME. Hivyo, nitumie fursa hii kuwakaribisha wadau wote wa viwanda na biashara pamoja na Watanzania kwa ujumla kushiriki katika program hizi.”
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi – TANTRADE, Dkt. Issa Salim, amesema TANTRADE imejipanga kufanya tafiti za kimasoko katika Jamuhuri ya Demokrasia ya Congo, Zambia na Sudan ya Kusini kwa lengo la kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinapenya katika masoko kadhaa ya kiwango Afrika Mashariki , SADEC na soko huru la Afrika.
Naye Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Ally Gugu amesema kuhusu viwanda vidogo na vya kati, mpango wa serikali unabainisha kuwa Wizara zitaweka nguvu katika kuhamasisha wadau ili kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati ambavyo vinatumia teknolojia ya kisasa itakayopelekea kuleta tija na ufanisi katika kuzalisha bidhaa ambazo zinaagizwa kwa wingi.
“Wafanyabishara wengi wamekuwa wakisema ifike ukomo wa kuagiza bidhaa ambazo pengine tunaweza kuzizalisha ndani kama vijiti vya kutolea uchafu kwenye meno, pamba za kutolea uchafu kwenye masikio, sukari, mafuta ya kula n.k ambapo bado kuna fursa ya kuweza kuhamasishana ili kuhakikisha tunazizalisha hapa nchni “.
Maonesho ya mwaka huu yalianza na bonanza maalum la maziwa lililofanyika tarehe 3 Desemba, 2022 likiongozwa na Mheshimiwa Abdallah Ulega (Mb.), Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi kwa lengo la kuhamasisha unywaji maziwa yanayozalishwa nchini na kutarajiwa kumalizika tarehe 9 Desemba mwaka huu. Maonesho hayo yameenda sambamba na kauli mbiu inayosema ‘Nunua bidhaa za Tanzania Jenga Tanzania’.
More Stories
Kiswaga:Magu imepokea bilioni 143, utekelezaji miradi
Zaidi ya milioni 600 kupeleka umeme Kisiwa cha Ijinga
Kamishna Hifadhi ya Ngorongoro atakiwa kupanua wigo wa Utalii nchini