December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kushirikisha sekta binafsi kutekeleza miradi

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WIZARA ya Ujenzi imesema ili kuipunguzia Serikali gharama kubwa za utekelezaji wa miradi hiyo sambamba na kupunguza muda mrefu unaotumika katika kutekeleza miradi, kuna haja ya kushirikisha sekta binafsi kwa utaratibu wa ubia (PPP).

Akiwasilisha Bungeni mpango wa Makadirio ya mapato na matumizi ya mwaka wa fedha 2024/25,Waziri wa Wizara hiyo Innocent Bashungwa amesema kuwa kwa kutambua mchango wa Sekta Binafsi, Serikali imefanya maboresho makubwa kwenye
Sheria ya PPP kwa lengo la kuvutia uwekezaji wenye tija na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu.

Ametaja Maboresho muhimu
yaliyofanyika katika sheria hiyo ni pamoja na Kuruhusu taratibu mbadala za utatuzi wa migogoro, ikiwa ni pamoja na upatanishi na usuluhishi, pamoja na mashauri ya uwekezaji kusikilizwa kwa kutumia mahakama zitakazokubalika baina ya pande zote mbili badala ya mashauri hayo kusikilizwa katika mahakama za ndani.

Aidha Kuweka takwa la miradi yote ya PPP kutekelezwa kupitia kampuni maalum ya
kusimamia mradi husika, (Special Purpose
Vehicle) ambapo ushiriki wa sekta ya umma katika kampuni hiyo hautakiwi kuzidi
asilimia 25.

“Kutoa nguvu kwa Waziri mwenye dhamana
ya PPP kuruhusu miradi (solicited projects) yenye sifa maalum kutopitishwa kwenye mchakato wa ushindani chini ya masharti maalum.

“Lengo ni kuharakisha utekelezaji
wa miradi ya hiyo kwa kutoa nafasi ya
kujadiliana moja kwa moja na sekta binafsi bila kupitia taratibu zilizozoeleka za ushindani,”amesema Bashungwa.

Amesema kuwa maboresho hayo yatasaidia kuhakikisha kuwa mazingira ya uwekezaji yanakuwa rafiki zaidi, yenye uwazi na yenye ufanisi mkubwa kwa wawekezaji wa ndani na wa kimataifa.

Ameeleza kuwa kuhusu miradi ya
barabara,iliyotekelezwa kwa utaratibu wa PPP kuwa Serikali inatekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya Kibaha – Chalinze – Morogoro –Dodoma Expressway yenye urefu wa kilometa 531.8.

Amefafanua barabara hizo zimepitia utaratibu wa PPP kwa Sehemu ya Kibaha – Chalinze (km 78.9), kazi inayoendelea ni uchambuzi wa Proposals(Evaluation of Technical & Financial Proposals) wa Makandarasi/ Wawekezaji waliofaulu Vigezo vya kupatiwa Nyaraka za Zabuni (Request for Proposals) ya kutekeleza mradi huu.

“Kwa sehemu ya Chalinze – Morogoro yenye urefu wa kilometa 84.9, Mshauri Elekezi
yupo katika hatua za mwisho kukamilisha
kazi ya Upembuzi Yakinifu.

“Kwa sehemu ya Morogoro – Dodoma (km
260) usanifu wa kina wa kawaida (Conventional Design) uko katika hatua za mwisho kukamilika,Usanifu utatumika
kujenga maono (Concept) ya Mradi wa PPP,”amesema Bashungwa.

Aidha amesema Serikali inaandaa andiko la ujenzi wa Barabara ya TANZAM kuanzia Morogoro – Iringa –Mbeya hadi Tunduma kwa kuanzia na sehemu ya Igawa – Mbeya hadi Tunduma ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kupunguza msongamano wa
magari katika mpaka na Zambia pale
Tunduma na pia msongamano wa magari katika Jiji la Mbeya ili kuijenga kwa utaratibu wa PPP.

Ametaja miradi mingine
iliyoainishwa na Wizara kwa ajili ya kutekelezwa kwa utaratibu wa PPP ni
Barabara za Pete Dar es Salaam (Outer
Ring Road – km 78.63 na Middle Ring
Road – km 53.31), Daraja la Pili la Kigamboni (Magogoni –Kivukoni) na Barabara ya Himo – Moshi – Arusha
(Tengeru – km 78).