January 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kushirikiana na wadau kukabiliana na changamoto ya afya ya akili


Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online


Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kushirikiana na wadau mbali mbali kukabiliana na changamoto ya afya ya akili ambayo inawakumba watanzania wengi kwasasa hususan kwenye maeneo ya kazi.

Mpango huo wa serikali umewekwa wazi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Prof. Joyce Ndalichako, alipokuwa akiwahutubia wanamichezo walioshiriki katika Bonanza la Waajiri lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) na kufanyika katika Viwanja vya Leaders jijini Dar es Salaam.

Amesema serikali itaendelea kushirikiana kikamilifu na wadau kuweka mipango ya kisera na kuimarisha miundombinu ya utoaji huduma kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kujenga vituo vya afya nchi nzima na kuongeza watalam wa afya ya akili kwenye vituo hivyo.

“Ninafahamu licha ya uwepo wa changamoto ya afya ya akili, wafanyakazi katika maeneo yao ya kazi wamekuwa wakikabiliwa na tishio la magonjwa yasiyoambukiza kama vile, saratani, magonjwa ya moyo na kisukari. Magonjwa haya kwa kiasi kikubwa yamekuwa yanasababishwa na mtindo wa maisha tunayoishi sambamba na kutokuwa na tabia ya kufanya mazoezi ya viungo vya miili yetu,” ameeleza Waziri Ndalichako na kuongeza:

“Hivyo niwaombe sana tuwekeze katika afya zetu kwa kufuata mitindo mizuri ya afya ikiwemo kula milo kamili na kufuata ushauri wa wataalamu wetu wa afya. Niwahimize Waajiri kuendelea kuwekeza katika michezo na program mbalimbali zinazojenga tabia ya kufanya mazoezi ya viungo.”

Akimkaribisha Waziri katika tukio hilo, Katibu Mkuu katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhandisi Cyprian Luhemeja, pamoja na kuwapongeza ATE kwa kuandaa Bonanza hilo, amesema:

“Bonanza hili ni changamoto kwetu kama Wizara yenye dhamana ya masuala ya Ajira na Vijana ambapo ndio tulipaswa kuandaa vitu kama hivi hivyo nasi tutakwenda kujipanga na kuona ni kwa namna gani tutaweza kuwa na matukio kama haya kwa lengo la kuwaendeleza vijana katika nchi yetu.”

Akizungumza katika bonanza hilo kwa niaba ya Taasisi chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda, amesema kutokana na ukubwa wa changamoto ya magonjwa yasiyo ambukiza miongoni mwa waajiri na wafanyakazi kwasasa ni wakati mwafaka kwa wadau na serikali kushirikiana katika kushughulikia changamoto hiyo.

“Kwa mujibu wa takwimu tulizozikusanya kwenye maeneo ya kazi kwa mwaka wa fedha 2022/2023 jumla ya wafanyakazi 350,000 walipimwa afya na OSHA ambapo asilimia 40 ya idadi hiyo walikuwa na uzito uliozidi wastani, hali inayowaweka katika hatari ya kupata magonjwa ya kuambukiza ikiwemo kisukari, shinikizo la juu la damu na saratani,” amesema Bi. Mwenda.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba-Doran, amesema ATE wameendelea kushirikiana na OSHA kutoa elimu kwa waajiri kupitia vikao vya wadau kuhusiana na masuala ya usalama na afya ili kuongeza tija katika uzalishaji.

“Bonanza la mwaka huu limebeba Kauli Mbiu ni: “Kuimarisha Afya ya Akili ili Kuongeza Tija Mahali pa Kazi”, lengo ni kuendelea kuhamasisha umuhimu wa kuimarisha afya ya akili mahali pa kazi na kuibua mjadala. Mazingira salama na yenye afya kazini yanapelekea kuwa na wafanyakazi wenye afya njema ambao ndio msingi mkuu wa uzalishaji mahali pa kazi. Kwahiyo sisi tumeendelea kufanya hilo kwa vitendo ambapo hivi karibuni tumeshirikiana na OSHA kufanya vikao 10 vya kisekta kwa lengo la kutoa elimu kwa wadau pamoja na kusikiliza na kutatua changamoto zao kuhusiana na huduma zetu,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa ATE.