Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, Babati
Serikali katika Bajeti ya Mwaka 2023/2024 imedhamiria kusogeza Huduma za Kipolisi karibu na wananchi kwa kujenga Vituo vya Polisi Kata nchi nzima sambamba na kupeleka Vyombo vya Usafiri yakiwemo magari na pikipiki ambayo yatasaidia mapambano mbalimbali dhidi ya uhalifu.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Masauni wakati wa Mkutano wa Hadhara na wananchi wa Kata ya Galapo iliyopo wilayani Babati Mkoani Manyara baada ya kuzindua Kituo cha Polisi Kata kilichojengwa na wananchi kwa kushirikiana na serikali huku pia serikali ikiweka mkakati wa kupeleka askari wenye vyeo vya nyota mojaa katika kila kituo nchi nzima.
“Serikali ya Awamu ya Sita ya Mama Samia (Dkt.Samia Suluhu Hassan), imedhamiria kusogeza huduma za Jeshi la Polisi karibu na wananchi, huu ni mkakati kabambe na pia ni mkakati mahususi na katika kutimiza lengo hilo kuna hatua kadhaa tumeanza kuzipitia, hatua ya kwanza ni kuhakikisha tunapeleka Polisi katika Kata zote za nchi hii kwa kuanzia mwaka juzi tulipeleka mafunzoni Askari Polisi na kuwapandisha vyeo kwa ngazi ya nyota moja na hatua ya pili ni kutafuta Vyombo vya Usafiri kwa ajili ya askari wetu, nataka kuwahakikishia katika Bajeti (2023/2024) tumetenga bajeti ya Shilingi Bilioni Kumi na Tano na tayari zishatolewa na zimelenga kununua magari katika wilaya zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili Wakuu wa Vituo katika wilaya zote waondokane na adha ya kutumia magari mabovu” alisema Waziri Masauni.
Akizungumza wakati wa Uzinduzi huo, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Lucas Mwakatundu alitaja gharama ya jumla ya ujenzi wa kituo hicho huku eneo la ujenzi wa kituo hicho cha polisi kata limetolewa na serikali ya Kijiji huku akitaja ongezeko la uhalifu,kuongezeka kwa wawekezaji wa vituo vya mafuta,taasisi za fedha yakiwemo mabenki,kuongezeka kwa shughuli za uzalishaji ikiwemo kilimo na biashara mbalimbali na kuimarisha usalama katika eneo hilo kuwa iliongeza chachu ya ujengwaji wa kituo hicho.
“Ujenzi wa Kituo cha Polisi Galapo ulianza mwaka 2007 kwa mawazo ya wananchi wao wenyewe,kituo hiki kina ukubwa wa eneo kwa mita za mraba 150 yaani urefu wa mita 15 na upana wa mita 10 huku jengo hili likijengwa kwa nguvu ya wananchi,serikali pamoja na wadau mbalimbali huku gharama za ujenzi wa kituo zikifikia Shilingi Milioni 52,982,262.50” alisema ACP Mwakatundu.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi Mbunge wa Babati Vijijini, Daniel Sillo aliishukuru serikali kwa kuunga juhudi nguvu za wananchi za kuimarisha amani na usalama katika maeneo hayo akiweka wazi kituo hicho kitahudumia kata nne huku akiomba kituo hicho kifanye kazi kwa masaa Ishirini na Nne ili wananchi waweze kupata huduma za kipolisi muda wowote watakapohitaji.
More Stories
TASHICO,yatoa ufafanuzi Mv.Serengeti kutitia upande mmoja
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua