Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma
WAZIRI wa Habari,Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema,umefika wakati wa Serikali kutenga fedha wa ajili ya vyombo vya habari ili kuvifanya viwe endelevu kwa maslahi mapana ya Taifa.
Akihitimisha hoja ya mapato na matumizi ya Fedha kwa mwaka 2024/2025 Waziri Nape amesema,bila vyombo vya habari nchi haitakwenda.
“Imefika wakati wa Serikali kutenga bajeti maalum kwa ajili ya vyombo vya habari maana bila vyombo vya habari nchi haitekwenda ,kwa hiyo ni muhimu tutenge fedha.”amesema Nape
Kuhusu madeni ya vyombo vya habari Nape amewaahidi wabunge kwamba atahakikisha hizo fedha zinalipwa ili vyombo vya habari visife.
Aidha amesema waandishi wa habari wapo salama chini ya mikono ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwani wakati wote amekuwa akihimiza uhuru wao.
Awali wakati akiwasilisha bajeti yake aliwashukuru wadau wote wa habari nchini ukiwemo Umoja wa Klabu za waandishi wa habari nchini kwa kuelimisha umma .
Baadhi ya Wabunge waliochangia bajeti hiyo wameiomba Serikali kulipa madeni na kufanya kazi na vyombo binafsi vya habari ili kuvifanya viwe endelevu.
Mbunge wa Viti Maalum Ester Bulaya (Chadema) amesema vyombo vya habari vinategemea matangazo kutoka serikalini,wanapolipwa ndiyo na wao wanapoweza kulipa mishahara na kujiendesha.
“Sasa leo wana madeni sugu zaidi ya shilingi bil. 18 na hapo kuna vyombo vingine madeni yao hayajawekwa,vyombo binafsi vinadai bil 7,TSN peke yake wanadai bilioni 11,hawa watu watafanyaje kazi,tunaomba hawa watu walipwe.”amesema Bulaya
Aidha ameishauri bajeti kuu ya serikali itenge angalau asilimia 0.3 sawa na shilingi bilioni 133 kusaidia uchumi wa vyombo vya habari ili viweze kuajiri na kutoa mikataba lakini pia kulipa wafanyakazi wao.
Kwa upande wake Mbunge wa Buchosa Erick Shigongo (CCM) amesema “hali ya vyombo vya habari ni mbaya ,vyombo vinashindwa kulipa wafanyaazi wake, au labda Serkali inataka vyombo vya habari vife,lakini naomba itambulike wazi hakuna maendeleo bila vyombo vya habari.”
Ametumia nafasi hiyo kuiomba Wizara ya habari itenge angalau asilimia moja ya bajeti yake iende kwenye idara za habari kwa ajili ya kuviwezesha vyombo hivyo kufanya kazi adhimu ya kuuhabarisha umma wa watanzania na dunia kwa ujumla.
Lakini pia Shigongo ameiomba Serikali iruhusu ifanye kazi na vyombo vya habari binafsi huku akishauri vyombo vya habari vya serikali vijitoe kwenye matangazo huku akisema haiwezeni vyombo vya serikali ambavyo vinapata ruzuku ya serikali kupambania matangazo na vyombo binafsi.
“Tukifanya hivi nina uhakika vyombo vya habari vitakuwa na nguvu na vyombo hivi vikiendelea kuwepo vitasaidia kupeleka taifa letu mbele .
Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya Bunge Mkurugenzi wa UTPC Kenneth Simbaya amesema kutokana na bajeti hiyo inaonesha mwaka ujao wa fedha inaonesha matumaini makubwa ya kupanuka kwa wigo utakaojenga mazingira mazuri ya waandishi wa habari kufanya kazi ya kuelimisha na kuhabarisha umma.
“Waandishi wa habari wanahitaji usalama wa kiuchumi na hata kimwili ili waweze kufanya azi yao vizuri,kwa hiyo bajeti ya 2024/2025 inaonesha matumaini makubwa ya kesho ya waandishi.”amesema Simbaya
Kuhusu madeni Mkurugenzi huyo amesema Seriali ikilipa madeni inayodaiwa na vyombo vya habari navyo vitakuwa na uwezo wa kulipa waandishi wake lakini pia vitaweza kujiendesha.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba