November 22, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kupunguza tozo kwa wafanyabiashara

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

NAIBU Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe ametembelea kikundi cha wauzaji wa mchele (Mbeya Rice Group) katika Kongano la wauzaji mchele soko la Mwanjelwa  jijini Mbeya huku akiwaeleza wafanyabiashara wa bidhaa hiyo  kuwa serikali itaendelea kuona na kupunguza tozo zisizo na tija kwao na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo ya Kigahe imekuja kufuatia malalamiko ya wafanyabiashara wa mchele katrika soko hilo la mchele kutozwa tozo nyingi na hivyo kusababisha bidhaa ya mchele kuuzwa kwa bei ghali.

“Naomba niwahakikishie kuwa serikali itandelea kuwaunga mkono katika shughuli zenu na ndiyo maana leo nimekuja nione kazi zenu lakini pia kusikia changamoto zinazokwamisha shughuli zenu ili tuweze kuzifanyia kazi.”amesema Kigahe

Aidha amewataka viongozi wa soko hilo waendelee kuboresha mchele wao ili kuhakikisha unakuwa ni bidhaa bora ambayo inaweza kushindanishwa katika soko la Kimataifa.

BAADHI ya wafanyabiashara na wafanyakazi katika viwanda vya kuchakata mpunga katika soko la Mwanjela jijini Mbeya

“Naomba mjitahidi sana katika uandaaji wa mpunga wakati mnapoelekea kuuchakata ili kupata mchele,hakikisheni mnaanika vizuri mahali ambapo hapawezi kusababisha mchele kuwa na mchanga lakini pia mtafute mashine ambayo inayoweza kupumbua mchele na chenga,lengo kubwa hapa ni kifaya bidhaa yetu ishindane kimataifa.”amesema Kigahe

Aidha amesema,Serikali inaendelea kuongea na taasisi za kifedha na hasa kwenye vikundi ili wafanyabaishara hao waweze kukopesheka na benki mbalimbali ikiwemo b enki ya TIB.

“TIB wana fedha za kutosha na wanalenga vikundi vilivyopo  kwenye sekta hii ya kilimo na riba yao haizidi asilimia nane ,na mngekuwa na SACCOs yenu mngekopa kwa asilimia nne mpaka tano ,sasa hii ingewawezesha kupata mitaji na hivyo kupata teknolojia mnazozihitaji kutoka katika kiwanda cha SIDO.

Ametumia nafasi hiyo kuitaka SIDO iwapeleke  TIB kuwatambulisha kwamba ni kikundi chenye tija katika uchumi wa nchi  ili waaminike na kuwawezesha kupata  mitaji na huduma nyingine  zitakazosaidia kuboresha biashara zao.

Vile Vileameielekeza SIDO iwasaidie kutengeneza teknolojia wananzohitaji kwa gharama nafuu au iwaunganishe na sehemu ambako ni sahihi ili waweze kupata hizo teknolojia

“Kwa hiyo mimi niseme sisi tutaendelea kuwasaidia,kuwatengenezea mazingira mazuri  zaidi ili mzalishe kwa tija .”

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Exaud Kigahe akiangalia moja ya mashine ya kuchakata mchele zinazomilikiwa na Mbeya Rice Group katika soko la Mwanjelwa jijini Mbeya .

Kuhusiana na suala la ushuru mkubwa lililolalamikiwa na wafanyabiashara hao,Naibu Waziri huyo ameiagiza Ofisi ya Katibu Tawala wa mkoa ilichukue hilo na waone namna ya kuangalia kupunguza ushuru ili waweze kuchukua wafanyabiashara wengi zaidi na kupata fedha nyingi licha ya kukusanya kidogo kidogo lakini  itaongeza uhiyari wa kulipa kodi na hivyo serikali kupata mapato mengi zaidi.

“Kwa hiyo nadhani hili tuliangalie kama serikali na hasa wenzetu wa halmashauri mtusaidie, kwa hiyo mtaangalia maeneo ya kodi na vibali mbalimbali wanapoenda kununua mazao kwa wakulima.”amesisitiza

Awali Katibu Mkuu wa Mbeya Rice Group Julius Ngalawa amesema,lichaya changamoto wanazokumbana nazo lakini wameendelea na biashara hiyo ambayo imeajiri zaidi ya watu 3000.

“Mbeya Rice Group,tunachakata tani 78,000 za mpunga.. ,na inashughulika na mnyororo wa thamani wa zao la mpunga wanaanza kwa mkulima mpaka kwa mlaji ,tuna vikundi vya wakulima katika maeneo mbalimbali tunafanya mikataba nao na pia tuna wakulima mmoja mmoja ambao ni binafsi wanakuja kukoboa,

“Pia Mbeya Rice Group tuna watu zaidi ya 3000 tunaofanya nao kazi ambao tumewaweka katika vikundi,kuna vikundi vya washushaji ,wabeba mchele,usaidizi mashineni,pia kuna wananwake wapatao wanane  wanaomiliki mitambo ya kukobolea mpunga.”

Aidha amesema ,kikundi hicho kinajishughulisha na uuzaji wa mchele nje ya nchi ambapo amesema biashara bado haiajwa rasmi lakini mpango wao ni kuhakikisha biashara hiyo inakuwa rasmi ili waweze kulipa kodi za serikali maslahi mapana ya nchi.

Amesema masoko ya mchele wanaouzalisha yapo katika nchi za Uganda,Zambia ,Botswana ,kwa hiyo Mbeya Rice Group tukajiongeza tukaona ni nafuu sasa tuwe na sehemu ambayo ni Packaging process ambayo tutakuwa tutatoa mchele katika mashine zetu tunauweka sehemu tunafanya ‘packaging’ tunaukatia vibali na kuusafirisha kwa njia halali ili serikali na wananchi kwa ujumla kila mmoja apate pato lake.

Kwa mujibu wa Ngalawa kikundi hicho kimeingia makubaliano na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia COSTECH ambapo walifanikiwa kupata wazo bunifu la mashine ya kukaushia mpunga na wamepata milioni 40 kutoka COSTECH kwa ajii ya kutengenezewa mashine ya kukaushia mpunga ambayo itakuwa ni suluhisho la ukaushaji wa mpunga na kutoa bidhaa bora ya mchele.

Kwa upande wake mfanyabiashara wa Mchele Joyce Mahenge amemuomba Naibu Waziri huyo awasaidie katika kupunguza utiriri wa kodi unaosababisha kuleta kero kwao na mchele kuuzwa kwa bei ghali.