November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali kujenga shule za sekondari 1,026 katika kipindi cha miaka mitano

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

SERIKALI imesema imeweka umuhimu katika umarishaji wa miundombinu ya elimu sekondari ambapo kupitia mradi wa Elimu wa SEQUIP  inatarajia kujenga shule 1,026 nchini katika kipindi cha miaka mitano 2021/22-2024/25 .

Akizungumza wakati akifunga Mkutano wa Mwaka wa wadau katika sekta ya Elimu uliofanyika Disemba 6 na 7 jijini Dodoma , Naibu Katibu Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Elimu Dkt.Charles Msonde amesema,kazi hiyo tayari imeanza katika mwaka wa fedha wa wa 2021/22 ambapo shule 232 za kata zinajengwa ili kuwapunguzia  wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule.

Aidha amesema, katika mwaka huo wa fedha serikali imetoa biloni 3 kila mkoa kwa ajili ujenzi wa wa shule za wasichana za mikoa .

“Ni  malengo ya serikali kuhakikisha kwamba katika miaka mitano ijayo shule hizi 1,026 ziweze kujengwa nchini na mwaka huu wa fedha serikali inategemea kujenga shule za aina hiyo 184 ambapo shule moja itajengwa katika Halmashauri hapa nchini.”amesema Dkt.Msonde

Vile vie ameeleza mikakati mingine ya Serikali ni pamoja na kurekebisha iundombinu katika shule za msingi na sekondari ikiwa ni pamoja na kurekebisha majengo yaliyochakaa au kubomoa na kujenga upya.

“Tunafahamu kwamba kupitia mafanikio ya elimu bila malipo kumekuwa na ongezeko kubwa katika uandikishaji wa wanafunzi katika shule za msingi na kidato cha kwanza katika shule za sekondari ,hii imesababisha uwepo wa wanafunzi wengi madarasani ,lakini Serikali imeamua kwa makusudi kupitia mradi wa ‘Boost’ katika miaka mitano ijayo kuanzia mwaka huu kuhakikisha kwamba  hali hii inaondoshwa.”amesisitiza

Dkt.Msonde amesema,tayari tathimini imeshafanyika katika shule zote zaidi ya 17,000 za serikali nchini ambapo shule zimefanyiwa tahimni za aina mbili ikiwemo uchakavu wa majengo ambapo hivi sasa kila shule inajulikana ina uhitjai gani.

“Katika eneo hilo tunafahamu kwamba zipo shule zinazohitaji ukarabati na nyingine zinahitaji kubomolewa ,zipo zinazohitaji kujengwa upya ama kufanyiwa ukarabati mkubwa na nyingine ukarabat mdogo ambapo katika shule zaidi ya 17,000 ,zaidi ya shule 7,000 zinahitaji ukarabati mkubwa .”amesema

Amesema tathimini ya pili ni kuangalia msongamano wa wananfunzi katika shule hapa nchini ambapo serikali imebaini kuna shule ambazo zina msongamano mkubwa sana darasani na kufuatia tathimini hiyo kuanzia mwaka huu wa fedha serikali inategemea kuongeza ujenzi wa madarasa na kujenga shule mpya zenye madarasa zaidi ya 9,000 .

Kwa mujibu wa Dkt.Msonde katika miaka ijayo ukarabati na ujenzi wa shule mpya utaendelea ukilenga kupunguza msongamano wa wanafunzi darasani ili waweze kujifunza kwenye  kwenye mazingira mazuri.

Amesema,maboresho yote hayo pia yanategemea maoni ya wadau hao wa elimu huku akisema maoni wanayoyatoa  ,Serikali inakwenda kuyafanyia kazi vizuri ili kuhakikisha kwamba mifumo ya elimu inaboreshwa.